Monday, August 7, 2017

WADAU WA MISITU WATAKIWA KUZALISHA KWA TIJA MAZAO NA BIDHAA ZA MAZOA YA MISITU NA NYUKI


Dodoma: Ikiwa zimebaki siku mbili kufika kikomo cha Maonyesho ya Kilimo na Mifugo, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amewataka wadau wa misitu nchini kuzalisha kwa tija mazao na bidhaa za mazao ya misitu na nyuki ili kufikia uchumi wa kati.

Akizungumza na wadau hao jana mara baada ya kutembelea Banda la Maliasili na Utalii katika Uwanja vya Maonyesho ya Kilimo Nzuguni - Dodoma alisema serikali imekusudia kuhakikisha inawawezesha wajasiliamari kufungua viwanda vidogo vidogo vitakavyozalisha kwa tija mazao na bidhaa mbalimbali ili kufikia uchumi wa kati.

Odunga alisema katika Mkoa wa Dodoma kuna eneo lililotengwa kwa ajili ya viwanda na kuwataka wadau wa misitu na nyuki kujiunga kwenye vikundi ili serikali iweze kuwasaidia kufungua viwanda vitakavyowawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora.

" Nimetumia muda mwingi kwenye mabanda ya wadau wa sekta ya misitu na nyuki kwa kuwa katika sera zetu tunataka kuona jinsi gani wananchi wanaweza kutumia misitu kwa kuzingatia matumizi endelevu ikiwa ni kutekeleza sera ya misitu na wakati huo huo kutekeleza sera ya viwanda kwa kuzalisha viwanda vinavyotumia malighafi za misitu," alisema Odunga.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Christina Mdeme alisema licha ya kuzalisha kwa tija mazao na bidhaa za misitu na nyuki, wajitangaze na kama bajeti ni tatizo watumie mitandao ya kijamii.

Mdau kutoka kampuni ya Arti Energy Limited ya Dar es Salaam, Abdalah Shehushi alisema kupiti ufadhili wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania wameweza kushiriki maonyesho mbalimbali nchini kuonyesha teknologia, kufundisha na kutoa vitendea kazi vya kutengenezea mkaa mbadala kwa kutumia mimea mikavu, nyasi, mabua na malanda.

“Mheshimiwa naomba nikuhakikishie kuwa tunaweza kutengeneza mkaa bila kukata mti na kuharibu misitu huku tukitekeleza sera ya viwanda kwa vitendo, Arti Energy inafadhiliwa na serikalini na taasisi mbalimbali kuhakikisha wadau wa misitu wanazalisha kwa tija mkaa mbadala bila kukata mti na kuharibu.

Shehushi alisema katika kuhakikisha wakazi wa Kanda ya Kati Dodoma wanazalisha kwa tija mkaa mbadala baada ya maonesho ya mwaka huu, watakaa chini na Kaimu Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa wilaya ya Chemba kuona jinsi gani wananchi wake wanaweza kunufaika na teknologia ya Arti Enegy.

Naye Mwenyekiti wa Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Charles Ngatigwa aliwataka wananchi kufika kwa wingi kwenye Banda la Wizara kupata fursa za utalii, misitu na nyuki zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.

Maonesho ya Kilimo (NaneNane) yalianza Agosti 1, 2017 kote nchini kwa ngazi mbalimbali za kanda huku Maonesho hayo Kitaifa yakifanyika Mkoani Lindi huku Maandalizi na maonesho ya Ki-Kanda yanaratibiwa na uongozi wa mikoa husika.

Maonesho ya 24 ya kilimo na sherehe za Nanenane yatafanyika kwa siku 8 yalianza Agosti 1, 2017 kote nchini kwa ngazi mbalimbali za kanda ambapo Kitaifa yatafika ukomo jioni ya Agosti 8, 2017 katika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

Kauli mbiu ya mwaka huh ni "Zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo/mifugo na uvuvi ili kufikia uchumi wa kati.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Chemba-Dodoma, Simon Odunga (katikati) akipewa maelezo ya bidhaa zilizotengenezwa na malighafi za misitu (vinyago) na mdau wa Wakala wa Huduma za Misitu kutoka kampuni ya Kasana Artist kutoka Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam, Bi. Rukia Katembo (mwenye sweta) katika Banda la Maliasili na Utalii Kwenye maonyesho ya Nane Nane Kanda ya Kati yanayofanyika Katika uwanja wa Nzuguni Dodoma kuanzia tarehe 01/08 hadi 08/08/2017 na kutoa wito kwa wananchi kutembelea banda hilo ili kuweza kujionea faida mbalimbali za uhifadhi wa misitu hususan katika kumuinua mwananchi kutoka uchumi wa kawaida hadi wa kati. Wa Mwisho kushoto ni mdau mwingine Angel Msangi.

Mdau wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzaniakutoka kampuni ya Jem Herbarist kutoka Bukoba inayozalisha bidhaa zake kwa kutumi mti wa Mlonge na Mshana, Bi. Janerose Mtayoba (mama mwenye kofia) akiwaeleza wananchi (wanaosoma maelezo ya dawa) waliotembelea Maonyesho ya Kilimo/Mifugo na Sherehe za Nane Nane Kanda ya Kati Dodoma matumizi ya dawa anazozalisha, kulia ni Katibu wa Chama cha Waganga na Wakunga wa Jadi Tanzania, Tabibu Issah Mkombozi akisikiliza maelezo hayo.

No comments:

Post a Comment