Tuesday, September 26, 2017

MAKALA MICHEZO - UCHAGUZI WA TFF ULIVYOSAMEHE UWANJA WA MAJIMAJI

Uwanja wa Majimaji Songea.

Na. Honorius Mpangala.

BADO sijafanikiwa kupata majibu na kujua ni nini wanachopewa kamati ya ukaguzi wa viwanja vinavyotumika ligi kuu. Yawezekana kuna mazingira ambayo yanafanyika ili kuweza kuruhusu viwanja kama wa Majimaji Songea kutumika ligi kuu. Januari 2017 katika moja ya makala zangu iliyohusu Viwanja niliandika mengi kuhusu viwanja visivyowatendea haki wachezaji wetu. Na katika hilo moja kwa moja huwezi kupindisha kulielekeza TFF kama wadau namba moja ndipo baadae liende kwa Wamiliki wa Uwanja.

Nashukuru makala ile nilipata ujumbe mwingi wa simu kutoka maeneo mbalimbali. Hatimaye Uwanja wa Namfua uliokuwa kama picha katika makala ile unarekebishwa. Niliandika kuhusu Namfua ikiwa daraja la kwanza na inapambana kupanda ligi kuu. Watu wa Singida kwa namna moja au nyingine naweza kusema walinisoma na walinielewa kwa sababu Uwanja wao ilikuwa sehemu ya kufungia mifugo kama mbuzi na ng'ombe.

 Shirikisho kuendelea kuwaheshimu watazamaji na kuwanyima raha wale wanaotazamwa uwanjani ni jambo linalosikitisha. Hata ikitokea kama tuna malengo makubwa ya kulifanya soka letu lichezwe maeno mengi  ya nchi basi tuna kazi ya kubadili mitazamo ya viongozi wetu kwa kiasi kikubwa. 

Uchaguzi mkuu wa TFF umefanya lile rungu la kufungia viwanja baada ya kukaguliwa lisifanye kazi kwasababu ya hofu ya kupunguza kura. Ikiwa tunaelekea kwenye uchaguzi wa shirikisho vifungo kadhaa vilifunguliwa kwa wale waliofungiwa. Hapo ndipo hali ya kiutendaji kwa wakati ule ilipokuwa ya kusaka kura zaidi kuliko kusimamia kwa weledi mambo ya yanayohusu soka.

Ni aibu kuona uwanja kama wa Majimaji ambao msimu wa tatu mfululizo Tangu timu ilipopanda Mara ya mwisho 2015 kuwa na nyasi zile. Kila msimu kamera za Azam TV zinapokuwa katika uwanja wa huo unasikitika mtazamaji. Viko vibanda umiza ambavyo wamiliki hufikia hatua ya kusema mechi ya Majimaji msilipe kiingilio maana inachezwa Kwenye jaruba lililotoka kuvunwa mpunga hivi punde. Kiuhalisia huwezi kutofautisha kati ya majaruba ya shamba la Nafco Kapunga kule Mbarali Mbeya na eneo la kuchezea la uwanja wa Majimaji. Halafu unakuta chama cha soka eneo hilo kinajinasibu kufanya vyema katika utawala wao. Unaweza kujiukiza maswali mengi kuwa mgawanyo wa mapato kwa wamiliki na chama cha soka yanatumika ipasavyo au ni kama shamba la miwa karibu na shule msingi.

Unapoukaribia uwanja wa Majimaji kwa nje ukiwa mgeni utajisemea moyoni kuwa huu ni uwanja mzuri sana. Mawazo yako yanakufanya uamini hivyo kutokana na mwonekano wake wa nje kwa zile kuta zilivyo safi. Uzio wa uwanja ule haufanani na uwanja wa Kambarage Shinyanga,Nangwamda Sijaona Sokoine,Wala uwanja Ally Hassan Mwinyi. Hii ni kutokana na ujenzi wake chini ya Aliyekuwa mkuu wa mkoa na Mbunge wa Songea Lawrence Mtazama Gama kusimamia vyema ujenzi wa uwanja. Gama aliwafanya wanaruvuma waone wana wajibu wa kujenga uwanja hivyo michango yao ilifanikisha kupatikana uwanja ule. 

Nyakati zote katika maisha maamuzi magumu huumiza upande mmoja kwa muda baadae hali huwa shwari baada ya kuona matunda ya maamuzi hayo hapo nyuma. Ni kipi kinachowafanya bodi ya ligi na shirikisho kushindwa kuufunga uwanja wa Majimaji hadi pale watakaporekebisha eneo la kuchezea?. Wakati huu ni kama hakuna anayeona hali ya viwanja hivyo lakini siku ikifika unaona kamati ina kaa na kupitia taarifa mbalimbali na kufanya maamuzi. Maamuzi hayo yanaweza kutokea baada ya Klabu kubwa ambazo inaaminika hawachezi Manungu kwasababu za kiusalama na badala yake zikacheza Jamhuri morogoro.

Hata kama FIFA wana viwango vyao katika kuuthibisha uwanja wa kutumika katika mshindano mbalimbali. Tujiulize je viwango vya TFF ndo vya kuukubali uwanja kama wa Majimaji kutumika katika ligi kuu. Ni jambo ambalo haliingii akilini kwa mpenzi yeyote wa soka kuona Shirikisho kukubali uwanja kama ule kutumika katika ligi kuu.
Uwanja wa Namfua ukiwa katika marekebisho ya mwisho.

Utaratibu wa ukaguzi wa viwanja uliingiliwa na uchaguzi na wagombea waliokuwa kwenye mfumo waliogopa kukimbiza kura endapo watatoa maamuzi baada ukaguzi kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi. Kama tutakuwa makini na kuhitaji haya mambo kutokutokea ni heri tukawa wakali kwa ukaguzi wakati timu zikiwa daraja la kwanza. Ukaguzi wa kuzingatia uzio unaotenganisha wachezaji na mashabaki pamoja na vyumba vya kubadilishia nguo na sehemu za kujisaidia hakuwezi kuonekana bora na kuufanya uwanja uko vizuri kama eneo la kuchezea litaoneka kama shamba la mpunga japo maeneo yote ni muhimu. Kamera zetu hazimuliki kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wala eneo la vyoo bali zinaelekezwa katika nyasi za uwanja ambapo mashabiki wanatazama soka.

Ifike wakati tusiwatupie mzigo wa lawama wamiliki pekee Bali  vyama vya soka vya mikoa na shirikisho vishikirikiane katika kuboresha maeneo ya kuchezea kwa kila mkoa.Ingefaa sana viwanja vyote wakati ligi itakaposimama kupisha mzunguko wa pili viwanja vyenye uhitaji wa marekebisho vikafungwa na kupisha urekebishaji huo.

Katika soka sheria namba moja ni uwanja na inafafanuliwa vizuri uwanja uanapaswa kuwa wa namna ipi, na hali ya eneo la kuchezewa lisiwe na nini. Ni kama tunaipuuza sheria hiyo katika ufafanuzi wake na badala yake tunajiandaa kupandisha timu sita na kushusha mbili ili kutimiza idadi ya timu ishirini katika ligi yetu.Kuna maana gani kufanya ukaguzi kwa wchezaji katika kujua vifaa wanavyoingia navyo uwanjani katika kutafsiri sheria namba nne, na ukashindwa kutumia sheria namba moja katika kulinda usalama wa wchezaji hao kuepuka kuumia kwasababu ya uwanja.

Yako mambo ambayo yanahitaji akili ya kiuongozi kuweza kuyaweka sana na kufika hatua ya wawekezaji kuvutiwa na uendeshaji wa soka letu. Mipango na maamuzi thabiti ndiyo yanayotoa dhana halisi ya umakini katika usimamizi wa ligi yetu. Umakaini huo hauwezi kuonekana kama tunaruhusu viwanja venye miundombinu mibovu kutumika hata yale makampuni yanayohitaji kuwekeza kwetu yataona umakini wetu ni mdogo sana.

Ripoti ya mwisho wa msimu kwa bodi ni moja ya vitu muhimu sana ambacho kinaweza kuwa chanzo cha kufanyia kazi Yale waliyoyaona yanaukakasi katika msimu mzima. Ripoti hiyo kama ingekuwa inaeleza wazi juu ya utumiaji wa viwanja vya kama Majimaji,Jamhuri Morogoro na vinginevyo ingeweza kusikia kauli ikitoka. Kinachoendelea katika soka letu ni kama wahusika kuongea sana bila utekelezaji. 

Wako watu wenye uchungu na soka letu ambao ushauri wao wanaoutoa kama ungekuwa unafanyiwa kazi basi tungekuwa tunasonga kila wakati. Kitu pekee ambacho unaweza kutofautisha ligi ya sasa na ile ya miaka kumi iliyopita ni ligi kuonekana kwenye TV,na maboresho ya Zawadi kwa washindi lakini hali ya miundombinu imebaki vilevile.

Labda tupeane maarifa kidogo,hivi tulishawahi kujiuliza kwanini Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam alienda na wataalamu waliotengeneza uwanja wa Bandari Tandika hadi katika uwanja Boko Veteran?. Je kuna kiongozi yeyote wa soka amewahi kwenda pale akapata maarifa jinsi uwanja ule ulivyotunzwa. Niliwahi kukatiza katika viwanja vya Gymkhana Dar es salaam nikajiuliza mengi baada ya kuona nyasi walizoweka na jinsi zinavyoonekana. Kujifungia ofisini au eneo moja huwezi kujua ni kipi kinafanyika kwa maendeleo ya soka letu.

Tunahitaji kuwa na viwanja vizuri katika eneo la kuchezea na sio majukwaa. Unapeleka mradi kwenye uwanja wa Nyamagana kwanini zile nyasi zisingewekwa katika uwanja wa CCM kirumba. Baadala yake tunakuja kulaumu soka walilocheza Tanzania dhidi ya Rwanda tukisema uwanja kikwazo. Kwani vikwazo vya viwanja vimeanza Leo nchi hii.

Tunakosa watu wenye mitazamo ya kuufanya umma ukafurahia mawazo yako. Hata kama wapo basi hawako katika mfuko ambao wanaweza kufikiwa moja kwa moja kutokana na kujiamini kwa walioko ofisini.

Upuuzwaji wa miundombinu hakuwezi kutufanya tuonekana tunaendelea kisoka kama akili yetu inabaki kwenye mapato ya mlangoni na tukashindwa kurekebisha hali ya viwanja vyenyewe.Haihitaji akili nyingi labda tukafikiria kuwaleta wataalamu toka nje kwani wako wataalamu wazalendo wanaweza kuwa msaada mkubwa. 

Tufike uwanja wa sikoine tupate maelekezo ya mtaalamu aliyesimamia mradi wa urekebishwaji wa eneo la kuchezea. Tufike Boko veterani na hata Gymkhana Dar lazima tutakuwa tumepata maarifa yatakayokuwa msaada kwa viwanja vyetu kuanzia ligi za ngazi za chini.

Ni kitendo cha aibu kila msimu wa ligi wadau na wapenzi kutia kero moja kila msimu. Kero ni viwanja na eneo linalolalamikiwa ni eneo la kuchezea.Hakuna anayeshtuka hakuna anayesumbua akili akaja na mipango ya namna ya kutatua kero hii ambayo iko kila msimu wa ligi.

Tusibakize akili zetu Dar es salaam peke maana kutoa maamuzi kwa mambo yenye kusababisha kero kunasaidia kuinua maendeleo ya eneo husika. Wakati watu wa Singida roho inawauma kwa timu yao kutumia uwanja wa Jamhuri Dodoma ndipo inapowapa hasira ya kurekebisha uwanja wao. Maamuzi yao magumu yameleta maendeleo katika uwanja wa Singinda pale Namfua.

Kuogopa kutoa maamuzi kwa hofu ya kuwaumiza watu Fulani hii haiwezi kuwa harakati za kuufanya moira wa Tanzania ufike mbali kwasababu kutakuwa na kuogopana kwa sababu ya Fulani. Tunapofurahia utumbuajibwa Rais wa nchi hii basi nasi tuige kwa manufaa ya soka letu siku zijazo.
0628994409
©Nishani Media.co.Ltd

No comments:

Post a Comment