Mwenyekiti wa kundi la makampuni ya Karimjee Jivanjee, Hatim Karimjee (kulia) akimkabidhi kifaa cha kusomea mmoja wa mwanafunzi aliyepata udhamini wa kusoma shahada ya uzamili katika uhifadhi wa mazingira ya wanyamapori katika bara la Afrika Zabibu Kabalika (kushoto) katika hafla iliyofanyika mkoani Arusha.
Mwenyekiti wa kundi la makampuni ya Karimjee Jivanjee akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuzindua masomo yaliyopendekezwa ya kozi ya uzamili katika uhifadhi wa mazingira ya wanyamapori mkoani Arusha, Nyuma Kulia ni Dr. Haydon wa chuo kikuu Glasgow kilichopo Scotland, akifuatiwa na Prof, Karoli Njau wa chuo cha sayansi na teknolojia cha Nelson Mandela, wengine ni wanafunzi waliopata nafasi ya masomo, Zabibu Kabalika (wa tatu kulia) na Evaline Munisi.
Mwenyekiti wa Kundi la makampuni ya Karimjee Jivanjee akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuzindua kozi ya uzamili iliyopendekezwa katika uhifadhi wa mazingira ya wanyamapori mkoani Arusha. kulia ni wanafunzi waliopata nafasi ya masomo ya shahada ya uzamili katika uhifadhi wa mazingira ya wanyamapori Evaline Munisi ( kwanza kulia) na Zabibu Kabalika.
Taasisi ya Karimjee Jivanje (KJF) imeongeza nguvu zaidi katika kuhifadhi na kusimamia mazingira ya bara la Afrika kwa kudhamini wanafunzi kutoka Tanzania kuendelea na masomo yaliyopendekezwa ya shahada ya uzamili katika eneo hilo.
Mwenyekiti wa heshima wa kundi la makampuni ya Karimjee Jivanjee nchini Tanzania, Hatim Karimjee alisema mpango huo wa masomo uliundwa na taasisi na mpaka sasa imejitolea kudhamini wanafunzi wawili mwaka 2016 na wanne mwaka huu.
Alisema Taasisi imetoa msaada wa dola 105,000 sawa na ( 236.2Millioni Tzs) mwaka jana ambapo wanafunzi wawili walichukua kozi ya shahada ya uzamili, na mwaka huu wanafunzi wanne wamedhaminiwa na taasisi ambapo imetoa msaada wa dola 210,000 sawa na (472.5 Miilioni Tzs) na ina mpango wa kutoa dola 180,000 sawa na (405Million Tzs) kwa ajili ya kudhamini nafasi za masomo mwaka ujao “Karimjee Jivanjee imefurahi kuzindua nafasi za masomo ya uhifadhi wa mazingira.
Wanafunzi hawa watajifunza masomo yalipondekezwa ya shahada ya uzamili ya usimamizi wa uhifadhi wa mazingira ya wanyamapori katika bara la Afrika. Tunapenda kushirikiana na chuo kikuu cha Glasgow nchini Scotland na chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo Arusha kuanzisha masomo ya shahada ya uzamili ambapo wanafunzi watasoma mwaka mmoja Glasgow na mwaka mmoja Mkoani Arusha. Wanafunzi hao watatambulika kama wanafunzi kutoka Karimjee,”
Alisema Karimjee. Alisema mpango huo wa shahada ya uzamili itakayofanyika ndani ya miezi 24 kipindi chote cha mwaka mmoja wanafunzi wataweza kujifunza masomo yao katika chuo kikuu Glasgow na mwaka mmoja nchini Tanzania watafanya utafiti wao katika chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo Arusha.
Kwa mujibu wa Bw. Karimjee, wanafunzi watakaofuzu katika masomo yao watatunukiwa tuzo ya shahada ya uzamili kutoka chuo kikuu cha Glasgow na shahada ya uzamili kutoka chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela. “Ni matumaini yetu kuwa kwa kusaidia wanafunzi kutoa nafasi za masomo itasaidia kuongeza idadi ya wataalamu wa kusimamia mazingira na masuala yanayohusiana na mabadiliko ya hali hewa,” alisema.
Programu ya Usimamizi wa kuhifadhi mazingira ya wanyamapori bara la Afrika ni programu ya kipekee ya uzamili inayotekelezwa pamoja na chuo kikuu cha Glasgow na Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela. Familia ya Karimjee ilianzisha taasisi mbalimbali za misaada kwenye miaka ya 1950 na kufanikiwa kujenga shule nyingi, hospitali, zahanati, misikiti na vituo vya huduma za jamii.
Moja ya misaada mkubwa kuwahi kutolewa ni ukumbi wa Karimjee, shule ya sekondari Usagara iliyoko Tanga (zamani iliitwa Karimjee School), kliniki ya Karimjee iliyopo Mnazi Mmoja na hospitali ya zamani ya Karimjee iliyopo Zanzibar. Wakati huo huo Karimjee imedhamini watanzania wengi kujifunza ndani na nje ya nchi.
Taasisi ya Karimjee Jivanjee ilisajiliwa mwaka 2009 na kuanza shughuli zake mwaka 2010 na hupata misaada kutoka Toyota Tanzania ambayo ni kampuni tanzu ya familia ya Karimjee. Taasisi inalenga kuwekeza katika elimu kama njia ya kuimarisha maendeleo ya kiuchumi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kifedha kwa wanafunzi wa sayansi kutoka Tanzania.
Taasisi imekuwa ikitoa nafasi za masomo kwa madaktari kuweza kuhitimu shahada ya uzamili katika matibabu ya saratani kwa watoto katika chuo kikuu cha Muhimbili (MUHAS). KJF pia inasaidia taasisi nyingine ikiwepo Young Scientists Tanzania (YST) na Read International. Mpango huu ni sehemu ya kujitolea ya KJF kusaidia sekta ya elimu nchini Tanzania na kuwekeza katika miradi ya kijamii inayoboresha maisha ya watu.
No comments:
Post a Comment