Tuesday, June 27, 2017

Watanzania washauriwa kuchangamkia fursa ya kwenda kuhiji Israel

Watanzania  wameshauriwa kuchangamkia fursa ya kutembelea  maeneo matakatifu nchini Israel kwa gharama nafuu inayokadiriwa kuwa kati ya nafuu inayokadiriwa kuwa kati ya Dola za Kimarekani 1700 na 1800. 
 Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bibi Devota Mdachi,  amesema jijini jana kuwa wadau wa utalii wa Israel wangependa kuona Watanzania wanatembelea Israel. 
Bibi Mdachi akiongozana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki ambaye alikuwa kiongozi wa msafara,  walitembelea Israel kwa siku tatu, walikutana na na wadau wa sekta ya utalii na kuwaeleza  vivutio vilivyopo nchini.
“Tumetembelea maeneo mengi ya kiroho ikiwemo miji ya Nazareth na Jerusalem, wenyeji wetu wamenipa ujumbe kuwa wanahitaji Watanzania waende wakahiji katika maeneo hayo kwa bei nafuu inayokadiriwa kuwa kati ya Dola za Kimarekani 1700 na 1800. 
“Fursa hii ni nzuri tafadhali tusiiache kwa sababu mbali ya hija lakini kuna mambo mengi mengine.  Watakaokwenda watakutana na raia wa mataifa mengine watawauliza kuhusiana na Tanzania,  maana yake mtageuka mabalozi wetu na kuvutia watalii wengi zaidi,” alisema Bibi. Mdachi.

Alibainisha kuwa kiasi hicho cha Dola 1700 au 1800 kinahusisha nauli ya kwenda na kurudi, malazi pamoja na ziara ya maeneo matakatifu ndani ya miji husika. 
“Kampuni ya Another World imeahidi ifikapo Agosti mwaka huu wataleta watalii kutoka Israel watakaotembelea maeneo ya Hifadhi ya Katavi, Mahale, Ngorongoro na Zanzibar.

Mmiliki wa kampuni ya Another World, Bw Shlomo Carmel ameahidi kuleta watalii zaidi ya 2000 kati ya Agosti na Disemba mwaka huu. 
Vilevile kuna wawekezaji katika sekta ya hoteli za viwango vya kimataifa wameahidi kuja kuwekeza nchini, kifupi imekuwa ni ziara yenye tija kwetu sote,” alibainisha Bibi. Mdachi. 
Balozi wa Tanzania nchini humo Balozi Job Massima, amesema  mbali ya ugeni wake katika nchi ya Israel  amebaini kuna kuna fursa nyingi za kiutali zinazoweza kunufaisha pande zote. 
“Huu ni mkusanyiko wangu wa kwanza hapa nchini tangu niwasilishe hati zangu za ubalozi, lakini nimeona namna Waisrael wanavyoipenda Tanzania, nami nimeona namna vivutio vilivyopo hapa vinavyofaa kwa Watanzania kuja kutalii. 
“Tunasema hii ni nchi takatifu, waumini wa dini zote duniani wanaguswa na namna moja au nyingine kuja kuitembelea. Hivyo nitatumia nafasi yangu ya ubalozi kuwa kiunganishi kwa Tanzania na Israel kwenye sekta hii muhimu ya utalii,” amesema Bw. Massima. 
Utalii ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya mapato nchini,  ambapo mwaka jana sekta ya utalii iliingiza kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 2 ikiwa ni sawa na Sh Trilioni 4, mwaka 2015 iliingiza Dola bilioni 1.9. 

Kiwango hicho cha mapato kiliifanya sekta ya utalii kuchangia asilimia 17.5 ya pato la taifa katika bajeti ya mwaka 2016/17 pamoja na kuingiza asilimia 25 ya fedha za kigeni.

No comments:

Post a Comment