Na Ismail Ngayonga,MAELEZO
JIJI
la Dar es Salaama ni miongoni mwa miji inayokua kwa kasi kubwa duniani,
huku ukuaji huo ukiathiri sekta mbali mbali za kijamii na kiuchumi
ikiwemo sekta ya usafirishaji.
Kwa
mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 inakadiria kuwa jiji la
Dar es Salaam lina wakazi milioni 2.4 na kuwa na kiwango cha ongezeko
la idadi ya watu cha asilimia 4.4 kwa mwaka huku ongezeko hilo
likisababisha kujitokeza kwa mapungufu katika utoaji wa huduma
mbalimbali.
Tangu
miaka ya 1990 kumekuwa na mipango mbalimbali ya kuboresha usafiri
katika Jiji la Dar es Salaam ikiwemo kuanzisha barabara za njia moja,
kuanzisha maegesho ya magari ya kulipia, na kuhamasisha kujengwa kwa
majengo yenye maegesho ya magari.
Pamoja
na jitihada za serikali ya jiji la Dar es Salaam na serikali kuu
kuboresha usafiri Jijini humo, bado kuna kero kubwa ya usafiri wa
abiria, hasa wakati wa saa za asubuhi na jioni ambapo ambapo ilimlazimu
mwananchi kuchukua takribani masaa matatu, kwa mfano, kutoka Mbezi Juu
hadi katikati ya jiji.
Katika
kukabiliana na changamoto hiyo, tangu mwaka 2008 Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD)
Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam imekuwa ikitekeleza miradi maalum ya
ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano wa magari katika barabara kuu
za Jijini Dar es Salaam.
Mhandisi
Miradi wa Ofisi ya TANROAD Mkoa wa Dar Es Salaam, Julius Ngusa anasema
mradi wa ujenzi wa barabara za pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam wa
awamu ya tatu ni moja ya mikakati ya Serikali ya kushughulikia tatizo
sugu la msongamano wa magari katika Jiji hilo ambapo utekelezaji wake
ulianza tangu wa mwaka wa fedha 2008/2009.
Anasema
kupitia mradi huo, Serikali ilichagua barabara tisa kwa ajili ya
kujengwa katika kiwango cha lami ikiwemo barabara ya Ubungo Bus
Terminal-Kigogo-Kawawa (6.4 km), barabara ya Jet Corner-Vituka-Davis
Corner (km 12), barabara ya Kinyerezi-Kifuru-Msigani-Mbezi mwisho (10
km), Tanki bovu-Goba (9.0 km), Kimara baruti-Msewe-Changanyikeni (2.6
km).
Anazitaja
barabara nyingine kuwa ni pamoja na Tegeta Kibaoni-Wazo
Hill-Goba-Mbezi/Morogoro (km 20) , Kigogo Round about-Jangwani-Twiga
katika bonde la msimbazi (km 2.72), Tabata Dampo-Kigogo na Ubungo
Maziwa- Mabibo External (Mandela) (2.25 km).
Mhandisi
Ngusa anasema miradi hiyo inajengwa katika awamu tatu za utekelezaji,
ambapo hadi sasa awamu ya kwanza ya miradi hiyo iliyohusisha ujenzi wa
barabara zenye jumla ya kilometa 19.42 tayari imekwishatekelezwa na
kukamilika tangu mwaka 2008.
Anaitaja
miradi iliyokamilika ni pamoja na barabara ya Ubungo-Kigogo-Kawawa
iliyokamilika mwaka 2010 kwa gharama ya Tsh. Bilioni 11.44, barabara ya
Kigogo-Msimbazi-Jangwani iligharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 7.64 ambayo
ilikamilika mwaka 2017 pamoja na barabara ya Jet Corner-Vituka-Devis
Corner iliyokamilika mwaka 2011.
“Kuhusu
Awamu ya pili yenye urefu wa kilometa 27.5 na ujenzi wa daraja la
Kinyerezi lenye urefu wa mita 40, ujenzi wake ulianza mwaka 2014 ambapo
hadi sasa kazi za ujenzi zilizokamilika kwa kiwango cha lami ni pamoja
na barabara ya Tangi Bovu (Samaki Wabichi)-Goba km 9 ilikamilika mwaka
2016 kugharimu kiasi Tsh. Bilioni 8.6 ” anasema Ngusa.
Kwa
mujibu wa Ngusa anasema pia katika awamu hiyo mwaka 2016 Serikali pia
ilikamilisha ujenzi wa Barabara ya Tegeta Kibaoni-Wazo Hill-Goba-Mbezi
Mwisho (km 20), kwa gharama ya Tsh. Bilioni 6.7.
Akifafanua
zaidi Ngusa anasema miradi mingine iliyokamilika ni pamoja na Barabara
ya kilungule (Maji Chumvi)- External/Mandela km 3.3, ambapo mradi huo
ulikamilika mwaka 2015 kwa gharama ya Tsh. Bilioni 4.4.
Aidha
Ngusa anasema mradi wa barabara ya kimara baruti-msewe (km 2.6)
uliopaswa kukamilika mwak 2016, umeshindishwa kukamilika kwa wakati
kutokana na kutokuwepo kwa nafasi ya kujenga barabara, ambapo hata hivyo
hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2017 mradi huo umefikiaa asilimia 80
ya utekelezaji wake.
Mhandisi
Ngusa anasema awamu ya tatu ya utekelezaji wa miradi hiyo ulioanza
kutekelezwa mwaka 2016 na 2017 unahusika ujenzi wa barabara za
Kifuru-Msigani, Goba-Makongo na Goba-Madale zenye urefu wa kilometa 14.1
na unatarajia kukamilika mwanzoni na mwishoni mwa mwaka 2018.
“Miradi
ya barabara ya Goba-Madale na Goba-Makongo hadi kufikia Septemba 30,
mwaka huu imekamilika kwa asilimia 50-52 wakati ule wa Kifuru-Msigani
umekamilika kwa asilimia 87, malengo ni kuhakikisha kuwa miradi hii
inakamilika kwa wakati kwa kuzingatia ubora na viwango tulivyojiwekea”
anasema Mhandisi Ngusa.
Anasema
baadhi ya changamoto inayokabili miradi hiyo ni pamoja na baadhi ya
nyumba zinazohitaji fidia, ambapo hata hivyo TANROAD kwa kushikiana na
Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) zimeanza zoezi la
uthamini na malipo yatalipwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI.
Anasema
Serikali pia inaendelea na ujenzi wa barabara za Msongola-Mbande (km
1), ununio-mbweni (km 1), kitunde-kivule (km 3.2), Dege-Gomvu (km 1) na
inatarajia kuanza awamu ya nne ujenzi wa barabara za Msigani-Mbezi
mwisho (km 2) na Makongo-Ardhi (km 5) wakati wowote kutoka sasa
kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
Kukamilika
kwa miradi hii kutasaidia kuongeza tija na ufanisi katika kuchochea
kasi ya maendeleo katika Jiji la Dar es salaam na taifa zima kwa ujumla
hasa tukizingatia zaidi ya 80% ya pato la ndani la Taifa linachangiwa na
Jiji la Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment