Saturday, July 1, 2017

HALMASHAURI YA MJI NJOMBE YAFUNGA MWAKA WA FEDHA 2016/2017 KWA KUTOA MISAADA KWA VITUO VYA WATOTO YATIMA COMPASSION NA UWEMBA MISSION


HYASINTA KISSIMA-NJOMBE

Halmashauri ya Mji Njombe imetoa misaada yenye thamani ya shilingi milioni mbili laki moja na arobaini kwa vituo viwili vya watoto yatima Compassion na Uwemba Mission ikiwa ni sehemu ya mapato ya ndani ya Halmashauri yaliyokusanywa katika robo ya nne ya mwaka wa fedha 2016/2017.

Akizungumza wakati akikabidhi misaada hiyo katika kituo cha watoto Yatima Compassion, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda amesema kuwa Halmashauri yake imejiwekea utaratibu wa kuhakikisha kuwa katika kila robo ya mwaka wa fedha inatenga fedha kwa ajili ya kusaidia jamii ya wenye uhitaji wakiwemo watoto yatima ili kuonesha upendo lakini pia kuijengea jamii tabia ya kuonesha upendo na kusaidia wale wote wenye mahitaji mbalimbali.

“Kila tunapokusanya mapato imekua ni utaratibu wa Halmashauri kwa kushirikiana na idara ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa jamii kuangalia makundi yenye uhitaji na kuona ni kwa namna gani tunayaongezea nguvu zaidi ili nao waweze kujikwamua kimaisha na kuona kuwa wao pia ni sehemu ya jamii inayotambulika na kuheshimika. 
 
Tumekua tukifanya hivi mara kwa mara na leo tunapofunga mwaka na kuanza mwaka mpya wa fedha tumeona kwa kile kidogo tulichokipata tuweze pia kugawana na watoto hawa na furaha yangu imeongezeka kwani mpaka sasa Halmashauri yangu tumefanikiwa kukusanya mapato kwa asilimia mia na kuvuka lengo .”Alisema Mwenda.

Kwa upande wake Afisa Ustawi Halmashauri ya Mji Njombe Hosea Yusto amesema kuwa kumekuwa na matukio mengi ya wazazi kuwatelekeza na kutowajali watoto wao matukio ambayo yamekuwa yakiongeza idadi ya watoto yatima katika vituo, watoto wa mitaani na amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanalea, kuwalinda na kuwa karibu na watoto wao ili kuepusha matukio mbalimbali yakiwemo ya ubakaji kwa watoto wadogo.

Akizungumza kwa niaba ya watoto wanaolelewa katika kituo cha yatima Compassion Imelda Msola amesema wanaishukuru Halmashauri kwa kuendelea kuwapatia misaada ya mara kwa mara, na misaada waliyopata hususani vifaa vya shule vitawasaidia katika kipindi hiki wanapoenda kuanza muhula mpya wa masomo na wameomba wadau mbalimbali kuendelea kuwasaidia ili waweze kufanikisha malengo yao kimaisha.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na Sukari, Mafuta, chumvi, Unga, Sabuni za kufulia, Mafuta ya Kujipaka nguo za watoto, Nepi, nguo za watoto, maziwa ya Kopo, dawa za meno, miswaki, daftari, kalamu. 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda wa kwanza kulia akiwa amembeba mtoto anayelelewa katika kituo cha watoto Uwemba Mission.Kulia kwake ni Afisa Maendeleo na Afisa Ustawi wa Jamii Hosea yusto
Mtoto Imelda Msola kutoka kituo cha watoto Compassion akitoa mkono wa asante kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda mara baada ya kukabidhiwa misaada mbalimbali katika kituo hicho
Misaada iliyokabidhiwa katika kituo cha watoto Uwemba Mission.

No comments:

Post a Comment