Wednesday, September 27, 2017

WAZEE WILAYA YA UBUNGO WAISHUKURU NIDA KWA KUWATHAMINI NA KUWAJALI

Baadhi ya Wazee wa kata ya Manzese wakisubiri huduma ya Usajili katika zoezi la kuwasajili wazee linaloendelea Wilayani humo kwa kuratibiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ofisi ya Wilaya ya Ubungo.
Zoezi la kuwasajili Wazee Kata ya Manzese likiendelea.Katika picha ni mmoja wa wananchi akisubiri kupigwa picha katika moja wapo ya hatia za Usajili na uchukuaji alama za Kibaiolojia.
Ndg. Anthony Mwasiguhu Afisa usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa akiingiz taarifa za Bi. Fatuma kwenye mfumo wa Usajili wakati zoezi la kuwasajili wazee likiendelea Kata ya Manzese. 
Bi. Neema Mbila Afisa Usajili Wilaya ya Ubungo akimsaidia Bi.Fatuma kujisajili wakati wa hatua ya uchukuaji alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki wakati wazoezi la kuwasajili wazee linaloendelea sambamba na usajili wa kadi za Afya kwa Wilaya ya Ubungo.


Wazee wa Kata ya Manzese Wilaya ya Ubungo mkoa wa Dar-es-Salaam wamefurahishwa na kitendo cha serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) kuwapatia fursa maalumu ya kusajiliwa Vitambulisho vya Taifa na wao kutambulika kama Raia sambamba na zoezi linaloendelea sasa la kuwasajili Kadi za Afya mpango ulio chini ya Manispaa ya Ubungo.

Wakizungumza wakati wa Usajili unaoendelea katika kata hiyo ukihusisha ujazaji fomu za maombi ya Vitambulisho, uchukuaji alama za Vidole, picha na Saini za Kielektroniki; wazee hao wamesema hii kwao imekuwa ni fursa ya pekee na kuomba NIDA kuendelea kusogeza huduma hizi kwa wazee waliopo kwenye maeneo mengine nchini.

Mzee Sudi Abdallah Sudi amesema “ Hii ni fursa adhimu sana na tunaomba muendee na moyo huu wa kutujali wazee na kusogeza huduma hii kwa wazee waliopo kwenye Kata zingine kwani itawasaidia wazee. Wazee wengi tunakosa fursa nyingi zikiwemo huduma mbalimbali kutokana na umri wetu mkubwa kwa kushindwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma zilikowekwa”

Kwa mujibu wa Afisa Usajili wilaya ya Ubungo (DRO) Ndugu Abdulrahman Muya ameeleza kuwa NIDA kwa kushirikiana na Manispaa ya Ubungo imefanikiwa mpaka sasa kusajiliwa wazee 500 katika awamu ya kwanza ya Usajili na wataendelea na awamu ya pili lengo likiwa kukamilisha Usajili wa wazee wote wanaoishi katika Wilaya hiyo.

Zoezi la Usajili Vitambulisho vya Taifa mbali na kuendelea katika Ofisi zote za Wilaya katika Mkoa wa Dar-es-salaam, zoezi hilo kwasasa linaendelea nchi nzima kupitia ofisi za NIDA zilizofunguliwa kwenye kila Wilaya nchi nzima.

No comments:

Post a Comment