Wednesday, September 27, 2017

WAFANYABIASHARA SOKO LA ILALA MCHIKICHINI JIJINI DAR ES SALAAM WAPEWA ELIMU YA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA

Mwezeshaji wa kisheria kutoka Shirika la Equality for Growth (EfG), Amina Mussa akitoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa jinsia kwa wafanyabiashara wa Soko la Ilala Mchikichini Dar es Salaam leo. 
Mfanyabiashara Shikei Ngosi, akielezea changamoto zinazotokana na ukatili wa kijinsia katika soko hilo.
Mwezeshaji Khadija Mohamed akitoa elimu ya upingaji wa ukatili wa kijinsia.
Mfanyabiashara, Mussa Ibrahim, akichangia jambo.
Juma Mohamed akichangia jambo.
Mfanyabiashara wa nguo katika soko hilo, Godrey Milonge akielezea changamoto za ukati wa kijinsia katika soko hilo.
Mwezeshaji wa Sheria kutoka Soko la Temeke Stereo, Batuli Mkumbukwa akichangia jambo.
Mwezeshaji Sheria,wa Soko la Kigogo Kisambusa, Mariam Rashid akitoa mafunzo
Mwezeshaji wa Sheria katika Soko la Ilala Mchikichini, Consolata Cleophas akitoa elimu hiyo.
Mfanyabiashara, Johnson Stephano akisoma moja ya kijarida kinachoelezea ukatili huo.
Mafunzo yakiendelea.
Ofisa Mradi wa Mpe Riziki si Matusi kutoka EfG, Suzan Sitha, akiwaeleza jambo wafanyabiashara wa soko hilo kuhusu kukomesha ukatili wa jinsia.



Na Dotto Mwaibale

WAFANYABIASHARA katika Soko la Ilala Mchikichini wamepatiwa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa jinsia masokoni .

Katika hatua nyingine wafanyabiashara wanaume wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia na wanawake wametakiwa kwenda kushitaki ofisi za masoko husika ili sheria ichukue mkondo wake kwa wahusika waweze kujirekebisha.

Mwito huo umetolewa na Mwezeshaji wa Sheria masokoni, Khadija Mohamed kutoka Shirika la Equality for Growth (EfG) wakati wanasheria wa shirika hilo wakitoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wafanyabiashara wa Soko la Ilala Mchikichini Dar es Salaam leo hii.

"Wakina baba mnapofanyiwa vitendo vya kijinsia na wanawake katika masoko msione haya nendeni kushitaki kwa viongozi wa masoko ili watuhumiwa waweze kukamatwa na kujirekebisha" alisema Mohamed.

Mohamed alisema vitendo vya ukatili wa jinsia hawafanyiwi wanawake pekee bali hata wanaume wamekuwa wakifanyiwa lakini wanaona aibu kwenda kushitaki.Mwezeshaji wa Sheria Batuli Mkumbukwa alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia katika soko hilo vimeshamiri hivyo alitoa mwito kwa wafanyabiashara wa soko hilo kuviacha. 

Mkumbukwa alisema ili kumaliza vitendo hivyo kwa makosa madogo madogo kama kutoa lugha ya matusi, kumshika mtu maunoni bila ya ridhaa yake mtuhumiwa amekuwa akipewa adhabu pamoja na kupigwa faini lakini kwa kosa la ubakaji adhabu yake ni kifungo cha maisha au miaka 30.

Mariam Rashid, ambaye ni mwezeshaji wa kisheria kutoka EfG alitaja ukatili wa kijinsia unaofanyika katika masoko ni ukatili wa kingono, uchumi, kisaikolojia na kimwili.Baadhi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vinafanyika katika soko hilo ni pamoja na wafanyabiashara kuwashika sehemu za siri wateja wao wa kike maarufu kama kunawa, kukojoa kwenye chupa za maji na kwenda kuziweka kwenye meza za 

wafanyabiashara, lugha za matusi, kujambisha na kutolipa fedha baada ya kuuziwa chakula na mama lishe.Wafanyabiashara katika soko hilo walisema kuwa kukithiri kwa vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia katika soko hilo kwa namna moja au nyingine vinachangiwa na wanawake wenyewe kutokana na tamaa zao kwa kuvaa nguo fupi na kujilengesha kwa wanaume ili wapate bure bidhaa wanazozitaka.

"Wanawake wanabakwa na kushikwa maungoni kwa kupenda wenyewe wala hawalazimishwi" alisema Juma Mohamed mfanyabiashara.

Ofisa Mradi wa Mpe Riziki si Matusi kutoka EfG, Susan Sitta alisema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwaongezea uelewa wafanyabiashara ili waweze kuacha kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika masoko ili kutoa fursa kwao kufanya biashara zao bila ya kuwa na bugudha.

Alisema mradi huo umefadhiliwa na Shirika la United Nations Trust Fund na kuwa unafanyika katika masoko ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Temeke.

No comments:

Post a Comment