Thursday, July 27, 2017

PROF. MAGHEMBE ATAMBUA MCHANGO WA VYOMBO VYA HABARI KATIKA VITA DHIDI YA UJANGILI NCHINI

NA HAMZA TEMBA - WMU

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amevipongeza vyombo vya habari nchini kwa mchango wake katika vita dhidi ya ujangili huku akitoa rai kwa vyombo hivyo kuongeza bidii katika kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa uhifadhi endelevu wa maliasili za taifa kwa faida ya jamii iliyopo na vizazi vijavyo.

Prof. Maghembe ametoa pongezi na rai hiyo leo wakati akifungua mkutano wa sita wa mwaka wa wahariri na wanahabari waandamizi wa vyombo vyote vya habari nchini ulioandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) jijini Tanga huku kaulimbiu ya mkutano huo ikiwa UTALII WA TANZANIA YA UCHUMI WA VIWANDA.

"Ujangili bado upo, Majangili tumepambana nao kweli kweli, na ninyi wanahabari mmetusaidia sana katika kuhabarisha jamii juu ya matukio ya kukamatwa kwao na hukumu wanazozipata, jambo ambalo limesaidia kujenga uoga kwa watu kushiriki katika vitendo hivyo", alisema Maghembe.
Alisema hofu hiyo pamoja na jitihada za Serikali za kupambana na ujangili imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya ujangili nchini hasa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambapo mizoga ya tembo inayotokana na ujangili imeonekana kupungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha ni miaka iliyopita.

Akizungumzia changamoto ya mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini amesema sheria za uhifadhi zinakataza watu kuingiza mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kisheria, hivyo ni wajibu kwa wanahabari kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutii sheria hizo.  "Ni vema wanahabari wakatumia kalamu zao vizuri kuelimisha jamii juu ya athari za muingiliano wa binadamu, mifugo na wanyamapori".

Alisema wanyamapori wanabeba virusi vya magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya bonde la ufa, ndigana, kifua kikuu, homa za vipindi (brucolosis) na kimeta, Magonjwa ambayo yanaweza pia kuambukiza mifugo na binaadamu wanaoishi karibu na wanyamapori. Alisema kuwa endapo muingiliano huo utaendelea kuwepo kwa muda mrefu unaweza kusababisha mlipuko mkubwa wa magonjwa hayo kwa binaadamu na mifugo hivyo kusababisha vifo vingi kwa wakati mmoja.

Prof. Maghembe alisema kumekuwepo na kisingizio cha kumega maeneo ya hifadhi nchini kwa ajili ya matumizi ya kawaida kutokana na ongezeko la wananchi jambo ambalo sio sahihi na kwamba njia pekee na salama ni kubadili mfumo wa matumizi ya rasilimali zilizopo ikiwepo ya ardhi kwa kutumia sayansi na teknolojia na kuweka matumizi bora ya ardhi kwa kulenga matokeo chanya.

Akizungumzia sekta ya utalii, Prof. Maghembe alisema wanahabari wanapaswa kuwa sehemu ya kukuza uchumi wa nchi kwa kushiriki moja kwa moja katika utoaji wa taarifa sahihi kwa Watanzania na wageni kuhusu sekta hiyo bila ubaguzi wa aina yeyote.

"Tuipende nchi yetu, tuitangaze na kuilinda, na katika habari hizi za uchumi tuweke itikadi zetu pembeni tuandike habari za kujenga nchi yetu", alisema Prof. Maghembe.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa, Alan Kijazi amesema sekta ya utalii inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni. Alisema asilimia 80 ya wageni wanaokuja nchini wanatembelea hifadhi za Taifa hususan za ukanda wa Kaskazini jambo ambalo linaweka msukumo wa kuendeleza na kutangaza hifadhi za nyanda zingine ili kuongeza idadi ya watalii na pato la taifa.

Akizungumzia mchango wa TANAPA katika uchumi wa taifa, Kijazi alisema mchango huo umeongezeka ambapo katika mwaka 2015/2016 shirika hilo lilichangia Shilingi bilioni 27 katika mfuko mkuu wa Serikali na mwaka 2016/2017 likachangia bilioni 34 sawa na ongezeko la bilioni saba.

Pamoja na mafanikio hayo alisema jukumu la kuendeleza uhifadhi nchini haliwezi kufanikiwa kwa jitihada za Serikali pekee bila kushirikisha wananchi kupitia vyombo vya habari, Hivyo akatoa rai kwa wanahabari kuiunga mkono Serikali katika kunadi sera za uhifdhi endelevu kwa maslahi ya taifa.

No comments:

Post a Comment