Wednesday, August 23, 2017

WAZIRI MKUU AWAKARIBISHA WACUBA KUJENGA VIWANDA TANZANIA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Balozi Lucas Domingo Polledo, ambapo amewakaribisha wafanyabiashara wa Cuba kuja kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya dawa. 

Amesema kwa sasa Serikali ya Tanzania inaagiza dawa kutoka nje ya nchi jambo ambalo linasababisha kutumia fedha nyingi, hivyo uwepo wa kiwanda utasaidia katika kupunguza gharama. Pia wawekezaji watakuwa na uhakika wa soko la bidhaa zao. 

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumanne, Agosti 22, 2017) wakati akizungumza na Balozi Polledo mjini Havana. Waziri Mkuu yuko nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. 

Alisema Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda nchini kama mkakati wa kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati, hivyo wafanyabiashara kutoka nchini Cuba wanakaribishwa kuja kuwekeza nchini, hususani katika viwanda vya dawa na sukari. 

Waziri Mkuu alisema licha ya Tanzania kuwa ni nchi ya amani na yenye utulivu wa kisiasa, pia imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo litawawezesha watakaokuja kuwekeza nchini kupata tija. 

Pia alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Cuba kwa ushirikiano mzuri na Serikali ya Tanzania kwa sababu Cuba ni mojawapo kati ya nchi zenye ushirikano wa muda mrefu na Tanzania hususani katika masuala ya Kisiasa, Kijamii, Kielimu na Kiuchumi. 

“Tanzania na Cuba zina historia ya kutosha. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere.” 

Kwa upande wake, Balozi Polledo alisema Serikali ya Cuba itahakikisha uhusiano wake na Serikali ya Tanzania unaendelea kuimarishwa. Pia alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi. 

Alisema licha ya kuwahi kufanya kazi kama Balozi katika nchi mbalimbali za Afrika, baada ya kufika Tanzania amefurahishwa na kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na kuimarika kwa hali ya siasa na amani.”Hali hii ni tofauti na mataifa mengine ya Afrika.” 

Pia Balozi Polledo alisema kwamba Serikali ya Cuba itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uboreshaji wa Sekta za Afya na Elimu, ambapo alisema jumla ya madaktari 50 wa Cuba wakiwemo maprofesa 11 wako nchini wakihudumia wananchi katika mikoa mbalimbali. 


IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMATANO, AGOSTI 23, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akisalimiana na Balozi wa Cuba Nnchini Tanzania Bwana Lucas Domingo Polledo walipo kutana kwa mazungumzo ya kikazi jana August 22/2017 akiwa katika ziara ya kikazi Havana Cuba. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment