Saturday, November 4, 2017

WANAFUNZI WATAKIWA KUTUMIA MITANDAO KUPATA MAARIFA

Wanafunzi wa Chuo cha Kodi (ITA) jijini Dar es Salaam, wametakiwa kutumia vyema teknolojia ya mawasiliano hususan mitandao ya kijamii kujifunza ili kupata maarifa badala ya kuitumia kwa mambo ambayo hayatawasaidia katika masomo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo wakati akiwakaribisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na chuo hicho kwa mwaka wa masomo 2017/18.Amesema vijana wengi wanatumia mitandao ya kijamii kwa masuala ya kijamii kwa kiwango kikubwa kuliko kuitumia kujifunza na kupata maarifa kwa mambo ambayo yatawasaidia kukuza kiwango cha elimu.

“Elimu ipo kila mahali siku hizi: katika vitabu, mitandao na tuna mambo mengi ambayo yanasaidia sana kujifunza tofauti na ilvyokuwa miaka 30 iliyopita. Ni wajibu wa wanafunzi kuitumia vyema mitandao hususan simu kujifunza na kupata maarifa”, alisema Prof. Jairo.

Mkuu huyo wa chuo amesema kwamba chuo cha kodi kinatumia mfumo wa kujenga umahiri kwa mwanafunzi ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu na ambao umelenga kumuwezesha mwanafunzi kujifunza badala ya kufundishwa. Ameongeza kwamba mfumo huo ndio utaratibu unaotumika ulimwenguni ili mwanafunzi anapohitimu awe na uwezo wa kujua nini cha kufanya katika fani yake na kwa Chuo cha Kodi ajue jinsi ya kukusanya kodi.

“Msije mkakaa mkategemea mtafundishwa tu na mtakaa na kumsikiliza mwalimu, hapana, tunawatarajia mjifunze kwa kutumia nyenzo mbalimbali zilizopo”, amesema Prof. Jairo na kuongeza kwamba huo ndio utaratibu unaotumika katika mfumo wa kujenga umahiri kwa mwanafunzi.

Katika hatua nyingine amewataka wanafunzi hao wa Astashahada ya Uwakala wa Forodha ya Afrika Mashariki, Shahada ya Usimamizi wa Forodha na Kodi na Stashada ya Uzamili ya Kodi, kuzingatia masomo kwani ndio lengo lao kuu la kuomba kujiunga na chuo cha kodi na kwa upande wake chuo cha Kodi kitatimiza wajibu wake kuhakikisha wanapata elimu wanayostahili na katika mazingira bora.

Aidha amewahakikishia wanafunzi hao kwamba wale watakaofaulu vizuri watapata ajira kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania kwani TRA huchukua wanafunzi waliofaulu kwa kiwango cha juu.Kuhusu maisha katika Chuo cha Kodi, Prof. Jairo amewataka wanafunzi hao kuishi kwa mujibu wa sheria za nchi pamoja na kufuata sheria ndogo ndogo na taratibu za chuo.

Pamoja na Mkuu wa Chuo cha Kodi, katika kuwakaribisha wanafunzi hao, pia walikuwepo Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma Justin Musa, Kaimu Mkuu wa Chuo, Utawala Emmanuel Masalu, Mkuu wa Huduma za Fedha Emmanuel Foya, Makamu wa Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo cha Kodi (ITASO) Darafu Abdalah, Wakuu wa vitengo mbalimbali pamoja na walimu.
Wanafunzi wapya katika Chuo cha Kodi wakifuatilia kwa makini maelezo ya Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo 
Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo (aliyesimama) akizungumza na wanafunzi wapya waliojiunga na Chuo hicho kwa muhula wa masomo wa kuanzia 2017/18. Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Huduma za Fedha Emmanuel Foya na Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Utawala, Fedha na Mipango Emmanuel Masalu. (Imeandaliwa na Robert Okanda Blogs) 
Wanafunzi wapya katika Chuo cha Kodi wakifuatilia kwa makini maelezo ya Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo 
Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo akisisitiza jambo kwa wanafunzi wapya waliojiunga na Chuo hicho kwa muhula wa masomo unaoanza 2017/18. Kushoto kwake ni Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Utawala, Fedha na Mipango Emmanuel Masalu na Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Justin Musa. 
Mmoja wa wananfunzi akiuliza swali wakati wa tujio la kuwakaribisha wanafunzi wapya katika Chuo cha Kodi (ITA) 
Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Utawala, Fedha na Mipango Emmanuel Masalu (Aliyesimama) akiwaeleza wanafunzi wapya katika Chuo cha Kodi masuala ya Utawala katika chuo hicho. Pamoja naye kutoka kulia ni Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Justin Musa, Mkuu wa masuala ya Fedha Emmanuel Foya na Makamu Mwenyekiti wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Kodi (ITASO) Darafu Abdalal .

No comments:

Post a Comment