Friday, September 29, 2017

MANISPAA YA DODOMA YAANZA KUANDAA HATI MILIKI ZA ARDHI ZA MIAKA 99 KWA KASI, BARAZA LA MADIWANI LAPONGEZA

NA Ramadhani Juma,OFISI YA MKURUGENZI 

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imekamilisha uandaaji wa hati 912 za umiliki wa ardhi za miaka 99 kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Magufuli Mei 15 mwaka huu wakati akitoa tamko la kuivunja iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na shughuli zote kuhamishiwa katika Manispaa ya Dodoma.

Akizungumza katika kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichopokea taarifa rasmi ya makabidhiano ya majukumu ya iliyokuwa CDA kuhamia Manispaa ya Dodoma jana, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi aliwaambia Madiwani na wananchi kwa ujumla waliohudhuria Baraza hilo kuwa, hatua hiyo imefikiwa katika kipindi cha miezi miwili ya Julai na Agosti, huku akiahidi kuwa,Manispaa hiyo itaendelea kutoa huduma hiyo na nyingine kwa kasi inayoendana na matarajio ya wananchi.

Alisema kati ya hati hizo, hati 674 zilizowasilishwa kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi zimeshasajiliwa na zipo tayari kwa ajili ya kukabidhiwa kwa wananchi husika, huku hati 238 zikiwa katika hatua ya kukaguliwa ili zisainiwe.

Alifafaua zaidi kuwa, uandaaji huo wa hati unaenda sambamba na utoaji wa vibali vya ujenzi kwa haraka, ambapo mchakato wa kutoa kibali cha ujenzi unakamilishwa ndani ya siku saba tu baada ya maombi kupokelewa mpaka muombaji anakabidhiwa kibali chake.

Kufuatia taarifa hiyo, wajumbe wa Baraza la Madiwani wakiongozwa na Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe wameipongeza Menejimenti ya Halmashauri na watumishi wote na kuwataka waendelee na juhudi hizo ili pamoja na mambo mengine kuufanya mji wa Dodoma ukue kwa kasi kwa kuwawezesha wananchi na wadau wengine kujenga. 
Mkurugenzi wa wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (kulia) ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi akizungumza wakati wa Baraza la Madiwani la Mnispaa hiyo.

No comments:

Post a Comment