Wednesday, July 26, 2017

MAHAKAMA YA PILI YA WATOTO NCHINI YAZINDULIWA MBEYA


Na Lydia Churi-Mahakama, Mbeya

Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma leo amezindua rasmi  Mahakama ya watoto katika jiji la Mbeya na kufanya idadi ya Mahakama hizo nchini kufikia mbili. Mahakama ya kwanza ya watoto iko Kisutu jijini Dar es salaam.

Mahakama hii ya Watoto iliyoanza kufanya kazi rasmi Aprili 18 mwaka huu jijini Mbeya pamoja na ile ya Kisutu zina kazi kubwa ya kuamua kesi za watoto wanaojikuta wana ukinzani na Sheria zinazohusu watoto nchini pamoja na kutafsiri sheria hizo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania alisema maendeleo endelevu ya Tanzania yatajengwa kwa misingi ya haki za watoto huku akinukuu andiko la shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na watoto (UNICEF) lisemalo maendeleo ya taifa lolote yatakamilika baada ya watoto kuwa na afya njema, salama pamoja na kupata elimu.

Alisema uzinduzi wa jengo la Mahakama hiyo ya watoto unaashiria safari ndefu iliyonayo Tanzania ya kuhakikisha haki za watoto zinalindwa kwa kuwa pia bado kuna mikoa mingi ambayo inahitaji huduma hii muhimu.

Prof. Juma alisema kazi kubwa ya Mahakama ya Tanzania ni kutoa tafsiri pana ya sheria zinazohusu haki za watoto ili kupanua wigo wa ulinzi kwa watoto huku akiwataka Majaji na Mahakimu nchini kutafsiri sheria hizo ili zitekeleze wajibu wao kisheria.

Akitolea mfano wa Sheria ya Watoto namba 21 ya mwaka 2009, Kaimu Jaji Mkuu alisema sheria hii inashirikisha mihimili yote mitatu hivyo haki zote zinazotajwa na sheria hii ni lazima zipatikane inavyostahili. Prof. Juma pia amewataka Mahakimu wanaosikiliza kesi za watoto kuainisha mapungufu ya sheria hii na kuyawasilisha kwenye kamati ya Jaji Mkuu inayohusu masuala ya Sheria.

Aidha, Kaimu Jaji Mkuu amewataka Majaji na Mahakimu nchini wanaosikiliza kesi za watoto kujisomea zaidi masuala yanayohusu maendeleo ya haki za watoto kwa kuzisoma taarifa za utekelezaji za nchini pamoja na zile za nchi nyingine ili kupanua uelewa wa sheria hizo.

Kaimu Jaji Mkuu pia amewataka Majaji na Mahakimu wote kusimamia na kuhakikisha masuala yote yaliyotajwa na Sheria pamoja na mikataba ya kimataifa kuhusu watoto yanatekelezwa pindi wanapofanya ukaguzi kwenye magereza mbalimbali.

Wakati huo huo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali amewaomba UNICEF kufikiria na kuangalia uwezekano wa kujenga majengo mengine manne ya mahakama za watoto katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Dodoma na Tabora ili kuwapatia Mahakimu fursa ya kujifunza kwa vitendo namna Mahakama za watoto zinavyofanya kazi.

Jengo la Mahakama ya Watoto jijini Mbeya lililojengwa kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na UNICEF limegharimu kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 415 ambapo Mahakama imechangia kiasi cha shilingi milioni 214 na UNICEF shilingi milioni 201.







Kaimu Jaji Mkuu Wa Tanznaia Mhe. Prof. Ibrahim Juma Akifungua Pazia Kuashiria Uzinduzi Wa Mahakama Ya Watoto Leoi Jijini Mbeya. Katikati Ni Mwakilishi Wa Unicef Nchini, Stephanie Shanler Na Kushoto Ni Jaji Kiongozi Wa Mahakama Kuu Ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali. 
Kaimu Hjaji Mkuiu Wa Tanznaia Mhe. Porof. Ibrahim Juma Akikata Utepe Kuzindua Jengo La Mahakama Ya Watoto Leo Jijini Mbeya. 
Kaimu Jaji Mkuu Wa Tanznaia Akizungumza Wakati Wa Hafla Hiyo 
Kaimu Jaji Mkuu Wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma Akiwa Katika Picha Ya Pamoja Na Viongozi Wa Mahakama Ya Tanzania Mara Baada Ya Kuzindua Mahakama Ya Watoto Leo Jijini Mbeya 
Msajili Mkuu Wa Mahakama Ya Tanzania Mhe. Katarina Revokati Akiwa Pamoja Na Mwakilishi Wa Unicef Nchini, Stephanie Shanler Na Jaji Wa Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Mary Levira Wakati Wa Uzinduzi Wa Mahakama Ya Watoto. 
Jaji Mfawidhi Wa Mahakama Kuu Kanda Ya Mbeya Mhe. Noel Chocha Akizungumza Wakati Wa Hafla Hiyo 

No comments:

Post a Comment