Thursday, September 28, 2017

SERIKALI: KASI YA MENDELEO YA TEKINOLOJIA INATULAZIMU KUFANYA MABORESHO YA MARA KWA MARA YA KANUNI ZETU

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo wakati wa kikao cha wadau wa sekta habari ili kujadili kanuni za maudhui ya utangazaji katika redio na tevelisheni, na kanuni za maudhui mtandaoni kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akifafanua jambo wakati wa kikao cha wadau wa sekta habari ili kujadili kanuni za maudhui ya utangazaji katika redio na tevelisheni, na kanuni za maudhui mtandaoni leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Utangazaji kutoka TCRA, Fred Ntobi, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi James Kilaba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Rodney Thadeus.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Rodney Thadeus akielezea jambo wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya habari ili kujadili kanuni za maudhui ya utangazaji katika redio na tevelisheni, na kanuni za maudhui mtandaoni leo Jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa Kamati ya Maudhui kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka akiwasilisha mada kuhusu kanuni za maudhui ya utangazaji katika redio na tevelisheni, na kanuni za maudhui mtandaoni wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya habari ili kujadili kanuni hizo leo Jijini Dar es Salaam.
Mwanasheria Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Phillip Filikunjombe akiwasilisha mada kuhusu kanuni za maudhui ya utangazaji wa na mitandao wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya utangazaji na mitandao ili kujadili kanuni hizo leo Jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Evodi Kyando akitoa maelezo kuhusu kanuni za maudhui ya utangazaji katika redio na tevelisheni, na kanuni za maudhui mtandaoni wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya utangazaji na mitandao ili kujadili kanuni hizo leo Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (katika) akifuatilia majadiliano ya wawakilishi kutoka vyombo vya habari vya elekroniki na mitandao wakati wa kikao cha kujadili kanuni za maudhui ya utangazaji katika redio na tevelisheni, na kanuni za maudhui mtandaoni leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi James Kilaba.
Mmoja wa washiriki wa kikao cha wadau wa utangazaji na waendeshaji wa mitandao Maria Sarungi Tsese (katikati) akichangia hoja wakati wa kikao cha kujadili kanuni za maudhui ya utangazaji katika redio na televisheni, na kanuni za maudhui mtandaoni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (waliokaa katika) akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa Televisheni na Redio mara baada ya kikao cha kujadili kanuni za maudhui ya utangazaji katika redio na tevelisheni, na kanuni za maudhui mtandaoni leo Jijini Dar es Salaam.

Picha na: Frank Shija – MAELEZO

……………….

Na Pascal Dotto, MAELEZO

Serikali imesema kasi kubwa ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano ambayo imeikumba sekta ya habari inalazimu jamii kufanya maboresho ya mara kwa mara ya Sera na Kanuni ili kuepusha matumizi mabaya ya vyombo vya habari.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel amesema kuwa katika kufanya hivyo ni wajibu wa wadau wote kushirikiana kutumia vyema maendeleo hayo ya tekinolojia kwa ajili ya ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.

Profesa Elisante alisema hayo leo wakati akifungua mkutano wa siku moja wa mashauriano miongoni mwa wadau wa sekta ya habari kuhusu mapendekezo ya Kanuni za maudhui yanayorushwa na vituo vya Utangazaji vya Redio na Televisheni na Kanuni za Maudhui Mtandaoni.

“Ni wajibu wetu kama taifa linalosimamia maadili na ambalo lingependa kudumisha amani na mshikamano, kutunga kanuni ambazo zitahakikisha kuwa kunakuwa na matumizi mazuri, sahihi na salama ya maudhui ya mtandaoni”Profesa Elisante alisisitiza.

Aliwaambia washiriki wa mkutano huo kuwa kuweka kanuni ni suala muhimu na kuwakumbusha matumizi ya mfumo wa habari mtandaoni wakati mwingine umetumika kupotosha jamii, kujenga chuki, kutoa habari za faragha za watu binafsi au habari zilizoleta sintofahamu miongoni mwa jamii.

Aliongeza kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni jambo muhimu kwa kuwa washiriki watapata fursa ya kujadili kanuni hizo ambazo baadhi zinadaiwa kuwa zimepitwa na wakati na pia haziendani na utendaji na kazi katika ushindani wa soko.

Katika mkutano huo ambao Profesa Elisante alikuwa mwenyekiti wake alieleza kuwa pamoja na kuwa bado kumekuwepo na mijadala mikali katika nchi nyingi zikiwemo za Magharibi kuhusu uwekaji kanuni lakini ukweli unabaki kuwa nchi hizo zimeweka sheria na kanuni zinazosimamia matumizi ya intaneti.

“Ni kweli kwamba tekinolojia hii ina changamoto katika usimamizi lakini hakuna uhuru usio na mipaka. Kwa hiyo imekuwa ni wajibu wa kila nchi kutafakari mahitaji na umuhimu wa kutoa miongozo itakayosaidia jamii na taifa” Alieleza Profesa Elisante.

Mapema akimkaribisha Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hassan Abassi aliwaeleza washiriki kuwa Mkutano huo ni muhimu katika historia ya maendeleo ya tasnia ya habari nchini kuwa umelenga kuweka kanuni bora zitakazoratibu tasnia.

“Tumeitana hapa kushauriana kuhusu kanuni hizi hivyo hakuna haja ya kueneza wasiwasi kuwa katika mitandao ya kijamii kuwa serikali imedhamiria kudhibiti vyombo vya habari” Dk. Abbassi aliwaeleza washiriki.

Wakati huo huo, Serikali imeongeza muda wa siku saba kwa wadau wa sekta ya utangazaji na mitandao kuwasilisha maoni yao kuboresha kanuni zilizopendekezwa. Uamuzi huo umefikiwa mwishoni mwa mkutano wa mashauriano kujadili kanuni hizo ambapo wadau wengi waliomba muda zaidi.

Akifunga mkutano huo Profesa Elisante alisema ni vyema wadau wakaitumia fursa hiyo kuwasilisha maoni yao kwa maandishi ili kuboresha kanuni hizo hatimae taifa kuwa na kanuni bora kwa faida ya jamii yote.

Katika maelezo yake kufunga mkutano huo Profesa Elisante aliwashukuru washiriki kwa kutoa maoni yao na kuahidi kuwa serikali itayafanyia kazi maoni hayo.

Alieleza kuwa ni ukweli kuwa vyombo vya habari vinafanya biashara na pia vina wajibu wa kuelimisha jamii hivyo vitu viwili havina budi kwenda sambasamba bila kuathiri upande mwingine.

No comments:

Post a Comment