Friday, June 9, 2017

NDAMA ahukumiwa kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya mil. 200


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu Mfanyabiashara Shabani Hussein (44) maarufu kama "Ndama mtoto ya Ng'ombe" kulipa faini ya milioni 200 au jela miaka mitano baada ya kukiri shtaka la sita la kutakatisha fedha ambazo ni dola za Marekani 540,000.



Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi, Mkuu wa mahakama hiyo Mhe. Victoria Nongwa.
Kabla ya hukumu hiyo kusomwa, upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Christopher Msigwa alimsomea maelezo ya awali (PH), Ndama dhidi ya shtaka lake hilo na kukiri.

Hatua hiyo ya Ndama kusomewa hukumu katika shtaka moja tu la utakatishaji wa fedha kati ya matano yanayomkabili limekuja baada ya wiki iliyopita kuomba kukumbushiwa mashtaka yake na kukiri shtaka hilo la utakatishaji wa fedha.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu Nongwa amesema mahakama imezingatia hoja za upande wa mashtaka na ule wa utetezi ambapo upande wa mashtaka uliiomba mahakama kwa mujibu wa sheria ya kutakatisha fedha kifungu cha 13 (a)cha Sheria ya kuzuia utakatishaji fedha, kumpa adhabu kali mshitakiwa kwa kuwa makosa hayo yanalenga kudidimiza uchumi wa nchi.

Amesema, mshitakiwa anastahili faini kwa kuwa ameipunguzia garama mahakama kuhusu shughuli za uendeshaji wa kesi hiyo ikiwemo gharama za kuleta mashahidi katika shtaka hilo.
Ameongeza kuwa, Sheria hiyo ipo kwa ajili ya kuonesha kuwa makosa kama hayo hayatakiwi kumnufaisha mkosaji hivyo, atatakiwa kulipa faini ya milioni 200 na asipolipa ataandikiwa hati ya kifungo cha miaka mitano jela.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili Msigwa alidai hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshitakiwa na ni rai ya Jamhuri kwamba mahakama imuadhibu mshitakiwa kuzingatia sheria ya kuzuia utakatishaji fedha.
Wakili wa utetezi, Wabeya Wakung'i aliomba mahakama impunguzie adhabu mshitakiwa kwa kuwa ni kosa lake la kwanza, familia yake inamtegemea pia mshitakiwa hakuonesha usumbufu na kwamba kukiri kwake kosa ni ishara ya kujutia kosa.
Katika shtaka hilo la sita, Ndama anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014, Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini pekee wa Kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye Benki ya Stanbic alijihusisha moja kwa moja kwenye uhamishaji wa dola za Marekani 540,000 na kuzitoa huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu la kujiapatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Katika maelezo ya awali, Wakili Msigwa alidai Ndama ni mkazi wa Mbezi Beach na kwamba Mei 14, 2013, Bushoboka Mutamola na Majibu Taratibu walisajili Brela Kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment Co. Limited na kupata hati ya usajili namba 992449 kwa ajili ya kujishughulisha na biashara ya madini.
Alidai Septemba 16,2013 kampuni hiyo ilifungua akaunti ya fedha za kigeni Benki ya Stanbic tawi la Viwanda na kupewa akaunti 9120000085152.

Imedaiwa kuwa, wakati wa ufunguzi wa akaunti hiyo, Ndama alijitambulisha kama Mwenyekiti mtiaji saini pekee kwenye benki hiyo ambapo aliwasilisha nyaraka mbalimbali ikiwemo barua ya utambulisho wa Kampuni, leseni ya biashara, namba ya utambulisho wa biashara (TIN) ambazo zilipokelewa mahakamani hapo.
Pia inaelezwa, Februari, 2014 Ndama na wanahisa wenzake waliingia makubaliano na Kampuni ya Australia iitwayo Trade TJL PTYL Limited wakijaribu kuonesha kuwa watauziana dhahabu kilogramu 207 zenye thamani ya dola za Marekani Milioni 8.2.
Wakidai watatimiza masharti ya mikataba waliandaa nyaraka za uongo ambazo ni kibali cha kusafirisha madini kwenda Australia, waliandaa kibali cha Umoja wa Mataifa kuonesha kuwa dhahabu hizo hazina jinai yoyote namba 28092 iliyoandaliwa Februari 20,2014, kuonesha wamelipa dola za Marekani 331,200 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama kodi ya usafirishaji " alidai Msigwa.
Pia alidai Ndama alimtaarifu mlipaji ambayo ni Kampuni ya Trade, kulipa fedha kupitia akaunti hiyo yenye jina la Muru ambapo baadae kampuni hiyo iliamini taarifa hizo na kulipa dola za Marekani 540,390 kwa tarehe tofauti.

Licha ya kukubali mashitaka hayo, Ndama alikana makosa mengine yakiwemo ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

baada ya ndama kukiri shtaka hilo la utakatishaji wa fedha ambalo halina dhamana, Hakimu Nongwa amemsomea masharti ya dhamana katika mashtaka mengine yaliyobakia ya kughushi na kutoa nyaraka za uongo, ambapo ametakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini dhamana ya milioni 600 au hati isiyohamishika ya kiasi hicho. 
Kesi hiyo itatajwa tena Juni 16 mwaka huu. 

Ndama amebakiwa na mashtaka matano yakiwemo manne ya kughushi na moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

No comments:

Post a Comment