Friday, May 5, 2017

Kaimu Balozi wa Marekani Nchini Atembelea Wabia Mkoani Mwanza, Aangazia ushirikiano kati ya Watu wa Marekani na Watanzania


Mwanza, TANZANIA. Tarehe 3 Mei, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Virginia Blaser alifanya ziara ya siku moja kuwatembelea wabia mbalimbali mkoani Mwanza kuona shughuli zao akiangazia ushirikiano imara uliopo kati ya watu wa Marekani na Watanzania katika sekta mbalimbali. 
Kaimu Balozi Blaser alianza ziara yake kwa kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari ambayo kwa miaka miwili iliyopita Ubalozi wa Marekani umekuwa ukiyafadhili. “ Uhuru wa habari ni muhimu sana katika jamii ya kidemokrasia inayolinda haki za watu,” alisema Kaimu Balozi Blaser katika hotuba yake katika maadhimisho hayo. Aidha, alisisitizia umuhimu wa waandishi wa habari na wadau wengine wa vyombo vya habari kushirikiana kwa kuchangia mawazo na kusaidiana kama sehemu ya mtandao mkubwa wa kimataifa unaotoa na kuelezea mitazamo mbalimbali na kuwapa raia sauti kuelezea kero na dukuduku zao.  
Katika ziara yake katika Taasisi ya Mafunzo ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Pasiansi, ambayo inatoa mafunzo ya uhifadhi wa wanyamapori na kukabiliana na ujangili kwa askari wa wanyamapori wa Kitanzania, Kaimu Balozi Blaser alishuhudia wanafunzi wakionyesha kwa vitendo ujuzi walioupata katika usimamizi wa sheria, mbinu za medani na historia ya viumbe asilia.  Serikali ya Marekani iliichangia taasisi ya Pasiansi kwa kufadhili mafunzo kwa wafanyakazi wake nane ili kusaidia kujenga uwezo wa kulinda wanyamapori nchini Tanzania.  
Hali kadhalika, Kaimu Balozi Blaser alipata fursa ya kushuhudia matokeo chanya ya msaada wa Serikali ya Marekani katika nyanja ya usalama pale alipotembelea Chuo cha Polisi Wanamaji cha Mwanza na kuona doria ya majini inayofanywa na askari hao kwa kutumia boti maalumu ya doria (Defender Boat) ilitolewa na Marekani chini ya Mpango wake wa Ubia na nchi za Afrika katika kulinda Amani (African Partnership for Rapid Response Peacekeeping).  Mbali na boti mbili zilizotolewa kwa Chuo cha Polisi Wanamaji, Marekani ilitoa boti nyingine nane kwa Tanzania na kuwezesha matunzo na matengenezo yake. 
Katika sekta ya afya, Kaimu Balozi Blaser alizungumza na watoa huduma zinazohusu matibabu na kinga dhidi ya VVU/UKIMWI kwa jamii wa kujitolea (Community Outreach Volunteers) ambao wamekuwa wakitoa elimu na huduma za kujikinga na VVU kwa makundi-rika yao chini ya mpango wa ICAP unaoendeshwa na Chuo Kikuu cha Columbia. Mpango huo ni wabia wa Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Maradhi (CDC) na Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI.  Aidha alikutana na wafanyakazi wa kujitolea wa Kimarekani kutoka Peace Corps wanaofanya kazi katika hospitali ya Bugando wakisaidia kuimarisha utoaji wa elimu kwa matabibu na wauguzi na kuimarisha taratibu za utoaji matibabu.  Akiwa katika Kituo Maalumu cha Matibabu ya UKIMWI kwa watoto  kiitwacho Baylor International Pediatric AIDS Initiative HIV Care Center of Excellence – kilichojengwa kwa ubia kati ya Serikali ya Marekani na Sekta binafsi nchini Marekani na kupata msaada wa wataalamu na uendeshaji wake kupitia Shirika la Marekani la Ushirikiano wa Kimataifa (USAID) –   Kaimu Balozi Blaseraliwashukuru wafanyakazi wa kituo hicho kwa kutoa matunzo na matibabu kwa watoto waliopata maambukizo ya VVU na kuchangia katika jitihada za kufikia lengo la Umoja wa Mataifa la 90-90-90 yaani kuhakikisha asilimia asilimia 90 ya walioathirika na maambukizi ya VVU wanapimwa na kujua hali zao kiafya, asilimia 90 ya watakaopimwa na kukutwa na VVU wanapata dawa za kufubaza  VVU na asilimia 90 ya waliopo kwenye tiba wawe wameweza kuvidhibiti virusi hivyo kwa kiwango kikubwa.

No comments:

Post a Comment