Saturday, November 25, 2017

UCHAGUZI WA MADIWANI KATA 43 NEC YASISITIZA AMANI NA USALAMA UCHAGUZI MDOGO WA MADIWANI

Na Clarence Nanyaro – NEC 

ARUSHA.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya Siasa na wadau mbalimbali wa Uchaguzi kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mdogo wa Madiwani utakaofanyika kesho (Jumapili) Novemba 22, 2017 unafanyika kwa amani na Utulivu na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga Kura.

Akisoma risala kwa umma leo Jijini Arusha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage amesema kuwa Wapiga Kura wapatao 333,309 wanatarajiwa kupiga Kura kuwachagua Madiwani katika Kata 43 za Tanzania Bara na kuongeza kuwa uchaguzi huo utafanyika katika Vituo 884 vya Uchaguzi ambako ndipo Wapiga kura walijiandikishia kupiga kura katika Uchgauzi Mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015.

Amesema kuwa tofauti na Chaguzi zilizopita,Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuzingatia masharti ya sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa kifungu cha 62 imewaruhusu wapiga kura ambao ama kadi zao za kupigia kura zimepotea au kuchakaa au kufutika kutumia vitambulisho mbadala kwenda katika vituo walivyojiandikisha ili waweze kupiga kura katika uchaguzi huu.

Jaji Kaijage amesisitiza kuwa masharti ya Mpiga Kura kuruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala yatazingatia sharti la kwamba majina ya mpiga kura lazima yafanane kwa herufi na majina yaliyoko katika kitambulisho mbadala ambayo yako katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

Ameeleza kuwa katika kutekeleza hatua hiyo,vitambulisho mbadala ambavyo Tume ya Taifa ya uchaguzi imeruhusu vitumiwe na Wapiga kura katika uchaguzi mdogo wa Udiwani ni leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia kinachotolewa na Mamlaka ya utambulisho nchini (NIDA), pamoja na pasi ya Kusafiria

Aidha,katika risala hiyo Jaji Kaijage amewataka Wasimamizi na Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi katika vituo vya kupigia kura kutoa kipaumbele kwa makundi maalum wakati wa kupiga kura. Aliyataja makundi hayo kuwa ni Wenye ulemavu wa aina mbalimbali, Wajawazito, Wenye watoto wachanga, Wazee na Wagonjwa.

Kuhusu Mawakala wa vyama vya siasa katika vituo vya Kupigia kura,Jaji Kaijage aliwasihi kufuata na kuzingatia,sheria Kanuni na taratibu zinazoongoza Uchaguzi katika kipindi chote cha Kupiga,Kuhesabu na kujumlisha kura vituoni.

Aidha, Jaji Kaijage, amewataka Wananchi,wapenzi na Wakereketwa wa vyama kutofanya kampeni ya aina yeyote katika siku ya upigaji kura ikiwemo kusambaza Vipeperushi, kuwa na bendera za Vyama vyao, na mavazi na kuwataka wananchi kueshimu sheria za nchi wakati wote wa upigaji Kura,kuhesabu na kujumlisha kura.

Katika Uchaguzi huu mdogo unaofanyika leo,Mkoa wa Arusha unaongoza kwa kuwa na Kata Nane ambazo zinafanya Uchaguzi huo. Kata hizo ni Ambureni,Makiba Maroroni, Leguruki na Ngabobo katika Halmashauri ya Meru,Kata ya Musa katika Halmashauri ya Arusha, Kata ya Muriet katika Jiji la Arusha na Kata ya Moita katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.

Uchaguzi huu ni wa Pili tangu kuanza kwa Mwaka huu,ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatakiwa kufanya Uchaguzi wa Madiwani mara mbili kwa Mwaka kwa Mujibu wa sheria. Uchaguzi mdogo mwingine wa Ubunge na Udiwani ulifanyika Januari 22, 2017.

No comments:

Post a Comment