Saturday, May 6, 2017

MAMA SAMIA AWATAKA WAKUNGA KUFANYA KAZI KWA BIDII

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameziagiza Halmashauri zote nchini zihakikishe zinajenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa afya hasa maeneo ya vijijini na kipaumbele kitolewe kwa wakunga ambao mara nyingi ndio wanatoa huduma za dharura kwa wanawake wajawazito na watoto.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo mjini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani sherehe ambazo zimehudhuriwa na Mamia ya wakunga kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Makamu wa Rais amesema kuwa halmashauri zikijenga nyumba karibu na vituo vya kutolewa huduma za afya zitasaidia kupunguza matatizo ya mama na watoto wanaotaka kupata huduma za dharura ikilinganishwa na hali ilivyo sasa ambapo baadhi ya watumishi wa afya hasa wakunga wanakaa mbali na maeneo yao ya kazi hivyo utoaji wa huduma za dharura kuwa duni.

Makamu wa Rais amewahimiza Wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia ujenzi huo kikamilifu kama walivyoshughulikia matatizo ya madawati katika maeneo yao ili kuhakikisha Taifa linafikia malengo yake ya kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi nchini.

Kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini, Makamu wa Rais amewahakikishia wakunga na watumishi wengine wa sekta ya afya nchini kuwa Serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto hizo ikiwemo uboreshaji wa maslahi kwa watumishi wa kada hiyo pamoja na kuongeza maradufu vifaa tiba,dawa na vitendanishi ili kuhakikisha wananchi kote nchini wanapata huduma bora za afya.

Amesema mpaka sasa upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya afya nchini ni imefikia asilimia 83 hadi kufikia mwishoni mwa Marchi 2017.

Makamu wa Rais pia amewahimiza wakunga kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia maadili na waache tabia ya kutoa lugha mbaya kwa wanawake wajawazito na wakunga watakaobainika kufanya vitendo hivyo wachukuliwe hatua kali ili kukomesha tabia hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Wizara yake itaendelea kusimamia ipasavyo utoaji bora za afya kwa wananchi pamoja na kusimamia maadili kwa watumishi wa sekta ya afya kote nchini.

Amesema anaimani kubwa kuwa baada ya Serikali kuiongezea Wizara ya Afya bajeti kutoka bilioni zaidi ya 700 katika mwaka wa fedha za 2016/2017 hadi Trilioni Moja kwa mwaka wa fedha 2017/2018 inaonyesha wazi dhamira ya dhati ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa kiwango hali ya juu nchini ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Kauli mbinu ya maadhimisho ya Siku ya Wakunga mwaka huu ni Wakunga,Akina mama na Familia ni washirika wa Kudumu.(Midwives,Women and Families Partners)

BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan akihutubia kwenye kilele cha siku ya Wakunga Duniani ambapo Kitaifa imefanyika mjini Dodoma. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Samia akihutubia Wakunga kwenye kilele cha Sherehe za Siku ya Wakunga Duniani iliyofanyika Kitaifa mkoani Dodoma kwenye ukumbi wa Julius K. Nyerere Chuo cha Mipango.
Wakunga wakirekodi hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa sherehe za Siku ya Wakunga Duniani ambapo kitaifa zimefanyika mjini Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akihutubia Wakunga waliojitokeza kwa wingi kwenye kilele cha Siku ya Wakunga Duniani ambayo Kitaifa imefanyika mkoani Dodoma na mgeni rasmi ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

No comments:

Post a Comment