Monday, July 31, 2017

Vijana washauriwa kujiunga na awamu ya tatu ya program ya Via Jiandalie Ajira

Meneja Malezi wa Taasisi ya Ujasiriamali na Ushindani Tanzania (TECC), Bw. Daniel Mghwira (katikati) akizungumza kuhusu kuanza kwa kwa awamu ya tatu ya program Via Jiandalie Ajira kwa halmashauri zote za Dar es Salaam, Mkindani Mtwara, Dodoma na Kibaha Pwani, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF),Bi. Haigath Kitala na kushoto Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara na Kilimo Tanzania(TCCIA),Bi. Magdalene Mkocha.

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 24 wameshauriwa kujiunga na awamu ya tatu ya program Via Jiandalie Ajira inayoendeshwa na Taasisi ya Ujasiriamali na Ushindani Tanzania (TECC) ili kupata mafunzo ya ujasiriamali, stadi za maisha, malezi ya kibiashara na kuunganishwa na taasisi za kifedha kupata mitaji kukabiliana na tatizo la ajira. 

Meneja Malezi wa Taasisi hiyo, Bw. Daniel Mghwira alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuwa vijana wajiunge na program hiyo ambayo imeingia katika awamu ya tatu kupata mafunzo hayo ili kukabiliana na tatizo la ajira. 

“Via Jiandalie Ajira awamu ya tatu inawalenga vijana wa Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam, Mikindani Mtwara, Dodoma na Kibaha Pwani,” na fomu za kujiunga zinapatikana katika ofisi za kata, ofisi za maafisa vijana za manispaa za maeneo hayo, aliongeza kusema Bw. Mghwira ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa taasisi hiyo.

Pia fomu hizo zinapatikana katika ofisi za Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (SIDO) na Chemba ya Wafanyabiashara na Kilimo Tanzania (TCCIA).

Alifafanua kwamba fomu hizo zinatolewa bila ya gharama ambapo vijana watakao chaguliwa watafundisha mafunzo ya ujasiriamali, stadi za maisha, malezi ya kibiashara na kuwaunganisha na taasisi za kifedha kupata mitaji kwa njia ya mikopo kwa masharti nafuu, hivyo ni fursa kwa vijana wa maeneo hayo.

Alisema kuanzia sasa hadi mwaka 2020 taasisi yao kupitia program hiyo itafundisha vijana ,3,000 katika mikoa hiyo na hiyo itafanya jumla ya vijana 4,000 wakijumlishwa na waliofundishwa katika program ya kijana jiajiri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF),Bi. Haigath Kitala alisema serikali imetoa kipaumbele katika uchumi wa viwanda, vijana wanahitajika kutumia fursa hiyo ili wasije kuwa watazamaji katika uchumi huo.

“Vijana wanapokuwa wamepata mafunzo kama haya, ni rahisi kwa mfuko wao kuwapatia mikopo ya riba nafuu,” na mfuko huo unatoa mikopo kwa vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi stadi na wanawake wazalishaji mali na wanahitajika kuwa katika vikundi, alisema. 

Alisema pia mfuko unatoa mkopo wa vifaa na wa dhabuni sababu vijana wengi wanashindwa kutekeleza dhabuni hizo kwa kukosa fedha.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara na Kilimo Tanzania,Bi. Magdalene Mkocha alisema chemba inashirikiana na taasisi hiyo katika kuwaandaa vijana kuingia katika ujasiriamali husani katika kutoa malezi.

“Tunapotaka kujenga kada nzuri ya wajasiriamali ni lazima kwa pamoja tushiriki katika hili,” na alitoa ombi kwa serikali na wadau wote kusaidia kusukuma jambo hilo,alisema.

Naye kijana ambaye amenufaika na mafunzo ya taasisi hiyo, Jackson Mmbando alisema mafunzo yanayotolewa na TECC yamewezesha kuanza na kuendesha biashara yake kwa mafanikio makubwa na anawataka vijana wenzake kuwa na nidhamu ya fedha ili kuanza au kuendeleza biashara.

Program hiyo ya Via Jiandalie Ajira inatekelezwa na TECC kwa kushirikiana na wadau wake kama Taasisi ya Kuendeleza Vijana Kibiashara ya Marekani (IYF), Mfukoa wa Rais wa Kujitegemea (PTF), SIDO, TCCIA , Manispaa au Halamashauri za Miji na Wilaya na sasa imefikia awamu ya mwisho kwa mwaka 2017.

No comments:

Post a Comment