Na Rajabu Mkasaba, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa kuwepo kwa mabadiliko
makubwa ya kimaendeleo baada ya kuundwa kwa Mamlaka ya Viwanja vya ndege vya
Zanzibar kumeweza kuongeza mapato na kuahidi kuimarika zaidi hali hiyo ndani ya
kipindi chake cha uongozi.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, alipokutana na
uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Bodi ya Wakurugenzi
ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege pamoja na Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege katika vikao vinavyoendelea Ikulu mjini Zanzibar.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka
hiyo kwa kufanya mabadiliko makubwa katika viwanja vya ndege vya Zanzibar hatua
ambayo imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa ongezeko la mapato katika viwanja
hivyo.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa licha
ya baadhi ya changamoto zilizopo lakini Mamlaka imeweza kupata mafanikio
makubwa na hivi leo viwanja vya ndege Unguja na Pemba viweza kuimarika na
kuleta tija kwa kuongeza mapato.
Akizungumza suala zima la fidia kwa wananchi waliojenga
pembezoni mwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar Dk.
Shein alisema kuwa ni vyema likatafutiwa ufumbuzi kwa kuwatafuta wahusika na
kuwasikiliza madai yao ili hatua za malipo ziendele kuchukuliwa.
Akizungumza na uongozi wa Wizara hiyo kupitia Bodi
ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba pamoja na Uongozi wa Shirika hilo, Dk.
Shein alisisitiza haja ya Shirika hilo kuzitambua na kuziorodhesha ili kujua
idadi ya nyumba zao zote za Unguja na Pemba pamoja na zile za Wakala hatua
ambayo pia, itasaidia kuepusha udanganyifu.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa
Bodi ya Shirika hilo pamoja na uongozi wa Shirika hilo kwa mafanikio makubwa yaliopatikana kwa kipindi
kifupi.
Alieleza haja ya kuwepo utaratibu wa kuwatambua
wakaazi wananoishi katika nyumba zote za Mji Mkongwe wa Zanzibar ili iwe rahisi
katika kutekeleza mipango ya Serikali huku akieleza azma ya Serikali ya kujenga
miji ya kisasa sambamba na kutekeleza mradi wa kufukia bahari katika eneo la
pwani ya Gulioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kisasa zikiwemo hoteli.
Wakati huo
huo, Dk.
Shein alikutana na uongozi wa Wizara hiyo walioongozana na Bodi ya Wakurugenzi
ya Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe na Uongozi wa Mamlaka ya
Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe na kueleza umuhimu wa kuweka utaratibu
maalum juu ya kupunguza foleni ya gari katika barabara inayopita katika Bandari ya Malindi.
Aidha, alieleza haja ya kuzingatia na kufuata
kanuni na misingi ya Sheria iliyounda Bodi hiyo ili Mamlaka hiyo na Bodi yake
iweze kufanya kazi kwa ufanisi pamoja na kufuata Sheria nyengine zote muhimu
huku akieleza umuhimu wa uhifadhi wa mji huo.
Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Idd alieleza kwamaba tabia ya kukodishwa nyumba kwa kutumia vilemba ambapo
hatua hiyo ndio chanzo kikubwa cha upotevu wa nyumba za Serikali huku akisikitishwa
na baadhi ya wananchi waliopewa nyumba na Serikali na wao kuzikodisha ama
kuziuza bila ya kufuata taratibu na sheria zilizopo.
Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Usafirishaji Balozi Ali Karume kwa upande wake alieleza hatua zzinazoendelea kuchukuliwa
katika Wizara yake katika kutoa ushirikiano uliopo kwa viongozi, wafanyakazi,
Bodi pamoja na wajumbe wake.
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Abdulhamid Yahya Mzee kwa uonde wake alisisitiza haja ya kuimarisha
usalama katika viwanja vya ndege vya Zanzibar kwani Mashirika ya ndege na hata
wageni hilo wamekuwa wakilipa kipaumbele.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Zanzibar Abdulhani Msoma aalieleza kuwa mapato yanayokusanywa katika viwanja
vya ndege yameongezeka kutoka TZS Bilioni 12.9 mwaka 2011/2012 hadi kufikia TZS
Bilioni 39.3 mwaka 2016/2017.
Alieleza kuwa idadi ya mashirika ya ndege
imeongezeka kutoka mashirika 63 mwaka 2011 hadi mashirika 78 mwaka 2016 ambapo
kati ya mashirika hayo, mashirika ya kimataifa yameongezeka kutoka 39 mwaka
2011 hadi 48 mwaka 2016 na mashirika 24 ya ndani yameongezeka hadi kufikia 30
mwaka 2016.
Aliongeza kuwa idadi ya abiria imeongezeka kutoka
753,971 mwaka 2011 hadi abiria 1,032,043 mwaka 2016 sawa na asilimia 137 kati
ya abiria hao abiria wa kimataifa wameongezka hadi kufikia 529,696 mwaka 2016
kutoka abiria 283,755 mwaka 2011.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Zanzibar
Mohamed Hafidh Rajab alisema kuwa licha ya uchanga wa Shirika hilo lakini
ukusanyaji wa mapato yataongezeka kutoka TZS bilioni 1.6 mwaka 2017/2018 hadi
kufikia TZS bilioni 48 katika mwaka 2021/2022 huku akieleza azma ya ujenzi wa
nyumba za makaazi zikiwemo za wananchi wenye kipato cha chini.
Nao uongozi wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji
Mji Mkongwe na Bodi yake ulieleza kuwa baadhi ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa
pamoja na washirika wa maendeleo wameonesha azma ya kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuuimarisha Mji Mkongwe wake ikiwa ni pamoja na kuzifanyia
ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba huku ukieleza hatua zilizofikiwa katika
utekelezaji wa miradi yake.
Katika vikao vya leo, Dk. Shein alikutana na
Uongizi wa Wizara hiyo pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege, uongozi wa Mamlaka pamoja na Bodi ya Shirika la Nyumba na Bodi ya
Wakurugenzi ya Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe na uongozi wake.
No comments:
Post a Comment