Friday, June 2, 2017

WAZIRI MKUU: TUMEBAINI MADAI HEWA YA BILIONI 21/-


* Ni kwenye malipo ya mawakala wa mbolea, awali yalifikia sh. bilioni 65.
*Akiri kukutana nao, asema wenye madai halali wote watalipwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imebaini madudu katika uhakiki wa madeni ya mawakala wa mbolea kwa sababu baadhi yao hawakuwa waaminifu.

“Tulipoanzisha mfumo wa kutoa pembeje kwa njia vocha kwa kuwatumia mawakala kupeleka pembejeo vijijini, tulibaini kuwa baadhi yao walikuwa siyo waaminifu. wakiorodhesha majina ya wakulima na kuandika kuwa wamewapa madawa napembejeo wakati hawapo.”

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Juni mosi, 2017) wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Morogoro), Bi. Devotha Minja kwenye kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu bungeni mjini Dodoma.

Bi. Minja alitaka kujua ni kwa nini Serikali haijawalipa mawakala hao hadi sasa licha ya kuwa inatambua kwamba walifanya kazi ya kusambaza pembejeo hizo.

“Tulijikuta tuna deni la shilingi bilioni 65. Nilipokutana na mawakala wiki mbili zilizopita, niliwaahidi kwamba tutawalipa lakini ni lazima watupe muda tufanye uhakiki ili kubaini kama kweli pembejeo zilifika. Kati ya shilingi bilioni 35 za madeni ya awali, imebainika kuwa sh. bilioni 6 tu ndiyo za halali. Na bado kuna sh. bilioni 30 nyingine zinafanyiwa uhakiki,” amesema Waziri Mkuu.

“Tumewasihi waendelee kuwa wavumilivu ili tukamilishe zoezi hili na tujue Serikali inadaiwa kiasi gani. Napenda niwahakikishie kuwa kazi hiyo inaendelea na tuko kwenye hatua za mwisho, na wale wote wenye madai halali ambao ni waaminifu watalipwa na Serikali.”

Akijibu swali la nyongeza ni kwa nini Serikali isiharakishe malipo hayo kwani kuna baadhi nyumba zao zimepigwa mnada na mabenki, na wengine wamepoteza maisha kwa sababu ya mshtuko, Waziri Mkuu alisema siku ya mwisho ya kufanya uhakiki ilikuwa jana Mei 31 kwa hiyo anasubiri taarifa kutoka Halmashauri zote kupitia kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Alisema wenye mabenki wameisikia kauli ya Serikali kwa hiyo hawana sababu ya kukimbilia kuuza mali za mawakala kwa njia ya mnada kwani hatua zinazochukuliwa na Serikali ni nzuri na zimeokoa mabilioni ya fedha.

Alisema watumishi wote wa umma waliohusika kwenye ubadhirifu huo, watachukuliwa hatua za kinidhamu.Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka wawekezaji nchini wasihofu hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhusiana na usafirishaji wa mchanga wenye madini kwenda nje ya nchi.

Akijibu swali ya Bw. Emmanuel Mwakasaka, Mbunge wa Tabora “Ninawasihi wawekezaji wasiwe na shaka kwa sababu lengo la Serikali ni jema. Tunataka tujiridhishe kuwa kuna nini hasa ndani yake. Hatuna jambo ambalo tumelifanyia kazi isipokuwa kwa watu wetu wa ndani,” amesema.

“Kila kitu kitakuwa wazi, ninawaomba Watanzania na wawekezaji wawe watulivu. Kazi tunayoifanya ni kwa manufaa ya Watanzania. Nia yetu ni kulinda rasilmali za nchi yetu, na hadi sasa bado hatujatoa taarifa rasmi, bado tunasubiri taarifa ya kamati ya pili,” alisisitiza.

Akijibu swali la nyongeza ni mikakati gani Serikali imeweka kwa kufunga mashine kwenye chanzo ili kuhakikisha tatizo hilo haijirudii tena, Waziri Mkuu alisema Serikali imekuwa inapokea wawekezaji ambao wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye eneo hilo. Alisema zamani kulikuw ana usiri wa kupata wawekezaji wa aina hiyo lakini hivi sasa kumeanza kuwa na uwazi katika eneo hilo.

“Tutaamua kujenga mashine zetu hapa hapa nchini au kuwakaribisha wawekezaji katika eneo hili au kuona uwezo wa Serikali ili tuweze kutatua tatizo la kupoteza mchanga ambao tunalazimika kuupeleka nje ya nchi kwa ajili ya uyeyushaji wa madini yaliyomo,” alisema.

Waziri Mkuu alisema hatua zilizochukuliwa na Serikali ni mwitikio wa kilio cha siku nyingi cha wananchi wa maeneo husika pamoja na waheshimiwa wabunge ambapo Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alimtuma aende Kahama kuchukua sampuli za mchanga na alipompa taarifa, Rais akaunda tume mbili za kufuatilia suala hilo.

No comments:

Post a Comment