Wednesday, August 30, 2017

TAMKO LA KUZINDUA MAADHIMISHO YA MIAKA 30 YA TAMWA


Na Edda Sanga
Wanaharakati wenzangu, karibuni TAMWA, mahali adhimu ambapo tumeamua kuzindulia maadhimisho ya miaka 30 ya Chama Cha Wandishi Wa Habari Wanawake Tanzania.
Jina la TAMWA si geni masikioni mwa Watanzania walio wengi, ikizingatiwa hiki ni chama kikongwe cha wanahabari Tanzania ambacho mithili ya chombo baharini, kimehimili mawimbi, makubwa na madogo, mitikisiko na misukosuko ya hapa na pale, na bado kikaweza kuelea katika bahari tulivu. Itoshe kusema, tumetoka mbali.
Mimi mbele yenu ni mmoja wa waasisi wa Chama Cha TAMWA, kwa niaba ya wenzangu kumi na mmoja, tulio hai ni kumi, ambapo wawili wametangulia mbele za haki. Namshukuru Mungu ametujalia neema ya kuuona Mwaka uliotutunuku fursa ya kuanzisha Chama hiki, japokuwa tunazindua harakati za maadhimisho haya, tukiwa na takriban siku 78 kufikia kilele hapo tarehe 17 Novemba Mwaka huu.
Tungependa ndugu zetu, marafiki zetu, wadau wetu, Watanzania wenzetu mmoja mmoja na katika ujumla wenu, muungane nasi kufurahia fursa hii ya kuadhimisha siku hii muhimu ambayo katika historia ya kuwepo kwetu, tunahesabu mafanikio lukuki tuliyoyapata.
Moja ya mafanikio hayo ambayo ni vigumu kusahau ni ushawishi, kuzengea na kuzonga kuliko fanyika kwa ustadi mkubwa , tukiwa na wenzetu TGNP, TAWLA, MEWATA, WLAC, LHRC, CRC na mashirika mengine kama hamsini hivi tukitetea kubadilika kwa sera, na sheria kandamizi zinazomnyima haki mwanamke na mtoto, hasa mtoto wa kike. Furaha yetu ilikamilika , pale Mwaka 1998 tulipofanikiwa kuongea na wabunge, wakatuelewa na kuwazawadia Watanzania SHERIA YA MAKOSA YA KUJAMIIANA , maarufu kama SOSPA. Utakumbuka pia sheria hii iliboreshwa Mwaka 2005.
Uzuri wa sheria hii ya SOSPA, ni kwamba kwa mara ya kwanza, ilitamkwa wazi kuwa ukeketaji ni kosa la jinai, ikampa mtoto wa kike ulinzi wa kutofanyiwa ukatili akiwa chini ya umri wa miaka 18.

Huko Zanzibar, sheria ya spinster ambayo ilimtaka mtoto wa kike aliyepata mimba chini ya umri wa miaka 18 afukuzwe shule na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, wakati mwanaume aliachwa huru kutokana na kutokuwa na kifaa cha DNA, marekebisho yalifanyika katika sheria hiyo ambapo kifungo kwa mtoto wa kike kilifutwa na mwanamume aliyempa mimba anawajibika kutoa matunzo ya mtoto hadi atakapofika miaka 18.

Januari 2008 ulizinduliwa mpango wa kuboresha hali za wanawake kiuchumi na kijamii uitwao WEZA, ambao ulitekelezwa na shirika la CARE TANZANIA, kwa kushirikiana na TAMWA ZBR. Mpango huu uliangalia shehia ya Unguja Kusini, na Kaskazini Pemba kwa kuhusisha makundi 300 ya wanawake 6,000 ambao waliunda vikundi vya kuweka na kukopeshana kwa ajili ya uwekezaji katika miradi ya uzalishaji mali na kuongeza kipato kwa ajili ya ustawi wa jamii. Azma hii ni katika kuhalalisha usemi maarufu kwamba ukimwezesha mwanamke, umeiwezesha jamii.
Mafanikio zaidi ni pale kwa kushirikiana na wenzetu wanasheria, Mwaka 1999 sheria ya ardhi na sheria ya ardhi ya vijiji, iltoa fursa kwa wanawake kumiliki ardhi, na kwa mara ya kwanza, wanawake waliruhusiwa kushiriki katika kutoa suluhu ya migogoro ya ardhi.
TAMWA, kwa ujasiri mkubwa, ilivunja ukimya wa mauaji ya vikongwe yaliyokuwa yakiendelea Shinyanga na kufanikiwa kufanya suala hilo liwe ajenda ya kitaifa. Aidha kwa kutumia vyombo vya habari tukishirikiana na mashirika mengine, tulifanikiwa kuongeza idadi ya wanawake bungeni kutoka asili mia 20 mwaka 2000 hadi 36 mwaka 2005 na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tulimpata spika wa bunge mwanamke, Mama ANNE Semamba Makinda ambaye ametuwakilisha vizuri hadi alipostaafu.

Kama kuna kazi kubwa na ya kusifika imefanywa, na inaendelea kufanywa kwa ufadhili wa DANIDA toka mwaka 2012 ni katika GBV, ambapo TAMWA ikishiriana na CRC kituo cha usuluhishi na ushauri nasihi , na bila kusahau bang style ambayo kwa mfumo wake inafanana na kampeni. Mfumo huu tuliutumia sana TAMWA, ambapo vyombo vya habari vinatumika kwa wakati moja kuandikia na kutangaza suala moja kupitia angle tofauti tofauti kwa kipindi cha wiki, wakati mwingine hata zaidi.
Huu ni mkakati tuliouibua wakati tunapanga mipango iliyotupatia ushindi wa SOSPA. Matokeo yake ni makubwa , HAYANA KIFANI.
Kwa mtindo huo vile vile tumekemea na kuhamasisha jamii iachane na mila potofu, za kuwaoza kinguvu watoto wa kike katika umri mdogo kwa wanaume ambao wana umri mkubwa. Sifa nyingine kubwa kwa TAMWA, ni mafunzo ambayo tumeendesha kwa nyakati mbali mbali kwa wandishi wa habari ili waziandike kwa jicho la jinsia.
Tumepinga ukatili dhidi ya watoto, tumehamasisha wazazi na walezi wawapeleke watoto wa kike shuleni ili wapate elimu, maarifa na ujuzi vitakavyosaidia kuwapa mawanda mapana ya fursa zilizopo ili wafaidi Maisha yaliyo bora kwa ajili yao na watoto wao.
Hatimaye tumeelimisha, tumehamasisha na tutaendelea na harakati hizo tukiamini watoto wa kike na wakiume wakizifahamu haki zao za kijamii, kiafya na kiuchumi, wataweza kuzipigania na kuzitetea, na hivyo taifa letu kuondokana na umaskini ili maendeleo endelevu yatapatikane katika kipindi kifupi.

Wanaharakati wenzangu, TAMWA toka mwanzo iliamini sana katika kufanya utafiti kabla ya kushughulikia tatizo lolote lile. Kwa mfano, tuliona wengi wetu tumejengwa kuimba nyimbo za kikoloni kama vile London bridge is falling down au where are you going my pretty maid. Huu ni utamaduni wa wenzetu ambao waliuingiza katika lugha yao.
Baada ya kutafakari, tukaona haina mantiki sisi Watanzania na hasa watoto wetu kuendelea kuimba nyimbo zinazo upaisha utamaduni wa wenzetu wakati tuna nyimbo zetu nzuri zinazo akisi mandhari mazingira, hulka, malezi na mazoea yetu. Tunazielewa zinatuhusu na zina mantiki, nyimbo kama mabata madogo madogo yanaogelea katika shamba zuri la bustani, au maua mazuri yapendeza au kofia nyembamba nk .Tukamtafuta mwanamziki wetu , mdogo wake marehemu Patrick Balisidya ambaye alitutengenezea cassette nzima ya nyimbo za watoto ambazo tuliwapa RTD wakati huo wazitumie kuweka mahanjam katika vipindi vya watoto. Kwa Bahati mbaya cassette haipo lakini kitabu kipo. Vivyo hivyo, wakati huo, suala la madawa ya kulevya lilikuwapo japo si kwa ukubwa tunaoushuhudia leo.
Tulifanya utafiti na kuangalia kiini chake, madhara yake na kuandika machapisho kadhaa kuihadharisha jamii kuingia katika angamizo la kizazi cha sasa na kijacho kama hatutafanya kazi ya ziada kuweka sheria kali dhidi ya wauzaji na watumiaji wa madawa ya kulevya. Waswahili wanasema mwanzo wa makubwa ni madogo na pia kwamba hata mbuyu ulianza kama mchicha. Kwetu TAMWA tulikemea,
Tuliandika sana na kufanya vipindi kadhaa redioni. TV wakati huo ilikuwa Znz tu.
Baadhi ya machapisho hayo ni Sauti ya Siti, ambayo ni sauti ya wanawake. Tumekuza sana sauti za wanawake na watoto, kudai washirikishwe katika maendeleo ya nchi ili kero zao zitatuliwe na mchango wao uthaminiwe na kuheshimiwa, waweze kuishi Maisha yenye hadhi na yenye ustawi.
Haya ni baadhi tu ya mengi yaliyofanywa na TAMWA.
Wakati tunaendelea na harakati hizi, tukiwa na umri huu mkubwa wa miaka 30. tunawiwa kuchukua nafasi hii ya kipekee kabisa, kuwashukuru wote, hasa wandishi wa habari ambao mmetuwezesha kuwafikia watanzania kwa idadi kubwa kwa kipindi chote hiki. Kama usemi wa Misri unavyodhihiri wakati wakizungumzia umuhimu wa mto Nile kwa uhai wao, kwamba no Nile, no Egypt, na sisi TAMWA tunasema no media no TAMWA. Nadhani mnanielewa. Kupitia kwenu vyombo vya habari, uelewa wa jamii umeongezeka, utayari wao kukemea madhila haya tunauona, tunausikia na tunausoma.

Kwa ushahidi zaidi tena wa kisayansi, TAMWA, inafanya kazi na inaendelea kufanya kazi katika wilaya kumi kwa ufadhili wa DANIDA unaoitwa GEWE I & 2 toka Mwaka 2012. Wilaya hizo ni WETE, (PEMBA KASKAZINI ) UNGUJA MJINI MAGHARIBI,UNGUJA KUSINI, KISARAWE,NEWALA MTWARA,MVOMERO MOROGORO,LINDI VIJIJINI,RUANGWA LINDI, KINONDONI NA ILALA DSM. Wakati mradi unaanza, uelewa wa watu katika wilaya hizo ulikuwa 11% , baada ya miaka 2, utafiti uliofanywa ulionyesha ongezeko la 4% hadi kufikia 16%. Kwa jicho la haraka haraka tunaweza kusema asili mi anne ni ndogo sana lakini ni kubwa kwa kipindi kifupi cha miaka miwili kwani kadri tunavyoendelea kuhamasisha na kuwapa uelewa na mbinu za kuchukua hatua, tutaona mabadiliko makubwa zaidi. Nini siri ya mafanikio yetu?

Tunapenda pia kutamka wazi, kwamba kujitolea kwetu, nyakati zile kwa hali na mali, na ujasiri wetu kushughulikia masuala ambayo kijamii bado yalikuwa na hat leo tunaweza kusema yana ukakasi, kumetujengea uwezo wa kuendelea kutetea haki za wanawake na watoto katika mfumo wa kisayansi. Uwezo wa kuthubutu umekuwa nguzo madhubuti na yote tuliyofanya tuliyaamini na tulichukulia kazi hiyo kama wito kwa jamii. Sisi tumepata faida ya kuwa wandishi tuisaidie jamii kwa ujumla wake nayo ipaze sauti lakini zaidi tulilenga wale walio dhalili miongoni mwetu wakiwamo wanawake , walemavu na watoto.

HUKO TUENDAKO:
Masuala ya unyanyasaji , ukatili wa kijinsia bado yapo, na naweza kusema ukatili umepitiliza kiwango cha ubinadamu. Hata ukatili kwa watoto unazidi. Hapa nazungumzia ubakaji ulawiti, utumikishaji watoto katika mashamba, majumbani , kwenye madanguro, ukatili wanaofanyiwa watoto mitaani majumbani mwetu na ndugu zetu, marafiki zetu, wageni wetu na majirani pia.

Mengi ya matukio haya hayaripotiwi TAMWA inasikitishwa sana na jamii inayoishi karne ya 21 kukosa ujasiri wa kuripoti na zaidi kukosa uzalendo wa kutoa ushuhuda ili haki itendeke.Kama anavyosema Rais wetu Mh. Magufuli, rushwa inasababisha haki isitendeke na sote tunajua jinsi ambavyo baadhi ya wenye mamlaka wanavyopindisha sheria na kufanya mwenye haki aonekane mhalifu na mhalifu aonekane mwenye haki. Katika masuala ya ukatili na unyanyasaji rushwa imekithiri sana na ni kikwazo kikubwa sana katika kazi inayofanywa na TAMWA. Bila ushirikiano wa dhati kati ya familia zetu na vyombo vya dola, madaktari, walimu, majirani, madhehebu ya dini na serikali, matatizo haya ya kijamii hayawezi kuisha. Tutaendelea kujenga kizazi kiso maadili, kilichopondeka mioyo, kisichojiamini, kilichodhoofu kiafya, kiakili ambacho pia kitakuwa hakina mwelekeo.

Kituo cha usuluhishi na ushauri nasihi hapa TAMWA, kina uwezo wa kuwahudumia waathirika wa matatizo hayo, lakini hatuna mahali stahiki pa faragha ambapo mteja anaweza kujieleza kwa uwazi na kwa kujiamini.
TAMWA inataraji kuweka jitihada zaidi katika kuwasaidia vijana hasa katika kukabiliana na tatizo jipya la ukatili wa kijinsia utokanao na matumizi ya ya mitandao, yaani internet.
Tunawasaidia vijana ili wawe na mtazamo chanya katika Maisha yao na vizazi vyao. Wawe na mbinu za kutambua kupambana na ukatili huu mpya unaoendelea kukua kwa nguvu na kusambaa kwa haraka katika jamii yetu.

TAMWA, inataraji kuongeza mawasiliano ya karibu na vijana kupitia kurasa za face book, instagram twitter na kuboresha tovuti yetu ya www.tamwa.org ili iwe na taarifa nyingi zaidi za muhimu kwa jamii hasa kwa kizazi kipya cha dot.com.
Kwa mantiki hiyo, lengo la mkutano huu, ni kuzindua harambee ya kuchangisha fedha ili tupate kituo cha kuwasaidia wahanga wa ukatili wa kijinsia ikiwezekana nchi nzima.
Aidha, tunaandaa kitabu kinacho akisi safari yetu ya miaka 30, yakiwemo mafanikio, matatizo, changamoto na mafunzo tuliyo pata katika kipindi chote hiki. Tuna mpango pia wa kutengeneza documentary ya kielectroniki itakayoelezea mengi zaidi kuhusu TAMWA.
Tuna imani kubwa Watanzania watatuchangia kwa hali na mali , ili haya tuliyopanga kufanya, yawezekane. Tunaomba tuwe sote katika mwelekeo wetu wa kutetea haki za binaadamu, kapinga ukatili dhidi ya wanawake, walemavu na watoto, ili TANZANIA yetu iwe na amani endelevu. 

ASANTE SANA KWA KUSIKILIZA.


NJIA ZA KUCHANGIA:
1. KWA NJIA YA TIGO PESA: -
Piga *150*01# OK
Chagua Lipia Bili
Ingiza Namba ya kampuni 606060
Weka Namba ya kumbukumbu 606060
Ingiza Kiasi kisha namba yako ya siri kukamilisha.
Jina la kampuni ni TAMWA

2. KWA NJIA YA BENKI:
Jina la Bank CRDB
Account namba: 01J2027600600
Jina la Account: TAMWA

Kwa maelezo zaidi tupigie simu namba 0222772681 au 0222771005 TAMWA.


No comments:

Post a Comment