Wednesday, May 3, 2017

MSONDO VS SIKINDE KUWASHA MOTO MEI 20, TRAVENTINE JIJINI DAR.


Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

HISTORIA inaendelea tena kuandikwa baada ya bendi kongwe mbili za muziki wa Dansi nchini DDC Mlimani Park "Sikinde Ngoma Ukae" na OTTU Jazz "Msondo Ngoma" zitakutanishwa tena katika jukwaa moja kumtafuta nani mkali wa kulisakata rumba Mei 20 mwaka huu.

Bendi hizo kongwe zitakutana tena katika jukwaa  moja  na kumtafuta nani mkali huku kila upande ukitamba kumgaragaza mwenzake na kuibuka kidedea katika mpambano huo.

Pambano hilo linatarajiwa  kufanyika Mei 20 Mwaka huu katika ukumbi wa Traventine Magomeni huku mashabiki wa kila upande wakiombwa kuja kuhudhuria kwa wingi kuwaona wakali hao huku burudani za  nyimbo za zamani zikiratajiwa kutawala kwenye usiku huo.

Akizungumza kuelekea pambano hilo, mratibu Abdulfareed Hussein alisema mpambano huo wa nani zaidi utamuliwa na mashabiki wa dansi watakaojitokeza siku hiyo na zaidi kutakuw ana zawadi ambayo ni siri itakayotolewa siku hiyo.

Alisema kiingilio cha pambano hilo kitakuwa ni Sh. 10,000 ili kuwapa nafasi wadau wa dansi kushuhudia na kutoa maamuzi ya nani zaidi kati ya bendi hizo mbili.

"Hili pambano ndio litakata mzizi wa fitna, ambapo mashabiki ndio wataamua nani zaidi kati ya Msondo au Sikinde kwani ni muda mrefu sana hawajakutana jukwaa moja " alisema.

Wakati huo huo Mmoja wakilishi wa Sikinde, Abdallah Hemba alisema wamejiandaa vizuri kutoa burudani na kuhakikisha kwamba wako vizuri kuliko Msondo.

" Hawa jamaa wametukimbia sana, hivyo kila tunapotaka kukutana nao wanakuwa na safari naona Mei 20 ndio mwisho wao," alisema.

Nao Meneja wa Msondo, Said Kibiriti alisema wamejiandaa vyema hivyo katika pambano hilo wataimba nyimbo mchanganyiko na zaidi kambi hyao itakuwa Pemba na wanawaahidi mashabiki wa bendi yao kuja kwa wingi.

" Tutaimba nyimbo mchanganyiko, pia tutaimba nyimbo zetu mpya, tunaamini mpambano huo ndio utaweza kuamua nani kati yao ni zaidi," alisema Kibiriti.
Mratibu Abdulfareed Hussein akiwa katika picha ya pamoja na waimbaji wa bendi za  DDC Mlimani Park "Sikinde Ngoma Ukae" na OTTU Jazz "Msondo Ngoma" wakijiandaa na mpambano wa kumsaka Mkali nani Mei 20 mwaka huu.
 Mratibu Abdulfareed Hussein akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mpambano wa kumsaka mkali wa muziki wa dansi baina ya  DDC Mlimani Park "Sikinde Ngoma Ukae" na OTTU Jazz "Msondo Ngoma" utakaofanyika Mei 20 mwaka huu. Pembeni ni viongozi na waimbaji wa bendi hizo kulia ni Abdallah Hemba  kutoka Sikinde na kulia ni Meneja wa Bendi ya Msondo Said Kibiriti. 
 Muimbaji wa bendi ya Sikinde Abdallah Hemba akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mpambano huo baina yao na Msondo utakaofanyika Mei 20 mwaka huu. Kushoto ni  Mratibu Abdulfareed Hussein.
  Meneja wa Bendi ya Msondo Said Kibiriti akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mpambano huo baina yao na Msondo utakaofanyika Mei 20 mwaka huu akiwa sambamba na waimbaji wa timu hiyo Romario na Juma Katundu.

No comments:

Post a Comment