Thursday, May 4, 2017

WANAFUNZI ARUSHA WAPEWA ELIMU YA MADINI

Wanafunzi wa Shule wa Sekondari ya Arusha wakimsikiliza Mkufunzi kutoka  Taasisi ya  Gemological Insitute of America (GIA) , Elizabeth  Bokaba (hayupo pichani). Wanafunzi hao wamepata mafunzo kuhusu mafunzo ya Jimolojia.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Arusha wakifuatilia mafunzo kwa vitendo kuhusu elimu ya madini ya vito yanayopatikana chini, wakati wa Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito yanayoendelea jijini Arusha.
Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Eric Mpesa akiwaeleza jambo wanafunzi wa Shule ya Sekondari Arusha wakati wa mafunzo ya Jemolojia yaliyotolewa na Taasisi ya GIA wakati wa Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Vito Arusha yanayoendelea jijini Arusha.
Mkufunzi kutoka Taasisi ya Gemological Institute of America (GIA), Elizabeth  Bokaba, akiwafundisha elimu ya Jemolojia wanafunzi wa Shule ya Sekondari Arusha.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Arusha wakiangalia madini ya Tanzanite katika Banda la Kampuni Gliters Gems Limited  wakati walipotembelea mabanda ya maonesho baada ya kupata mafunzo ya Jemolojia.
Mfanyabiashara wa Madini wa Kampuni ya Abdulhakim Mulla akiwaonesha wanafunzi wa Shule ya Sekondari Madini ya Tanzanite. Mulla alitumia nafasi hiyo kuwafundisha tofauti ya madini yaliyonakishiwa na ambayo bado hayajakatwa.

Na Asteria Muhozya, Arusha.

 Jumla ya Wanafunzi 55 kutoka  Shule za Sekondari za Arusha Day, Arusha Sekondari na Wining Sprit wenye  umri kati ya miaka 12- 15 wamepatiwa mafunzo ya Jemolojia katika Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito yanayoendelea jijini Arusha.

Mafunzo hayo yanayojulikana kama GemKids yametolewa na  Wakufunzi kutoka  Taasisi ya Gemological Institute of America (GIA) na kuratibiwa na Kituo cha Jimolojia  Tanzania  Cha Arusha, (TGC).

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Mratibu wa TGC,  Erick Mpesa amesema kuwa, mafunzo hayo  ya Jemolojia, yanalenga kuwapa ufahamu wanafunzi ili kuwa na uelewa wa madini ya vito, kujua matumizi yake, kuyatumia na baadaye kuwawezesha  kuingia katika biashara ya madini huku wakiwa na uelewa mzuri na rasilimali hizo ambazo zinapatikana katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumzia mahusiano ya TGC na Taasisi ya GIA, Mpesa amesema kuwa, TGC imelenga kuendeleza ushirikiano na Taasisi hiyo kwa siku za baadaye hususani katika masuala ya utafiti na mafunzo na kuongeza kuwa, uhusiano uliopo baina ya taasisi hizo, umewezesha baadhi ya watumishi wa kituo hicho kupata mafunzo katika taasisi hiyo.

Kuhusu mpango wa TGC kutoa mafunzo  kwa Watanzania, alisema kuwa, tayari kupitia Maonesho ya Vito ya Arusha, kituo hicho kuanzia mwaka 2014 kimetoa mafunzo ya ukataji na unga'rishaji wa madini ya vito kwa  jumla wanawake 47 na kueleza kuwa,  hivi sasa jumla ya wanawake 18 wanaendelea na mafunzo hayo na wanatarajiwa kuhitimu ifikapo tarehe 19 ya mwezi huu.

"Kutokana na changamoto ya ajira wahitimu wetu tunawashauri kujiunga katika vikundi ili kuwawezesha kupata ruzuku pale zinapotolewa na Serikali. Hii inawezesha rasilimali inayotumika kuwafundisha kuwawezesha vijana hawa isipotee bure. Lengo letu ni kuwawezesha waweze kujiajiri na kuajiriwa," alisisitiza Mpesa.

Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Vito ya Arusha yalianza  rasmi tarehe 3 Mei na yanataajiwa kufungwa tarehe 5 Mei,2017. 

No comments:

Post a Comment