Wednesday, May 31, 2017

RC Rukwa atoa tahadhari ya Ebola kwa wananchi wa Kirando

Katika kuhakikisha Mkoa wa Rukwa Upo salama kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola yatakayoweza kujitokeza, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amefanya ziara ya siku tatu katika mwambao wa ziwa Tanyangika kwenye Kata ya Kirando, Kabwe na Kasanga vijiji ambavyo vipo jirani na nchi  ya DRC ili kujionea namna Halmashauri ya Nkasi na Kalambo zilivyojipanga kuhakikisha kuwa ugonjwa huo hautii mguu katika Mkoa na nchi kwa ujumla.

Ziara hiyo aliianza siku ya Ijumaa tarehe 26 hadi 28. 05. 2017 mara baada ya kumaliza kumalizika kwa mafunzo ya siku tatu yaliyohusu utumaji wa taarifa za magonjwa kwa kieletroniki (e-idsr) yenye kusisitiza tahadhari ya ugonjwa wa ebola uliopo katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yaliyotolewa kwa wahudumu wa afya wa Serikali na Sekta binafsi kwa Halmashauri mbili za Manispaa ya Sumbawanga na Sumbawanga vijijini.

Mafunzo ya awamu ya pili yanatarajiwa kumalizika tarehe 31. 05. 2017 kwa Halmashauri za Kalambo na Nkasi ikiwa ni muendelezo wa awamu ya kwanza kwa Halmashauri ya Sumbawanga Vijijini na Manispaa ya Sumbawanga yaliyoisha tarehe 26. Mwezi wa tano.

Ili kujiridhisha na maandalizi ya Halmashauri zinazopakana na nchi za jirani yaani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pamoja na Zambia Mkuu wa Mkoa alipita katika bandari maarufu za pwani ya ziwa Tanganyika na kuongea na vyombo vya usalama ikiwemo uhamiaji, Sumatra, TRA, jeshi la polisi, jeshi la wananchi, maafisa forodha pamoja na maafisa afya kutoka Wilayani.

Pia Mh. Zelote aliongea na viongozi wa serikali za vijiji na kata wakiwemo madiwani, watendaji wa kata na vijiji, wenyeviti wa vijiji na vitongoji, maafisa ugani wa kata na vijiji, maafisa afya wa kata na vijiji na kufanya mikutano ya hadhara ili kuwapa wananchi ujumbe aliokwenda nao katika kuhakikisha ugonjwa huo haunusi katika mkoa wa Rukwa na nchi ya Tanzania.
Pamoja nae Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Boniface Kasululu, Mratibu wa Chanjo Mkoa Gwakisa Pamoja na Afisa kutoka Wizara ya Afya wa usimamizi na ufuatiliaji Solomon Mushi, Mkuu wa Wilaya, makatibu tawala wa wilaya pamoja na kamati za ulinzi na usalama za Wilaya.

Katika kila Wilaya aliyopita Mh. Zelote alihakikisha anapewa taarifa za maandalizi ya Wilaya na kisha kwenda kwenye mipaka ili kujionea kwa macho yake maandalizi hayo na pia kuongea na wananchi wanoishi karibu na mipaka hiyo.

Wakati akiwa kwenye ziara hiyo Mh. Zelote alikuwa akisisitiza utayari pamoja na kujihadhari kwa viongozi wa serikali za vijiji na kata na pia kwa vyombo vya usalama vya maeneo hayo ya mipakani.

Katika suala la utayari Mh. Zelote Alisema kuwa wananchi wanapaswa kuelimishwa juu ya athari ya ugonjwa huo na namna ya kujikinga nao ikiwa ni pamoja na kuelezwa dalili za ugonjwa na njia za maambukizi ya ugonjwa huo na kuwasisitiza wananchi kwenda zahanati pindi wanapojiskia kuumwa na sio kukimbilia kwenye maduka ya dawa na kuagiza vidonge bila ya kujua ugonjwa anaoutibu.

Pia katika kusisitiza hilo Mh. Zelote aliwasihi wananchi kutokimbilia kwa waganga wa kienyeji pindi wanapoumwa na badala yake wakimbilie kwa wataalamu wa afya kwenye zahanati ama vituo vya afya. Na kuwaonya kuwa kupitia hizi taarifa za ugonjwa wa ebola kunaweza kukajitokeza matapeli ambao watajitangaza kuutibu ugonjwa huo jambo ambalo si kweli, hivyo aliweka msisitizo kuwa ugonjwa wa Ebola hauna Tiba.

“Mtu yeyote atakayejiskia vibaya basi haraka akimbilie kwenye zahanati ama kituo cha afya na sio kwa mganga wa kienyeji, na mjiepushe mbali  sana na matapeli wanaotibu watu vichochoroni ama wanaosema dawa ya Ebola ipo,…. Hakuna,” Mh. Zelote alieleza.

Pamoja na hayo Mh. Zelote alionya kuwa katika kusimamia jambo hilo hatakuwa na utani, dhihaka ama masihara kwayeyote atakaekiuka taratibu zilizowekwa ili kujihadhari na ugonjwa huo kuingia katika mkoa wa Rukwa.

“Mimi nafahamu kwamba watu wanaoishi humu kwenye mipaka wameoa ama kuolewa katika nchi za jirani, na kwamba watanzania utamaduni wetu ni ukarimu kwa wageni lakini katika hili tupunguze ukarimu mpaka jambo hili liishe, na yeyote atakayegundulika anamhifadhi mgeni kinyume na taratibu, huyo ni mhalifu,” Mkuu w Mkoa alisema.

Katika kuonesha athari kubwa inayoweza kupatikana endapo uginjwa huo utapenya katika nchi yetu Mh. Zelote alieleza kuwa gharama za kumshughulikia mgonjwa mmoja ni kubwa sana na kuongeza kuwa endapo ugonjwa huo unathibitishwa kwenye nchi Fulani basi tatizo hilo si la nchi hiyo tu ni la dunia nzima.

“Nguo inayotumika kumshughulikia mtu mmoja inauzwa milioni 10 na kwa wenzetu huko afrika ya magharibi Ivory Coast ambako walikumbana nao watu 11,000 walifariki, wakiwemo madaktari ambao walikuwa wakiwauguza wagonjwa, mtu mmoja tu akiupata basi kijiji kizima kinafungwa hakuna mtu kuingia katika kijiji hicho wala kutoka,” Mh. Zelote alisisitiza.

Lakini pia aliwatoa hofu wananchi na kuwaambia kuwa mpaka sasa Tanzania hakuna mgonjwa hata mmoja wa Ebola.

Nae Daktari wa Mkoa Dkt. Kasululu alisema kuwa tangu ugonjwa huo kutolewa taarifa na Wizara ya Afya tarehe 12. 05. 2017 watu watatu wlikuwa wamefariki na wengine 12 walikuwa wako chini ya uangalizi lakini hadi kufuikia tarehe 25. 05. 2017 idadi ya wagonjwa iliongezeka hadi kufikia wagonjwa 45 na kuongeza kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka kadiri siku zinavyokwenda mbele.

“Idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeak kila kukicha hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunajiandaa na kujihadhari kweli, maana wagonjwa hawa wapo kwenye misitu ambapo usafiri wa kawaida haufiki isipokuwa Helkopta na pikipiki, hivyo wagonjwa wanaweza kuwa wengi na bado hawajajulikana,” Dkt Kasululu alisisiza.

Nae Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Dk. Makundi Maige alielezea mikakakti ya Halmashauri ya Nkasi namna ilivyojipaga kuhakikisha wanakaa mbali na ugonjwa hatari wa Ebola.

“ Wilaya imeainisha kata tatu za Kirando, Kabwe na Wampembe ambazo zimetengwa kwaajili ya kupokea wageni kutoka nchi za jirani, tukifahamu kuwa katika mwambao wa Ziwa Tanganyia kuna Kata 10 ambazo ugonjwa huu unaweza kuingia kwa urahisi, ambazo ni Kabwe, Kirando, Wampembe, Itete, Kipili, Mkinga, Korongwe, Ninde, Kizumbi na Kala,” Dk. Makundi aliainisha.

Katika kubainisha upokezi wa wageni hao Dk. Makundi alisema kuwa kituo cha Wampembe kitapokea wageni wanoelekea kijiji cha Kilambo hadi Msamba, Kituo cha Kirando kitapokea wageni wanaoelekea kijiji cha Ninde hadi Kazovu na kituo cha Kabwe kitapokea wageni wanaoelekea kijiji cha Utinta hadi Kalila.

Na kuongeza kuwa wageni wote kutoka nchi za jirani watalazimika kupitia katika vituo hivyo na sio kuingia kiholela kama ilivyozoeleka na kabla ya kuendelea na safari zao watakuwa wakichunguzwa afya zao.

Kwa kuzingatia namna ugonjwa huo unavyoenea Wilaya imetenga eneo maalum kwaajili ya matibabu ili kuepuka kuchanganya wagonjwa watakaobainika kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola.

Pamoja na hayo Wilaya imejipaga kuzizungukia kata zote 10 na kutoa elimu kwa wananchi na viongozi wa maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha viongozi wa dini, wazee maarufu, vijana, waalimu na wanafunzi juu ya ugonjwa huo hatari.

Nao upande wa Wilaya ya Kalambo  walieleza mipango yao juu ya udhubiti wa ugonjwa huu, ambapo mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Alcado mwamba aliweza uainisha tahadhari mbalimbali ambazo Wilaya imezichukua kuhakikisha wanaudhibiti ugonjwa huo kutokuingia katika Wilaya hiyo.

Miongoni mwa tahadhari walizochukua ikiwa ni kuwasambazia wananchi vipeperushi vyenye kutoa elimu ya ugonjwa wa Ebola lakini pia kuihamasisha jamii kutoa taarifa haraka kwa uongozi wa serikali pindi tu wakibaini kuna mgeni aliyeingia kinyume na taratibu zilizowekwa.

No comments:

Post a Comment