Thursday, August 24, 2017
SERIKALI KUWASHUGHULIKIA WAHALIFU MTANDAONI
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliokutanisha Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na uongozi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kupata elimu juu ya Sheria ya Usalama wa Mitandao, Utekelezaji wake na namna ya kuchukua tahadhari, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Hamza Juma (wa pili kulia), akizungumza na wajumbe wa Kamati na watendaji wa TCRA katika ziara ya kikazi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani.
Mwanasheria Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Philip Filikunjombe akiwasilisha mada kwa wajumbe wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar inayohusu Sheria ya Usalama wa Mitandao. Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam ulikuwa na lengo la kutoa elimu juu ya Sheria ya Usalama wa Mitandao, utekelezaji wake na namna ya kuchukua tahadhari .
Wajumbe wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakisikiliza mada iliyokuwa inawasilishwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Barnabas Mwakalukwa (hayupo pichani), wakati wa ziara ya kikazi katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, ametoa onyo kali kwa wale wanaofanya uhalifu kwa njia ya mtandao kuchukua tahadhari kwani hawapo salama na kuahidi kuwashughulikia kwa mujibu wa Sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, katika mkutano uliokutanisha uongozi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Naibu Waziri Ngonyani amesisitiza kuwa serikali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini wamendelea kufanya doria katika mitandao ili kubaini watu ambao wanatumia vibaya mitandao.
“Tutumie mitandao kwa ajili ya kuleta maendeleo na si kinyume chake kwani ukifanya uhalifu wowote kwa njia ya mtandao tutakukamata popote ulipo na kukuchukulia hatua kwa mujibu wa sheria”, amesema Eng. Ngonyani.
Aidha, Naibu Waziri Ngonyani amewataka wananchi kutumia kikoa cha Tanzania (.tz), na Kituo Mahiri cha Taifa cha Kuhifadhi Data (NIDC), kwa ajili ya kuhifadhi taarifa zao ili zisiingiliwe kwa urahisi na kuweza kuibiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Hamza Juma, ameitaka Mamlaka hiyo kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa jamii kuhusu masuala ya matumizi ya mtandao kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
“Nawaomba TCRA na vyombo vya habari nchini msaidie kusambaza elimu hii kwa wanachi ili waweze kupata uelewa wa masuala ya matumizi salama ya mtandao na changamoto zake”, amesisitiza Mhe. Juma.
Kwa upande wake Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Barnabas Mwakalukwa, ametoa onyo kali kwa wale wanaotumia mitandao vibaya katika kuleta uchochezi wa kidini, kisiasa na kutumia majina ya viongozi na watu maarufu kwa ajili ya kufanya utapeli kuacha mara moja kwani Jeshi la Polisi litahakikisha linachukua hatua kali za kisheria dhidi yao.
Amewataka wananchi kuwa tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa zinazohusu uhalifu wa kimtandao ili kuweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kwani suala la ulinzi na usalama ni letu sote.
Tangu kuanzishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 kumewezesha Jeshi la Polisi nchini kufuatilia kwa karibu na kushughulikia uhalifu mtandaoni ambapo kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Juni, 2017 Jeshi la Polisi limeweza kukamata watuhumiwa 315, kufikisha mahakamani kesi 153, kesi 19 zilipatikana na hatia na zingine zipo chini ya upelelezi.
No comments:
Post a Comment