Sunday, November 5, 2017

DC URAMBO: WAKULIMA 4,268 WAJIANDIKISHA KULIMA PAMBA MSIMU UJAO.

NA TIGANYA VINCENT-RS –TABORA

JUMLA ya wakulima 4,268 wilayani Urambo wamejiandikisha kulima zao la Pamba katika msimu wa kilimo unatarajia kuanza wakati wowote mwezi huu.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Urambo Angelina Kwingwa wakati akitoa taarifa ya maandalizi ya kilimo hocho kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey ambaye anazungukia vijiji mbalimbali vinavyolima pamba kwa ajili ya utoaji wa elimu juu ya ulimaji bora.Alisema kuwa idadi ya wakulima wanatoka Kata 15 ambao wamo katika vijiji 49 wameleta makisio yao ya kulima zao hilo na kuongeza wakifanikiwa kulima zinaweza kupatika zaidi tani 2000.

Kwingwa alisema kuwa maandalizi yanakwenda vizuri ambapo wanatarajia kupata mbegu ambazo zimependekezwa na Bodi ya Pamba zisizokuwa na Manyoa tani 31.2 kwa ajili ya kusambaza kwa wakulima kwa ajili ya kuanza kilimo hicho.Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mwanri aliwaonya wakulima na wafanyabiashara kutoingiza mbegu za manyoya ambazo zimepigwa marufuku na kuongeza kuwa mkulima atakayepanda mbegu hizo atalazika kuzing’oa.

“Hapa mbegu tutakayopanda ni UKM08 na sio nyingine …nikikutana mtu amepanda mbegu iliyopigwa marufuku ya manyoa nitavuruga shamba lake na kuwachukulia hatua watu ambao watakuwa wamebainika kuingiza mbegu hiyo” alisisitiza Mwanri.

Alisema kuwa wakulima wanatakiwa kuzingatia ushari wa kitaalamu ikiwemo umbali kutoka shimo moja hadi jingine na mstari moja hadi mwingine ili waweze kuwa na idadi ya miche inayotakiwa na 20,000 hadi 22,000 katika ekari moja.

Mwanri alisema kuwa idadi hiyo itawawezesha wakulima kupata kilo kuanzia 1000 hadi 1200 kwa ekari moja ambapo itakuwa ni zaidi ya zile walizokuwa wakipata za 250 hadi 300 wakati wakilima bila kutumia utaalamu na mbegu bora.Aliongeza kuwa mtu yoyote atakayetaka kulima zao hilo ni vema akazingatia Sheria na taratibu zinazoongoza zao hilo ili asije akajikuta katika matatizo ya kushitakiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora  yuko katika ziara maalumu ya kutembelea maeneo yote yanayolima zao la pamba kutoka wilaya za igunga, Nzega, Uyui, Kaliua na Urambo kwa lengo la kuwahamasisha watu washiriki kilimo hicho na vile vile kutoa elimu juu ya kilimo bora kitakacho wasaidia kuzalisha mazao mengi na ya ziada.

No comments:

Post a Comment