Tuesday, September 5, 2017

AFYABANDO KAMPENI KUWAKOMBOA WATANZANIA


 Mtaalam Mwelekezi wa Afyabando-Nordic Foundation Tanzania, Dkt. Respicius Salvatory akiongea na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Septemba 3 2017, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kujishindia kadi ya bima ya Afya ijulikanayo kama ‘AfyaBando’. Kulia ni Afisa Mwandamizi Mipango na Utawala wa Taasisi ya Nordic, Maria Nimrod na Afisa Tehama wa Taasisi hiyo, Dickson Leonard.
 Afisa Mwandamizi Mipango na Utawala wa Taasisi ya Nordic, Maria Nimrod akifafanua jambo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kujishindia kadi ya bima ya Afya ijulikanayo kama ‘AfyaBando’. Pamoja naye ni Mtaalam Mwelekezi wa Afyabando-Nordic Foundation TanzaniaDkt. Respicius Salvatory (wa pili kulia) , Afisa Tehama wa Taasis hiyo, Dicson Leonard Afisa Afya na Teddy Uledi. (Imeandaliwa na Robert Okanda Blogspot) 
HOTUBA   YA MTAALAM MUELEKEZI WA MRADI WA AFYABANDO. DKT. RESPICIUS SALVATORY KATIKA UZINDUZI WA KAMPENI YA KUAMASISHA WATANZANIA KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA KUPITIA KAMPENI YA AFYABANDO INAYORATIBIWA NA TAASISI YA NORDIC FOUNDATION TANZANIA LEO TAREHE 03/08/2017 KEBB’Y HOTEL.
Ndugu Waandishi wa habari
Napenda kuchukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika mahali hapa. Pia mimi kama mtumishi wa umma kwenye sekta ya afya napenda kuwashukuru sana Waandishi wa habari kwa kuitikia wito wetu huu kwani kampeni tunayoizindua leo yaani Afyabando ni muhimu sana kwa kila Mtanzania.
Mimi napenda kujikita kwenye mambo muhimu ambayo napenda watanzania waweze kuyajua na kuyafanyia kazi.  Kwanza kabisa mimi naongea kwa uzoefu wa miaka mingi ya kazi katika jiji letu hili kama sehemu ya Tanzania.  Kwa siku tunapokea wagonjwa wengi sana tena sana. Kwa kutokana na uzoefu huo pamoja na kupokea wagonjwa wengi nimekuja hapa ndugu Waandishi kuwaomba na kutoa Elimu kwa Watanzania umuhimu wa Bima ya afya. Ndugu zangu si utani tena, Bima ya afya ni muhimu sana, hivyo inabidi tusaidiane kuondoa changamoto  zifuatazo ili watu wengi wapate kujiunga.
  1. KUONDOA MTIZAMO HASI/MTIZAMO FINYU KUHUSU BIMA YA AFYA.
Ndugu Waandishi ni muhimu tushirikiane kutoa elimu kwa umma ili kuondoa mtizamo hasi dhidi ya bima ya afya. Nadharia ya Bima ni jambo ambalo halijazoeleka kwa jamii zetu hivyo ni jukumu la kila mtu kutoa elimu na kumuamasisha mwenzake umuhimu wa kuijunga na bima. Ugonjwa haupigi hodi hivyo ni vizuri kuacha kuwa na mtizamo hasi kuhusu Bima. Ni jambo la kushangaza watanzania wanapenda sana kuchangia misiba na kwa pesa nyingi lakini hawana utamaduni wa kuchangia wapendwa wao kupata Bima ya afya. Ni jambo la kushangaza watanzania wanapenda sana kuchangia harusi, kitchen party , birthday party na mambo mengi lakini watanzania hawana utamaduni wa kumchangia ndugu kuwa na Bima ya afya.
Ndugu Waandishi wa habari ninawaomba kupitia hadhara hii kuwajulisha Watanzania kuwa huu sasa ni wakati wa kubadilika na kutumia umoja wetu kuanza kuchangia ndugu na jamaa kadi za bima. Ni vizuri tuanze kuamasishana hivyo. Sisi watumishi wa hospitali za umma mnatupatia wakati mgumu sana, anafika mgonjwa hana bima wala pesa za matibabuhata chakula. Ndugu na jamaa ndipo wanaanza kuanza kuchanga tena kwa shida na inabidi mgonjwa tumpokee na kumuandika madeni. Naomba watanzania waache kusubiri kuchangia misiba waanze kampeni za kifamilia, kijamii na maeneo yao ya shughuli za kazi hasa hasa sekta binafsi kuanza kuchangia kadi ya bima. Tuanze kukumbushana na kuulizana je wewe una kadi ya bima. Watanzania tuache tabia ya kuchangia pesa nyingi harusi lakini bila kuchangia kadi ya Bima.
Tunaomba waandishi wa habari tusaidieni sana kufikisha elimu hii ili tuweze kuwa na mwamko wa kuchangia Bima zetu za afya kwa nguvu na hari mpya. Ni kwa msingi huu sasa watanzania wachamkie fursa hii yah ii kampeni ya Afyabando kwa kucheza hii bahati nasibu ya kijamii yenye uhakika kwani washindi ni wengi na hata kwa shilingi mia tano mtu anapata Bima ya afya. Naomba Waandishi na nyinyi changamkia hii fursa ya kupata Bima kwa kujiunga na Afyabando tusipende kuchangia misiba bali tupende kuchangia kuboresha afya zetu kupitia Bima ya afya.
  1. TABIA YA MATIBABU YA MAZOEA NA HOLELA KWA KUKOSA BIMA YA AFYA
Ndugu Waandishi wa habari  napenda  kusisitiza kuwa kumekuwa na tabia yakufanya matibabu ya mazoea kwa mtindo wetu wa mila yaani kufanya matibabu pasipo vipimo. Watu wengi wanashindwa kwenda kupima afpya zao na kufanya uchunguzi kwa sababu hawana Bima ya afya na kutoa pesa kufanya hivyo ni mpaka mtu awe mgonjwa. Hata akiwa mgonjwa wengi wanafanya matibabu ya mazoea ya kwenda kwenye maduka ya dawa mitaani na kununua dawa kwa kufanya hisia mbali mbali za magonjwa yanayowakabili. Matokeo yake wengine wanameza dawa zenye mathara makubwa kwenye miili yao na kupelekea vifo au magonjwa kuwa sugu. Ndugu waandishi wa habari na ndugu watanzania tuache hii tabia ya matibabu holela ni hatari sana kwa afya zetu ni wengi chazo kikubwa ni kukosa bima ya afya. Hivyo tuchangamkie Afyabando ili tuweze kuepuka matibabu holela nay a mazoea.
  1. TUWE NA MTIZAMO CHANYA KWAMBA BIMA YA AFYA NI KINGA KWA WAGONJWA
Ndugu Waandishi wa habari, Bima ya afya ni kimbilio la wagonjwa na ni muhimu sana kila Mtanzania kuwa nayo. Ni jambo la kushangaza kuwa bado kuna Watanzania wengi hawana Bima ya afya. Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha zaidi ya watanzania asilimia 73% hawana bima. Hili ni jambo la hatari kwa kuzingatia kuwa gharama za maisha zimepanda sana. Hivyo kuna watanzania wenzetu wengi sana hawana Bima ya afya. Ili tuweze kuokoa maisha yao ni jambo la maana  sana kujenga mtizamo chanya kuhusu bima.  Napenda kupitia kwenu kutoa wito huu kwani kuna watu wengi wanapoteza maisha na kuzidiwa na magonjwa kwa kukosa matibabu sahihi. Wengi wanatumia njia za mkato na za kubabaisha kwa sababu hawana pesa wala bima hivyo kujikuta wanachelewa kupata matibabu hivyo kusababisha ugonjwa kuwa mkubwa na matokeo kupelekea vifo ambavyo vingweza kudhuhirika (Preventive death) . Sasa tunachamgamkie fursa ya Afyabando. Tuamasishane kwa kila mtanzania aweze kupata Bima ya afya.
  1. CHANGAMOTO YA IMANI POTOFU/  TIBA MBADALA
Ndugu Waandishi wa habari kuna napenda kuwaomba watanzania kujua kuwa magonjwa yapo tusitafute njia ya mkato ya kuyakabili kwa kutumia imani zetu na wengine kwenda kwenye tiba mbadala hata kwa magonjwa yanahitaji huduma ya kisayansi.
Sasa niombe watanzania tumie makundi yenu ya kijamii kutafuta bima ya afya kama vile makanisani, vyama vya familia, ukoo, vyama za saccos, vicoba na vikundi vyote hivi vijikite katika kuamasisha umuhimu wa bima. Tuache tabia ya kupenda njia za mkato kwenye tiba mbadala hata kwa magonjwa ambayo siyo ya mchezo mchezo.
UFAHAMU SAHIHI WA NADHARIA YA BIMA KUWA NI RAHISI KULIKO KULIPA KWA PESA TASILIMU.
Ndugu waandishi wa habari matibabu kwa njia ya Bima ya afya ni kwamba mgonjwa anakuwa amechangiwa na watu wengi sana na wengine hawapati maradhi. Lakini mgonjwa anayetumia pesa inabidi atumie pesa nyingi kwa sababu anajigharamia mwenyewe hata waswahili wanasema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Na jambo hili napenda kusisitiza kwamba kuna magonjwa ambayo gharama zake ni kubwa sana kwa mtu wa kawaida hata mtumishi wa umma au binafsi ni gharama sana kumudu. Mfano kwa sasa kuna watanzania wengi wenye matatizo ya figo wanaenda clinic mara tatu kwa wiki ambapo gharama za siku si chini ya laki tatu au nne. Clinic ya figo yaani Dialysis ni gharama sana kwa mtu binafsi kugharimia na hii ndiyo kazi ya bima duniani kote hivyo nawaomba waandishi wa habari tusaidiane kuwaelimisha watanzania ili tuokoe maisha yao. Mfano mwingine, miaka ya siku hizi magonjwa ya moyo nayo yameongezeka sana hivyo kuna wagonjwa wengi sana. Magonjwa haya pia matibabu yake ni gharama sana kwa mtu wa kawaida kumudu. Sasa changamoto ni kwamba mtu ukiugua inakuwa vigumu sana baadhi ya kampuni za bima kukubali maana wanaona wewe ni mzigo kabla ya kuchangia. Kwa sasabu hizi za kisayansi ni lazima kila mtanzania kuchangimkia bima ya afya.
Tafadhali waandishi tuwaelimishe watanzania wajiunge na bima ya afya kwani gharama za matibabu kwa magonjwa niliyotaja hapo juu ni kubwa mno. Fikiria asilimia 73% ya watanzania hawana bima hivyo lazima wapo wengi wanateseka na wengine wanauza mali zao zote kwa matibabu ambapo wangekuwa na bima wasingeweza kuwa kwenye matatizo. Ndugu zangu wanahabari , nrudiaa tena na tena, watanzania tujiunge na bima ya afya na sasa niwashukuru sana Nordic Foundation Tanzania kwa kuja na kampeni hii ya Afyabando na  kweli, hii ni mkombozi kwa wanyonge na watu wengi wasio na bima ya afya.
HITIMISHO
Napenda kuwashukuru ndugu zangu waandishi wa habari, pia nawashukuru viongozi wa Taasisi ya Nordic Foundation Tanzania na pia nawashukuru sana nyote mliohudhuria shughuli hii ya kuzindua kampeni hii kwa watanzania. Narudia watanzania tuchangamkie bima ya afya na kwa sasa naomba tujiunge na Afyabando kwani nimejulishwa kuwa droo ya kwanza ya bahati nasibu hii ya afayabando ni wiki ijayo jumapili ambapo kadi kumi za bima zitatolewa zenye uwezo wa kuwapatia bima familia ya watu sita, mke na mme na watoto wane. Hivyo nunua ticket yako kwa shilingi 500/= tu ili uweze kupata bima ya mwaka mzima. Kwanza bahati nasibu hii ni ya kijamii siyo biashara ndiyo maana washindi ni wengi sana kwani kwa washindi kumi ni fursa kubwa kwa wengi kupata. Na pia wale ambao hawakupata droo ya kwanza wanaweza kupata droo ya pili au  ya tatu. Hakuna kupoteza kwenye Afyabando kwani husipopata wewe anapata jirani yako au ndugu yako au mtanzania mwenzako.
Asante kwa kunisikiliza
Dkt. Respicius Salvatory
Mtaalam Mwelekezi Afyabando-Nordic Foundation Tanzania

No comments:

Post a Comment