NA HAMZA TEMBA - WMU
.........................................................................................
Katika kuhakikisha sekta ya utalii
nchini inaendelea kukua kwa kasi, Serikali imesema itaimarisha utalii wa Misitu
ya Asili nchini iweze kutoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa tofauti na
ilivyo hivi sasa ambapo hutegemea zaidi utalii wa wanyamapori.
Hayo yamesemwa jana wilayani Lushoto
na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani wakati akiwa
kwenye ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua migogoro
mbalimbali ya uhifadhi.
Alisema sekta ya utalii nchini
imekuwa ikitegemea sana wanyamapori na kusahau vivutio vingine kama vile misitu
ya asili ambayo ndani yake kuna mimea na viumbe hai mbalimbali adimu duniani na
ambavyo hupatikana Tanzania pekee.
“Tumezoea zaidi utalii wa
wanyamapori, utalii wa misitu unaweza kuzidi hata wa wanyamapori, kwenye misitu
yetu ya asili tunajivunia mimea adimu ya asili na viumbe hai mbali mbali kama
vile ndege, vyura, vipepeo, mijusi nakadhalika, tunachotakiwa kufanya ni
kutunza misitu yote ya asili, tuiboreshe na kuitangaza ili kupata watalii wengi
zaidi na pato la taifa liendelee kukua”, alisema Makani.
Kwa mujibu wa tovuti ya Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tanzania ina jumla ya Hifadhi za Misitu ya
Asili 100, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na hifadhi za taifa ambazo zipo
16 pekee, idadi hiyo kubwa pamoja na upekee wake inatoa fursa pana ya
kuendeleza sekta ya utalii nchini.
Akizungumzia mafanikio, Makani
alisema sekta hiyo inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimia 25 ya
mapato yote ya fedha za kigeni. Alisema pamoja na faida hizo, sekta hiyo
inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uharibifu wa misitu ya asili
ambayo ni muhimu kutafutiwa suluhu ya kudumu ili kunusuru misitu hiyo.
“Ni lazima tutafute njia endelevu ya
ulinzi wa misitu, hatuwezi kuwa na askari wa kutosha, walinzi na mitutu, njia
sahihi ni ulinzi shirikishi, tuwaelimishe wananchi umuhimu wa misitu na
tuwaeleze watanufaikaje, tofauti na zile faida za ujumla za upatikanaji wa mvua
na hali nzuri ya hewa, hii itasaidia sana kuwaleta karibu kwenye uhifadhi wa
pamoja”, alisema Makani.
Akizungumza na wananchi wa kijiji
Nywelo wilayani humo kuhusu mgogoro wa mpaka baina ya kijiji hicho na shamba la
miti Shume, Makani alisema tatizo lililopo ni uelewa tofauti kuhusu mpaka huo
baina ya pande hizo mbili, hivyo akuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) kutuma wataalamu wa upimaji waliopima eneo hilo awali
waje wafanye uhakiki wa mpaka huo kwa kushirikisha uongozi wa wilaya,
halmashauri na kijiji hicho ili kuondoa tofauti hizo na kumaliza mgogoro huo
ndani ya wiki mbili zijazo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Lushoto, Januari Lugangika alisema wilaya yake inakabiliwa na changamoto
mbalimbali za uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti ya asili,
uchimbaji wa madini kwenye maeneo ya hifadhi, uchomaji moto misitu na uhaba wa
watumishi.
Katika ziara yake hiyo wilayani
Lushoto, Naibu Waziri Makani alitembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Magamba na
Shamba la Miti la Shume, alifanya pia vikao vinne vya ndani na mkutano mmoja wa
hadhara ambapo alijibu kero mbalimbali za wananchi.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani
(kulia) akijibu kero mbalimbali za uhifadhi kwa wananchi wa Kijiji cha Shume
Nywelo, Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya siku moja ya
kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani
(wa pili kushoto) akisikiliza moja ya kero kuhusu uhifadhi kutoka kwa Abunio
Abraham Shangali (wa pili kulia) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Shume Nywelo,
Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja ya
kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani
(wa pili kulia) akizungumza na viongozi wa kikundi cha uhifadhi na utalii cha Friends
of Usambara kilichopo Lushoto Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya siku
moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani
(kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Sigareti Lugangika
katika kijiji cha Shume Nywelo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua
migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
Muwakilishi
wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mwalimu Elias
Mkwilima akijibu baadhi ya hoja katika mkutano huo uliofanyika katika
kijiji cha Nywelo jana wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga.
No comments:
Post a Comment