Tuesday, May 30, 2017

MAGHEMBE APONGEZA OPERESHENI YA KUONDOA MIFUGO HIFADHINI MKOANI KAGERA

Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto) akisalimiana na Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera katika ziara yake mkoani humo kuzungumzia operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa kisheria na mahakama. Anayeongoza utambulisho huo (kushoto) ni Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu. 
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera, mjini Bukoba kuhusu operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa kisheria. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro. 

NA HAMZA TEMBA - WMU
---------------------------------------------------------

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Kagera unaongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu kwa kufanikisha operesheni ya kuondoa mifugo katika maeneo ya hifadhi mkoani humo huku akitoa tahadhari kwa watumishi wa hifadhi hizo kupoteza ajira zao endapo wataruhusu mifugo hiyo kurudi tena katika hifadhi hizo.

Ametoa pongezi na tahadhari hiyo jana mjini Bukoba wakati akizungumza na uongozi wa mkoa huo na kusema kuwa, kazi hiyo ni ya kupongezwa sana kwakua imeleta matumaini ya uhifadhi mkoani Kagera na taifa kwa ujumla.

“Napenda niwashukuru kipekee kabisa kwa jinsi ambavyo mlifanya ile operesheni ya kuondoa mifugo kwenye hifadhi zetu, tulifanya kwa ueledi uliotukuka, hata kama umesikia watu wanalalamika lakini hakuna aliyesema kuku wangu waliuawa, walipigwa risasi, tulinyang’anywa mifugo, kazi hii ilifanywa vizuri na kwa ueledi mkubwa sana”, alisema Prof. Maghembe.

Aliongeza, “Hatutaruhusu tena mifugo hiyo irudi huko ndani ya hifadhi, hili ni jambo kubwa ambalo ni wajibu wa wahifadhi wote kuhakikisha  kwamba hakuna mifugo itakayokuwa inaingia humo ndani, Kuanzia sasa kama tutakuta mtu ameingia kwenye hifadhi yako wakati tunamuondoa tunamuondoa yeye na wewe na familia yako yote ili mbegu yako mbaya isibaki katika uhifadhi wa wanyamapori”.

Alisema ili kuimarisha ulinzi katika hifadhi hizo, utaratibu wa kutumia ndege maalum za doria na “drones” (ndege zisizo na rubani) utawekwa ili kuwabaini wahalifu watakaokuwa wamekaidia agizo hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.  

“Tutakua tunarusha ndege mara moja kila baada ya wiki tatu au wiki mbili kuhakikisha kwamba hakuna mtu anaingia na mifugo humo ndani, lakini pili tutafanya doria na ndege zile ambazo hazina marobani kuhakikisha kwamba tunaangalia kinachotokea humo ndani wakati wote.

“Najua wanaweza kubadilisha “system” (utaratibu) ikawa ya usiku na hawa askari hawa tutawapa mafunzo maalum chini ya jeshi la wananchi wa Tanzania, kuanzia miezi sita mpaka tisa, wajifunze namna ya kuhangaika na hawa ambao wanaingia kwenye hifadhi zetu”, alisema. 

Akizungumzia operesheni hiyo, alisema ulitolewa muda maalum kwa watu kutoa mifugo yao kwa hiari katika mapori ya akiba na hifadhi za misitu mkoani humo ambapo wale wote waliotii hakuna mashtaka yeyote yalifunguliwa dhidi yao ispokuwa wale waliokaidi walifikishwa mahakamani na mifugo yao ikataifishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kifungu namba 111 sehemu ya kwanza ambayo inaruhusu kutaifisha mali itakayokutwa hifadhini.

Alisema kuwa kumekuwepo na malalamiko mbalimbali juu ya utaratibu wa upigaji mnada mifugo iliyotaifishwa ikiwemo minada hiyo kufanyika ndani ya maeneo ya hifadhi, wenye mifugo kutoruhusiwa kuingia na wakati mwingine kuwepo kwa malalamiko ya idadi tofauti ya mifugo iliyotaifishwa na inayopelekwa mnadani.

Ili kuondoa malalamiko hayo alielekeza kuwa baada ya amri ya mahakama kutoka ni lazima mamlaka ya Wilaya husika ijulishwe na zoezi hilo lifanyike katika maeneo ya wazi ili kila mwananchi anayehitaji aweze kushiriki mnada husika.

“Minada hii ifanywe kwa maelekezo ya mamlaka, hukumu ikitoka mkuu wa wilaya ajulishwe, na kwamba mifugo kadhaa itapigwa mnada, na yeye ataamua mnada ufanyike wapi na lini, na iwe sehemu ambayo kila mtu anaweza kufika, minada hiyo iwe ya wazi na matangazo yatolewe ili malalamiko yasiwepo ndio maana maelekezo yametoka minada isitishwe kwa muda wa siku saba mambo haya yawekwe sawa”, alisema Maghembe.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu alishukuru kwa ushirikiano alioupata kutoka Wizara ya Maliasili katika kipindi chote cha utekelezaji wa operesheni hiyo ambayo amaeielezea kuwa na mafanikio makubwa ikiwemo wanyamapori kuanza kurudi kwenye maeneo yao katika Mapori ya Akiba ya Biharamulo Burigi na Kimisi.

“Niishukuru wizara yako mmetupa ushirikiano mzuri, kule tumesafisha tumehakikisha hakuna mifugo, hakuna kilimo, vitendo mbalimbali vya kibinadamu vilivyokuwa vikifanywa kule vya kilimo, ukataji miti hovyo, kuchoma mikaa, kulima mashamba mbalimbali ya mahindi, bangi, mirungi sasa hayapo tena, Nashukuru kwa muda huu mfupi wanyama wengi wamesharudi, wengi tuu, hadi Simba wamesharudi kwenye maeneo yao” alisema Kijuu.

Operesheni ya kuondoa mifugo na wananchi waliovamia Hifadhi ya Misitu ya Biharamulo, Nyantaka na Ruiga na Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi mkoani Kagera ilianza tarehe 30 Machi, 2017 ambapo jumla ya mifugo 5,939 ilikamatwa (Ng’ombe 5754, Mbuzi 140 na kondoo 45) na watuhumiwa 185 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.  
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera, mjini Bukoba kuhusu operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa kisheria. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro (kulia), Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Diwani Athuman (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa. 
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akizungumza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera, mjini Bukoba. 
Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Maliasili (katikati waliokaa) na kamati ya ulinzi na usala ya Mkoa wa Kagera muda mfupi baada ya kikao cha kujadili operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa kisheria.
 Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii (katikati waliokaa), Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu (wa pili kulia waliokaa), Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro (wa pili kushoto waliokaa), Katibu Tawala Mkoa huo, Diwani Athuman (kulia waliokaa), Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa (kushoto waliokaa), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Laibooki (katikati waliosima) na maofisa wa Mamlaka hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu (kushoto) akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Laibooki (wa pili kushoto) Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Kudhibiti ujangili, Faustine Masalu (kulia).
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa (kulia), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (katikati) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Laibooki (kushoto). 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akisalimiana na uongozi wa Wilaya ya Biharamulo alipotembelea wilayani humo kwa ajili ya kutoa maelekezo ya Serikali kuhusu operesheni ya kuondoa mifugo katika maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyokamatwa na kutaifishwa na mahakama. Anayeongoza utambulisho huo (kulia) ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Sada Malunde.
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na usala ya Wilaya ya Biharalamulo na watumishi wa sekta ya wanyamapori wilayani humo. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza Kamati ya Ulinzi na usala ya Wilaya ya Biharalamulo na watumishi wa sekta ya wanyamapori wilayani humo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Sada Malunde na Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Diwani Athuman (kushoto). 
 Baadhi ya askari na watumishi wa Idara ya Wanyamapori wa Wilaya ya Biharamulo.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, viongozi wa mamlaka za uhifadhi, watumishi na kamati ya ulinzi na usala ya Wilaya.
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akiagana na Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Diwani Athuman pamoja na viongozi wengine wa chama na Serikali wa Wilaya ya Biharamulo baada ya kumaliza ziara yake Mkoani humo ya kujadili operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa kisheria. 

No comments:

Post a Comment