Wednesday, July 26, 2017

MANJI KUOMBA DHAMANA MAHAKAMA KUU

Na Mwene Said wa Blogu ya Jamii, Dar es Salaam.

Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeupa muda wa siku tano kuwasilisha pingamizi la awali dhidi ya maombi ya dhamana ya kesi ya  uhujumu uchumi inayomkabili  Mfanyabiashara Yusufali Maji (41) na wenzake watatu.

Manji na wenzake, pia wanakabiliwa na  kukutwa na vitambaa vya sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)  isilivyo halali vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 236.5.

Hata hivyo, mfanyabiashara huyo amefungua maombi yaliyosajiliwa kwa namba 122/2017, kupinga hati iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kuzuia dhamana dhidi yake na yalitajwa jana mbele ya Jaji Isaya Arufani.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Paul Kadushi, Simon Wankyo na Tulumanywa Majigo, ulidai mahakamani kwamba wanaomba muda kwa sababu wana nia ya kuwasilisha pingamizi la kupinga maombi ya utetezi.

Pia, ulidai kuwa wanaomba mahakama iwape muda wa kuwasilisha majibu ya hati ya maombi ya mshtakiwa.

Jaji Arufani alisema upande wa Jamhuri uwasilishe majibu na pingamizi lao Agosti Mosi na upande wa utetezi kama watakuwa na majibu ya nyongeza wawasilishe Agosti 2 na mahakama hiyo itasikiliza maombi hayo Agosti 4, mwaka huu.
Katika maombi hayo,  Manji anaiomba Mahakama Kuu kutengua hati ya DPP ya kuzuia dhamana yake  iliyowasilishwa Julai 5, mwaka huu aliposomewa mashtaka ya uhujumu uchumi ikiwamo kukutwa na sare hizo.

Aidha, anaiomba mahakama iridhie kumpa dhamana kwa sababu ana matatizo ya kiafya.

Kwa mujibu wa hati ya maombi hayo, Manji anadai kuwa anasumbuliwa na maradhi ya moyo  na kwamba ameambatanisha vyeti vya daktari katika maombi yake.

Katika kesi ya msingi,  Manji na wenzake wanatuhumiwa kukutwa na mihuri ya mbalimbali ya JWTZ isilivyo halali vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 236.5.
Mbali na Manji, washtakiwa wengine ni,  Ofisa Rasilimaliwatu Deogratias Kisinda (28), Mtunza Stoo, Abdallah Sangey (46) na Mtunza Stoo msaidizi, Thobias Fwele (430
Ilidaiwa katika shtaka la kwanza kuwa Juni 30, mwaka huu eneo la Chang'ombe Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Manji na wenzake walikutwa na askari polisi wakiwa na Mabunda (majola) 35 ya vitambaa vya vinavyotengezea sare za JWTZ zenye thamani ya Sh. milioni 192.5 na kwamba zilipztikana isivyo halali.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa mekutwa Julai Mosi, mwaka huu eneo la Chang'ombe 'A' Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na mabando nane ya sare za JWTZ zenye thamani ya Sh. milioni 44.

Upande huo wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa, Juni 30,mwaka huu eneo la tukio la kwanza, washtakiwa walikutwa na mhuri wa JWTZ uliokuwa na maandishi 'Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha Jeshi JWTZ' bila kuwa na uhalali kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.

Majigo aliendela kudai katika shtaka la nne, siku ya tukio la tatu, washtakiwa wote kwa pamoja walikuwa na mhuri wenye maandishi "Kamanda Kikosi 834 Kj Makutupora Dodoma" bila uhalali kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.

Shtaka la tano, siku ya tukio la tatu na la nne, mshtakiwa alikutwa na mhuri wenye maandishi "Comanding Officer 835 Kj  Mgambo P.O BOX 224 Korogwe" bila kuwa na uhalali kitendo ambacho kinahatarisha uslama wa nchi.

Ilidaiwa katika shtaka la sita, Julai Mosi, mwaka huu eneo la Chang'ombe 'A', washtakiwa wote walikutwa na pleti namba za gari zenye usajili wa SU 383 iliyopatikana isivyo halali.

Majigo alidai katika shtaka la saba, eneo la tukio la sita, washtakiwa walikutwa na pleti namba za gari zenye namba ya usajili SM 8573 iliyopatikana isivyo halali.

Kwa mujibu wa mashtaka hayo yaliyofunguliwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa taifa, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha hati ya kuzuia dhamana kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), akiomba washtakiwa wasipewe dhamana kwa usalama wao na maslahi ya taifa.

Pia, DPP alieleza sababu nyingine kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kushughulikia dhamana dhidi ya kesi hiyo.
Kesi ya msingi pia itatajwa Agosti 4, mwaka huu katika Mahakama ya Kisutu.

No comments:

Post a Comment