Monday, April 3, 2017

Wazazi watakiwa kuwa waangalifu na watoto wao wanaosoma nje


Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel akizungumza jambo kwenye mkutano wa wazazi ambao watoto wao wanasoma nje ya nchi
Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu, Prof. Simon Msanjila akiwaasa wazazi kwenye mkutano wa wazazi ambao watoto wao wanasoma nje ya nchi

Robert Shetkintong, Naibu Balozi wa India nchini akifuatilia mijadala katika kikao cha wazazi ambao watoto wao wanasoma nje ya nchiBaadhi ya wazazi walioshiriki mkutano wa wazazi ambao watoto wao wanasoma nje ya nchi mwishoni mwa wiki.

Wazazi wametakiwa kuwa waangalifu wa watoto wao wanaosoma nje ili kuhakikisha wanasoma na kuhitimu vizuri kama inavyotakiwa.

Akizungumza na wazazi ambao watoto wao wanasoma nje, Mkurugenzi wa kampuni ya uwakala ya Global Education Link, Abdulmalik Mollel amesema hilo likifanyika taifa litanufaika zaidi.

“Tuendelee kushirikiana kwa pamoja ili kuona watoto wetu walioko nje kwa masomo wanamaliza masomo yao na kutimiza ndogo zao inavyotakiwa. Sisi wazazi tuna mchango mkubwa sana katika hili,” alisema Mollel mwishoni mwa wiki.

Alifafanua kwamba kuna watoto wamekuwa wakipewa fedha nyingi na wazazi wao kiasi kwamba nao wanapofika nje huwa bize kufanya matanuzi badala ya kusoma kama ambavyo tunatarajia.

“Unakuta mtoto anapewa fedha nyingi hadi anashindwa kujua azitumie kwa matumizi gani, ndipo hapo wengine unakuta wanajiingiza kwenye ulevi na mambo mengine kama hayo. Ni lazima tunapowapa fedha tujiridhishe je ni kwa ajili ya nini na wanazitumiaje,” alisema Mollel.

Kwa mujibu wa Mollel ni jambo zuri mzazi au mlezi kuhakikisha mwanae anapata matunzo bora ikiwamo kumpatia kile ambacho anaamini kwamba kitamsaidia kusoma vizuri, lakini kwenye suala la kuwapa fedha nyingi watoto huwachanganya kimaisha na kusababisha baadhi yao kujikuta wakifanya ambavyo hawamkutarajia.

Mollel ambaye alikuwa akiongea katika kikao cha wazazi ambao wanasoma nje baada ya kuunganishwa na GEL, alishauri kuundwa kwa umoja wa wazazi ambao watotyo wao wanasoma nje kupitia GEL (GELPA), ushauri ambao uliungwa mkono na wazazi.

Wazazi waliokuwepo kwenye mkutano huo waliunga mkono kuanzishwa kwa GELPA, huku wengine wakitaka jambo hilo lifanywe mara moja iwezekanavyo wakisema kuwa lina umuhimu mkubwa.

Naye Robert Shetkintong, Naibu Balozi wa India nchini ambaye alikuwa kati ya wazungumzaji katika mkutano huo amewahakikishia Watanzania kwamba nchi yake ni sehemu salama kwa wageni kusoma.

“India ni nchi nzuri, haina ubaguzi wa aina yoyote, unaweza kuona hata mimi naona kama mwafrika, naonekana kama mchina kwa kiasi fulani, lakini ndio naibu balozi wa taifa la India hapa Tanzania,” alisema.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu, Prof. Simon Msanjila alisema “Hata mimi nimewahi kusoma nje, ninazijua changamoto za kusoma nje, lakini ninachoweza kushauri ni kwa wazazi kushirikiana na kulea jamii yetu iliyoko huko nje. Kwenda kusoma nje kuna faida kadhaa ikiwamo kuchukua mawazo mapya kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Profesa Msanjila aliwashauri pia watu na makampuni yanayofanya kazi ya uwakala wa vyuo vya nje kuhakikisha wanafuatilia vyuo wanavyoviwakilisha vinatambulika.

“Mzazi unawajibika kufuatilia vyuo ambavyo mtoto wako anatarajia kwenda kusoma. Unaweza kulazimisha ili mradi aende nje kwa sababu tu unapenda aende nje, lakini nawashauri kwamba ni suala la msingi sana kuhakikisha mtoto anasoma katika chuo ambacho kweli kinatambulika.


Akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa, Mkurugenzi wa GEL, Abdulmalik Mollel alisema “Nikuondoe hofu kuhusiana na vyuo tunavyowakilisha, kwani utaratibu ambao tunautumia ni kwamba kabla ya kuanza kupeleka wanafunzi katika chuo, huwa tunakifuatilia na kukipeleka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili kuhakikiwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment