Tuesday, May 30, 2017

Bunge lapitisha Bajeti ya Wizara

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amewasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Mahiga katika hotuba yake aliliomba Bunge kupitisha kiasi cha shilingi150,845,419,000 ambapo katika kiasi hiki cha fedha shilingi142,845,419,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 8,000,000,000 imetengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.

Bajeti hii ya mwaka 2017/2018 pamoja na mambo mengine imepanga kutekeleza malengo makuu muhimu kulingana na majukumu ya Wizara kama ifuatavyo;

  • Kutangaza mazingira mazuri ya nchi yetu kwa ajili ya uwekezaji kutokana na historia yake ya miaka mingi ya amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa; 
  • Kuendelea kufuatilia utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa kwa nchi yetu na nchi wahisani, mashirika ya kikanda na ya kimataifa katika kusaidia utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo; 
  • Kuendelea kuratibu Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali katika kuvutia wawekezaji na watalii, kutafuta nafasi za masomo, ajira na nafasi za kubadilishana uzoefu na kutafuta masoko; 

  • Kusimamia, kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa kati ya nchi yetu na nchi nyingine na ile ya mashirika ya kikanda na kimataifa; 

  • Kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya viongozi mbalimbali wa kitaifa; 
  • Kuendelea kusimamia balozi zetu katika kutekeleza majukumu ya uratibu hasa kutafuta wawekezaji, fursa za ajira, nafasi za masomo na masoko kwa bidhaa zetu; 
  • Kuendelea kufuatilia kwa karibu mageuzi kwenye taasisi za Umoja wa Mataifa kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Baraza la Kiuchumi na Kijamii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo; 
  • Kuongeza uwakilishi wetu nje kwa kufungua Balozi mpya na Konseli Kuu na kuendelea kununua, kujenga na kukarabati majengo kwa ajili ya makazi na ofisi za Balozi kwa kadri hali ya fedha itakavyoruhusu; 
  • Kujenga mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa kiuchumi kati yetu na vyombo mbalimbali vya Kikanda na Kimataifa, unaozingatia maslahi ya Taifa letu; 

  • Kuendelea kutetea na kusimamia maslahi ya nchi maskini kwenye mikutano yote mikubwa na hasa ile ya Umoja wa Mataifa na taasisi zake. Vilevile, tutaendelea kufanya mazungumzo na nchi tajiri duniani ili kuhakikisha zinatekeleza ahadi mbalimbali zilizotoa ili kuharakisha maendeleo ya nchi maskini. Kwa mfano, ahadi za G8 na ile ahadi ya kila nchi tajiri kutoa asilimia 0.7 ya pato lake la Taifa kwa nchi zinazoendelea na kutoa asilimia 0.2 ya pato lake kwa nchi maskini sana duniani kama msaada; 
  • Kuendelea kutambua jumuiya za watanzania wanaoishi ughaibuni na kuweka utaratibu utakaowawezesha kuchangia maendeleo ya taifa;
  • Kuratibu maandalizi na kushiriki kwenye majadiliano katika mikutano ya Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mikutano ya Vikundi Kazi na Wataalam; 
  • Kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri ya Afrika Mashariki, miradi na programu za Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa miaka kumi wa Umoja wa Fedha katika kuelekea kwenye eneo la Sarafu Moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; 

  • Kuratibu zoezi la mapitio ya Sheria za Tanzania ili kuwezesha Watanzania kunufaika na utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu majadiliano na kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kuanzisha Eneo Huru la Biashara baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na COMESA na SADC pamoja na Eneo Huru la Biashara la Afrika; 
  • Kuratibu majadiliano kuhusu maeneo ya ushirikiano katika uendelezaji wa miundombinu ya kiuchumi (reli, barabara, bandari, nishati, viwanja vya ndege na hali ya hewa) na kijamii (elimu, afya, mazingira, jinsia na watoto) katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiforodha katika biashara baina ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu ushiriki wa Tanzania katika Mikutano ya Bunge la Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu na kushiriki katika maandalizi ya Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzingatia mfumo wa Confederation; 
  • Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha Baraza la Usalama la Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha Itifaki ya Utawala Bora ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kutoa Elimu kwa Umma juu ya fursa zitokanazo na mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu mapitio, utafiti, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu na kufanya uchambuzi wa utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Taasisi ya TradeMark East Africa Wizarani, Wizara nyingine, Idara, Taasisi za Serikali na sekta binafsi; na Kukamilisha kuandaa Sera Mpya ya Mambo ya Nje 
Hotuba ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 mara baada ya kuwasiliswa ilijadiliwa na kuchangiwa na Wabunge mbalimbali na hatimaye kupitishwa na Bunge hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb) akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Bungeni mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb) akijibu hoja mbalimbali za Wabunge wakati wa Kikao cha Bunge baada ya kuwasilishwa kwa bajeti ya Wizara Mjini Dodoma. 
Baadhi ya Waheshimiwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali nchini wakifuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bungeni mjini Dodoma. 
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga akifurahia jambo na Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Peter Msigwa mara baada ya kuwasilisha hotuba ya bajeti Bungeni mjini Dodoma. 
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga, Naibu Waziri Dkt. Susan Kolimba, Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz Mlima na Waziri Kivuli wa Wizara Mhe. Msigwa wakiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi na baadhi ya Wabunge. 
Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga na Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz Mlima wakishirikishana jambo baada ya kuwasilisha hotuba ya Madirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2017/2018 katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga akijibu hoja za wa Bunge Bungeni. 
Waziri Mhe.Dkt. Mahiga na Naibu Waziri Mhe.Dkt. Susan Kolimba wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji mbalimbali wa Wizara mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara Bungeni Mjini Dodoma.

No comments:

Post a Comment