Saturday, November 4, 2017

DC SHINYANGA AKUTANA NA WAKULIMA WA PAMBA SHINYANGA VIJIJINI KUHAMASISHA KILIMO CHA KISASA

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro leo Ijumaa Novemba 3,2017 amewatembelea wakulima wa zao la pamba katika kijiji cha Sayu kata ya Pandagichiza halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kuwahamasisha kulima zao hilo kwa njia za kitaalamu/kisasa ili kilimo hicho kiwe na tija kwa ajili ya kujikomboa kiuchumi.

Akizungumza katika kikao na wananchi wa kijiji hicho ambacho ni maarufu kwa kilimo cha pamba,Matiro aliyekuwa ameambatana na wataalamu wa zao la pamba,aliwataka wakulima wa zao hilo wilayani humo kulima kisasa kwa kufuata kanuni 10 za kilimo ikiwemo kulima kwa kutumia kamba.

Alisema wananchi katika wilaya hiyo wamekuwa mstari wa mbele katika kulima zao la pamba lakini wamekuwa hawapati faida kutokana na kulima njia zisizo za kitaalamu.

“Tunataka kufanya kilimo biashara ili kiwe na tija,hatupati mazao ya kutosha kutokana na kutolima kitaalamu,naomba mwaka huu tuwasikilize wataalamu wetu wanatuambia nini,nataka tubadilishe maisha yetu kupitia pamba”,alisema Matiro.

Aliwashauri wananchi ambao hawana uwezo wa kunua mbegu za pamba wajiorodheshe majina yao,ijulikane wapo wangapi na wanahitaji mbegu kiasi gani ili serikali ya wilaya hiyo ione namna ya kuwasaidia ili waweze kulima kisasa.

“Tutaongea na wadau wa pamba ili tujue tunafanya nini,sasa hivi tunaingia katika msimu wa pamba,hatutaki pamba yetu kufanyiwa mambo yaliyokuwa yanafanyika huko nyuma,tunataka tuwe na chama cha ushirika ili hata tukiamua kuwapa mbegu wale walioshindwa waweze kupata kupitia chama chao cha ushirika”,alieleza Matiro.

“Kijiji hiki kinasifika kwa kilimo cha pamba na mazao mengine kama choroko na dengu,naomba mujitahidi kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo lakini msisahau kulima mazao ya chakula na muepuke kuuza chakula chote”,alieleza.

“Serikali haina shamba,jitahidini mnapolima mazao ya biashara limeni pia mazao ya chakula na mhakikishe mazao yale mnahifadhi kwa ajili ya chakula cha baadae”,aliongeza.

Aidha aliwahamasisha wananchi hao kupanda miti ili kukabiliana na tishio la jangwa mkoani Shinyanga ambapo kupitia kampeni ya Shinyanga Mpya,Mti Kwanza kila kaya inatakiwa kupanda miti kuanzia mitatu.

Katika hatua nyingine aliwataka wataalamu wa kilimo kukaa na wakulima na kuwashauri njia nzuri za kufuata katika kilimo.Mmoja wa wakulima katika kijiji hicho,Samwel Nkilijiwa alieleza kuwa tatizo kubwa wanalokabiliana nalo kuwa ni pembejeo ambao dawa za maji zinazotumika kuua wadudu hazijafanyi kazi kama ilivyokuwa kwa dawa za mafuta ambazo sasa hazitumiki.

“Hii dawa ya maji wanayotupa haiui wadudu wanaoshambulia pamba yetu,kwanza inawasha sana huwezi hata kumsogelea mke wako,tunaomba ile dawa ya mafuta tuliyokuwa tunaitumia zamani,hii haifai”,aliongeza Nkilijiwa.

Hata hivyo Mkaguzi wa pamba wilaya ya Shinyanga,Benjamini Madama alisema tatizo la wakulima kulalamikia dawa ya maji inatokana na kipindi cha nyuma wafanyabiashara wa dawa hiyo walikuwa wanachakachua dawa hiyo na kuonekana feki na sasa serikali imechukua hatua hivyo hakuna dawa feki kinachotakiwa wakulima wafutae ushauri wa wataalamu wa pamba.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sayu kata ya Pandagichiza leo akiwahamasisha kufuata njia za kisasa kulima zao la pamba-Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa Sayu
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akisisitiza wananchi kulima mazao ya biashara pamoja na yale ya chakula
Wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga
Mkulima wa Pamba Nicholaus Selena akieleza kero yake kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
Mkulima wa Pamba Samwel Nkilijiwa akieleza changamoto wanayopata pale wanapotumia dawa ya maji ya kuua wadudu ambapo alisema dawa hiyo haiui wadudu hivyo kuomba dawa ya mafuta waliyokuwa wanatumia zamani 
Afisa Kilimo wa wilaya ya Shinyanga Edward Maduhu akitoa ufafanuzi kuhusu kilimo cha pamba
Diwani wa kata ya Pandagichiza Charles Masele Kabogo akizungumza katika kikao hicho
Afisa tawala wa wilaya ya Shinyanga Charles Maugira akizungumza katika kikao hicho
Mkulima wa pamba katika kijiji cha Sayu Ezekiel Nchange akishikana mkono na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro baada ya kumpatia shamba mkuu huyo wa wilaya ili alime zao la pamba katika kijiji hicho
Mkaguzi wa pamba wilaya ya Shinyanga,Benjamini Madama akitoa elimu kwa wakulima wa pamba juu ya njia ya kisasa ya kulima zao hilo
Mkaguzi wa pamba wilaya ya Shinyanga,Benjamini Madama akionesha kamba zinazotakiwa kutumika katika kilimo cha pamba
Kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Sayu Paul Selena akizungumza katika kikao hicho
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akipokelewa katika shule ya msingi Sayu kwa ajili ya kupanda mti
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akipanda mti wa kumbukumbu katika shule ya msingi Sayu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya Shinyanga Mpya Mti Kwanza ambapo wananchi wamekuwa wakihamasishwa kupanda miti ili kukabiliana na hali ya jangwa mkoani Shinyanga
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiendelea na zoezi la kupanda mti katika shule ya msingi Sayu
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Sayu ambapo aliwasisitiza kuwa mabalozi wa upandaji miti katika jamii
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na baadhi ya viongozi na wananchi wa kijiji cha Bulambila kata ya Mwalukwa ambapo pia ni maarufu kwa kilimo cha zao la pamba ambapo pia aliwahamasisha kulima zao hilo kwa njia za kisasa ili lilete tija
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiteta jambo na Diwani wa kata ya Mwalukwa,Ngassa Mboje ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Vijijini.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments:

Post a Comment