Thursday, August 24, 2017

Mpangokazi wa kitaifa wa Haki za Binadamu katika biashara mbioni kukamilishwa

Na MbarakaKambona,

Wadau wa haki za binadamu kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo za serikali, taasisi binafsi na wafanyabiashara wamekuta na kupitia rasimu ya kwanza ya mapendekezo ya Mpangokazi wa kitaifa wa Haki za Binadamu katika biashara.

Wadau hao walikutana Agosti 23, 2017 katika kikao kilichofanyika katika ofisi zaTume ya Haki za Binadamu jijini Dar es Salaam kujadili rasimu hiyo kufuatia utafiti uliofanywa na wataalamu na maoni yaliyokusanywa kutoka katika maeneo mbalimbali ya biashara.

Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,Mhe.Iddi Ramadhani Mapuri alisema kuwa kuanzishwa kwa mpango huo kumelenga katika kuhakikisha kuwa mifumo yote ya kitaifa na kimataifa ya sera na sheria inazingatia na ulinzi na utetezi haki za binadamu wakati wote wa utekelezaji wa majukumu ya kibiashara na kuweka mifumo ya utatuzi wa migogoro ya waathirika pale itakapojitokeza.

Utafiti huo ambao ulifanyika Mei, 2017 ulihusisha wadau mbalimbali wakiongozwa na Tume, zikiwemo taasisi za serikali, taasisi binafsi, wafanyabiashara na wananchi ulifanyika katika maeneo maalum yaliyochaguliwa ikiwemo maeneo ya kilimo katika Mkoa wa Mbeya- Mbarali, Maeneo ya viwanda Mkoani Dodoma na Singida na maeneo yaUtalii upande wa Zanzibar uliofanyika.

Utafiti huo unafuatia tamko la Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilitolewa mwaka 2011 linalotaka nchi wanachama kuanzisha Mpangokazi wa kitaifa wa Haki za Binadamu katika maeneo ya biashara ili kutoa muongozo wa kulinda uvunjifu wa haki za binadamu katika maeneo hayo.

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Francis Nzuki wakati akiongea na waandishi wa habari katika mkutano huo alitoa mifano kadhaa waliyoiona wakati wa utafiti huo moja wapo ni katika maeneo ya Kilimo ambapo wakulima walio wengi wanatumia dawa mbalimbali katika kuzalisha mazao yao kitu ambacho kwa namna moja au nyingine inahatarisha maisha ya watu na mazingira yao, hivyo ni vyema shughuli hizo zikawekewa miongozo ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza baadae.

Aidha, Mhe. Iddi Ramadhani Mapuri alitumia nafasi hiyo ya mkutano kuwakumbusha wadau na wananchi kwa ujumla kwamba utetezi na ulinzi wa haki za binadamu sio wa serikali, taasisi binafsi wala wafanyabiashara peke yao, bali ni jukumu la watu wote.

Pia aliwakumbusha wadau kuwa kazi iliyo mbele yao ya kuandaa mpango huo ni kubwa hivyo ufanisi wao katika maandalizi ya mpango huo utasaidia na kurahisisha utekelezaji wake kitaifa na kimataifa.

Mchakato wa maandalizi ya mpango huo unatokana na ahadi ya Serikali iliyoiweka katika Mpango kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu (NHRAP) wa mwaka 2013-2017 ambapo Serikali ilifunga ahadi ya kuanza kuandaa mpango endelevu wa Haki za Binadamu katika maeneo la biashara.

Mchakato huo unafadhiliwa na taasisi ya Denmark, Danish Institute for Human Rights (DIHR) na Centre for Research on Multinational Corporation (SOMO).

 Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe.Iddi Ramadhani Mapuri akiongea na washiriki wa kikao cha wadau wa haki za binadamu wakati akifungua mkutano huo uliofanyika katika ofisi za Tume zilizopo  jijini Dar es Salaam Agosti 23, 2017. Kulia kwake ni Kamishna Mkaazi wa Tume Zanzibar, Mhe. Mohamed Hassan na Kushoto kwake ni  Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Bwn. Francis Nzuki
 Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Bwn. Francis Nzuki akiongea katika kikao cha wadau wa haki za binadamu mara baada ya Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe.Iddi Ramadhani Mapuri (katikati) kufungua rasmi mkutano huo.
 Mmoja wa watoa mada ya haki za binadamu na biashara, Bi. Nora Gotzmann akiwasilisha mada yake iliyohusu masuala ya Biashara na Haki za Binadamu, jinsi ya kulinda, kuheshimu na namna ya kupata utatuzi wa migogoro inapojitokeza.
 Mratibu wa Mradi wa kuandaa Mpango kazi wa Haki za Binadamu na Biashara kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jovina Muchunguzi akiongea na washiriki wa kikao hicho cha wadau wa haki za binadamu wakati akiwasilisha mada.
 Sehemu ya washiriki wa mkutano huo wakijadiliana namna ya kuboresha Mpangokazi huo.
Mmoja wa washiriki katika mkutano huo, Bwn. Constantine Mugusi akifafanua jambo kwa wana kikundi wenzake wakati wa majadiliano ya kuboresha Mpangokazi huo.

No comments:

Post a Comment