Monday, June 12, 2017

MAFUNZO YA AWALI YA KANUNI ZA UKOPESHAJI KATIKA KILIMO YAENDESHWA

 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB), Bw. Francis Assenga (kulia) akihimiza jambo kwa washiriki wa Mafunzo ya Awali ya Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo. Mafunzo hayo ya siku sita yanafanyika kati ya TADB, NABAD na MIVARF, yanaendelea katika Hoteli ya Beach Comber, Dar es Salaam.

Na mwandishi wetu,
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na  Benki ya Taifa ya Kilimo na Maendeleo Vijijini India (NABAD) na Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) zimeanza kutoa Mafunzo ya Awali ya Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo.

Mafunzo hayo ya siku sita (6) yanalenga kuwajengea uwezo watoa huduma hasa kutoka mabenki na taasisi za kifedha nchini kuweza kutoa huduma kwa wakulima kwa wakati na kuzingatia tija wakulima nchini ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

Akifungua mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa TADB alisema kuwa katika kuunga mkono kwa vitendo juhudi za serikali kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania, TADB imeamua kuwajengea uwezo wadau kutoka mabenki na taasisi za kifedha nchini kwa kushirikiana na  NABAD na MIVARF ili kuweza kutoa huduma kwa uhakika ili kuwakomboa wakulima nchini.

“Mafunzo haya yanalenga kuunga mkono juhudi za Serikali ili kuharakisha  mapinduzi na maendeleo katika Sekta ya Kilimo, ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini na pia kutoa kiasi cha zaidi ya  asilimia 65 cha mali ghafi kwa ajili ya viwanda vya nchi,” alisema.

Bw. Assenga aliongeza kuwa TADB imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia kuyajengea uwezo mabenki na taasisi za kifedha ili kuchagiza upatikanaji na utoaji wa fedha ili kusaidia maendeleo ya kilimo nchini.

Kwa upande wao wakufunzi wa mafunzo hayo kutoka NABAD, walisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watoa huduma watoaji wa mikopo kwa upande wa kilimo kufahamu kwa undani vigezo vya kuzingatia wakati wa utoaji wa mikopo hiyo.
 Meneja Msaidizi wa Mafunzo kutoka NABAD, Dkt. R.S. Reddy akizungumza kuhusu mafunzo hayo. Mafunzo hayo ya siku sita yanaendeshwa kwa pamoja kati ya TADB, NABAD na MIVARF.
 Meneja Msaidizi wa Mafunzo kutoka NABAD, Bw. M.R. Gopal akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa Mafunzo ya Awali ya Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo. Mafunzo hayo ya siku sita yanaendeshwa kwa pamoja kati ya TADB, NABAD na MIVARF.
 Washiriki wa Mafunzo ya Awali ya Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo wakifuatilia kwa makini ufunguzi wa mafunzo hayo. Mafunzo hayo yanafanyika katika Hoteli ya Beach Comber, jijini Dar es Salaam.
 Mshauri wa Kiufundi wa MIVARF, Bw. Ravi Malik (kushoto) akimkabidhi zawadi kutoka NABAD Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB), Bw. Francis Assenga (kulia). 
Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment