Friday, June 9, 2017

DKT.KIKWETE -VIWANDA VYA KUSINDIKA MATUNDA VISIWAKANDAMIZE WAKULIMA

Rais mstaafu wa awamu ya nne dk .Jakaya Kikwete akishika Mwenge wa Uhuru uliopita kutembelea shamba lake la mananasi lililopo Bago -Kiwangwa Bagamoyo .(Picha na Mwamvua Mwiny.
Rais mstaafu wa awamu ya nne dk .Jakaya Kikwete na mkewe mama Salma Kikwete wakikimbiza Mwenge wa Uhuru uliopita kutembelea shamba lake la mananasi lililopo Bago -Kiwangwa Bagamoyo .
 
Kongozi wa mbio za mwenge kitaifa Amor Hamad ,akizungumza baada ya kupata taarifa ya ujenzi ,wa kiwanda cha kusindika matunda cha sayona kilichopo Mboga – Msoga Chalinze ,kutoka kwa afisa uhusiano wa kampuni mama ya MMI ,Abubakar Mlawa
………………………….


Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo 

RAIS mstaafu wa awamu ya Nne ambae pia ni mkulima wa tunda la mnanasi ,dk.Jakaya Kikwete,amewataka wamiliki wa viwanda vya matunda kuacha kuwakandamiza wakulima kwa kununua matunda kwa gharama ya chini .

Amesema viwanda hivyo vinasaidia kupatikana kwa masoko ya ndani lakini vimekuwa havina uwiano wa gharama zinazolingana na maumivu anayoyapata mkulima.Aidha dk. Kikwete ameeleza kumekuwa na changamoto ya kushuka kwa soko kwa wakati mwingine hali inayokuwa ikisababisha wakulima kupata hasara kwa matunda kuoza yakiwa mashambani .

Akitoa taarifa ya shamba lake la mananasi lililipo Bago-Kiwangwa wilayani Bagamoyo ,wakati Mwenge wa Uhuru ulipokwenda kutembelea shamba hilo ,alisema kilimo cha matunda kina tija endapo utalima kisasa na kuwa na soko la uhakika .

Kikwete alieleza ,viwanda vya usindikaji matunda mbalimbali ,vinapaswa kumjali mkulima ambae amekuwa akipata shida na kutumia gharama kubwa kuandaa shamba .“Wakati utafika watakosa matunda ,kutokana na gharama yao hailipi ,wakulima wa matunda tushindwa kukubali kuuza kwa bei ya chini ambayo hailipi ” alifafanua .

Rais huyo mstaafu ,alimwambia kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa 2017 ,Amor Hamad Amor ,kuwa mananasi huvunwa baada ya miezi 18 tangu kupandwa .“Bei ya mauzo hutegemea wanunuzi na wachuuzi wadogowadogo ambao hununua kwa ukubwa wa nanasi sh 400 hadi 800 inapovunwa kutoka shambani .

Dk.Kikwete alisema ,shamba lake lina ukubwa wa hekari 200 ambapo hekar 64 ndizo zimelimwa na zipo kwenye hatua ya palizi .Alisema pia wana chama chao cha wakulima wa matunda Kiwangwa wana ambapo wanamatayarisho ya miche mipya ya kuweza kuuzika nje za nchi.

“Mwenge kwa kuangaza shambani kwangu ni ishara ya nuru ,basi nitapata neema baadae,nashukuru kwa kuja kutembelea shamba langu kujionea shughuli nazofanya baada ya kustaafu” alisema .Kiongozi huyo pia alipita kujionea shughuli za ujenzi wa kiwanda cha Sayona kinachomilikiwa na kampuni MAMA ya MMI steel,kilichopo kata ya Mboga.

Afisa uhusiano wa kampuni za MMI steel ikiwemo Sayona,Abubakar Mlawa ,alimwambia kwamba ,kiwanda cha Sayona kimefikia asilimia 70 ya ujenzi na mwezi novemba mwaka huu kinatarajia kuanza kazi.Alieleza kiwanda hicho,kwasasa kimeajiri watu 100 wakiwemo mafundi ujenzi na kitakapoanza kazi kitaajiri watu 800.

Mlawa alisema,mahitaji makubwa ni matunda zaidi ya tani tisa kwa siku, hasa maembe,nyanya na matunda mengine hivyo wakulima wa matunda wachangamkie fursa hiyo.Alisema kiwanda cha Sayona ni moja ya uwekezaji mkubwa mkoani Pwani,na kinalenga kugharimu dollar mil.55 sawa na sh.bil.120 katika ujenzi wake.

Nae kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa ,Amor Hamad ,alipongeza serikali kwa kuondoa ushuru wa mazao ya matunda na kuongeza kodi kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi hali inayoonyesha taifa kutaka kukuza soko la ndani.Alimpongeza rais mstaafu wa awamu ya nne Dk. Kikwete na kuwataka  wakulima wa zao hilo kuiga mfano wake wa kulima kwa tija .

Amor aliwataka wananchi kujishughulisha kwa kufuata nyayo za waasisi wetu akiwemo Kikwete na waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda .“Niipongeze serikali kwa jitihada hizo kwani inaonyesha serikali inataka kukuza soko la ndani la nchi na wakulima kuthaminika  ili kujiletea maendeleo.

Mwenge wa Uhuru june 10,unatarajia kukabidhiwa mkoani Morogoro ,ukiwa Chalinze na Bagamoyo umepitia miradi iliyogharimu bil.128

No comments:

Post a Comment