Wednesday, November 29, 2017

TPDC laendesha zoezi la Upimaji Afya kwa Wananchi wa Songo Songo

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuanzia tarehe 24/11/2017 hadi 25/11/2017 limeendesha zaoezi la upimaji wa magonjwa mbalimbali kwa wananchi wa Songo Songo ambao wamekuwa wakilazimika kusafiri zaidi ya masaa mawili kufuata huduma ya vipimo hivyo katika Hospitali ya Kilwa kivinje.

Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni Tanzu ya TPDC inayosimamia uendesheshaji na utunzaji wa Miundombinu ya Uchakataji na Usafirishaji wa Gesi Asilia inayoitwa GAS COMPANY (GASCO) Mhandisi Baltazari Mrosso wakati wa ufungaji wa zoezi hilo ameeleza kuwa ni wajibu wao kama Shirika kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii zenye lengo la kuboresha maisha ya Wananchi wa Songo Songo ambao pia ni tegemeo kubwa katika shughuli zinazofanywa na Shirika kuanzia kwenye uzalishaji wa gesi visimani, uchakataji kiwandani na usafirishaji.
Diwani wa Kata ya Songo Songo Mh. Said Mwinyi akifungua rasmi zoezi la upimaji kwa kukipatiwa huduma ya upimaji wa Shinikizo la Damu kutoka kwa Daktari Octavian Modest.

“Sisi kama Shirika la Umma ambalo limewekeza katika Kisiwa hiki katika shughuli za uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia tunao wajibu wa kushirikiana na wananchi pamoja na uongozi wa Songo Songo ili kuboresha maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, kuboresha uhusiano na kuendelea vyema na shughuli za uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia na hivyo leo hii tunahitimisha zoezi la upimaji wa afya kwa wananchi wa Songo Songo pamoja na kukabidhi vifaa tiba vya upimaji wa ugonjwa wa Kisukari ambavyo hapo awali havikuwepo.” Alieleza Kaimu Meneja Mkuu GASCO.
Daktari wa TPDC, Octavian Modest akimtibu moja ya Wazee wa Kijiji cha Songo Songo waliojitokeza katika zoezi la upimaji wa Afya liloratibiwa na kufadhiliwa na TPDC.

Mhandisi Mrosso aliongezea kuwa utaratibu huu wa upimaji wa Afya ni endelevu na utakuwa unafanyika mara kwa mara pamoja na kuchangia kwenye ununuzi wa vifaa tiba mbavyo vinasabisha usufumbufu kwa wananchi wa Songo Songo kusafiri baharini kwa mwendo wa zaidi wa masaa mawili kufuata huduma za vipimo na tiba mbalimbali katika Hospitali ya Kilwa Kivinje pamoja na hayo alimuomba Mh. Diwani wa Kata ya Songo Songo kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuhamasisha Wananchi kuondoa woga wa kupima afya zao.
Wahudumu wa Afya wakimsaidia Mmoja wa Wazee waliojitokeza kupima afya zao katika Zahanati ya Songo Songo.

Aidha Mh. Diwani ndugu Mh. Said Mwinyi wa Kata ya Songo Songo ameonyesha kufurahishwa na kitendo cha TPDC kutekeleza zoezi hilo kwa wananchi wa Songo Songo ambalo limeonyesha utayari wa TPDC katika kuhakikisha Kijiji cha Songo Songo kinaimarika katika Sekta ya Afya.

“Kwakweli TPDC mmetupenda wana Songo Songo kwa kutupatia huduma hii muhimu kwa ajili ya kujua afya zetu kitendo ambacho kinamuwezesha kila mmoja kujitambua hali yake, kujikinga na kujitunza na maradhi mbalimbali pamoja na kupata tiba sahihi kulingana na tatizo lililogundulika kama hali halisi ilivyo bado tuna upungufu wa vifaa tiba na leo tunshukuru TPDC kutupatia vifaa vya kupima ugonjwa wa Kisukari ambavyo hatujawahi kuwa navyo na tunaamini vingine hapo mbeleni mtatuletea ili kuhakikisha nasi ndugu zenu tunapata huduma bora ya afya” alieleza Mh. Diwani.
Baadhi ya Wananchi wa Songo Songo wakiwa kwenye foleni ya kusubiri kufanyiwa vipimo vya magonjwa mbalimbali katika Zahanati ya Kijiji cha Songo Songo Mkoani Lindi.

Aidha wakati wa ufunguzi wa huduma hiyo, akieleza nia ya zoezi hilo muhimu kwa wananchi, Meneja Mawaasiliano wa TPDC, Marie Msellemu amesema upo umihimu mkubwa wa kila Mtanzania kujua afya yake ili aweze kujikinga na maradhi mbalimbali, kudhibiti madhara ya maradhi aliyonayo, kuimairisha afya zetu na kuweza kulitumikia taifa kikamilifu.

“Sisi kama TPDC tunaona ni wajibu wetu kuhakikisha ndugu zetu wa Songo Songo ambao eneo lao ndilo gesi iligundulika kwa mara ya kwanza wanapata fursa ya kupima na kutambua afya zao ili waweze kuwa na nguvu na afya bora na hivyo kuwawezesha kutekeleza shughuli zao za kila siku na ndio maana TPDC tumeamua kuendesha zoezi hili muhimu kwa wananchi wa Songo Songo” Alieleza Bi. Msellemu.

Zoezi la upimaji wa Afya liliambatana na mashindano ya mpira wa miguu, mpira wa pete na utoaji wa hundi ya Shilingi 4,613,100 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mwalimu wa Shule ya sekondari ya Songo Songo.

No comments:

Post a Comment