Sunday, April 2, 2017

Vijana wametakiwa kutumia sekta isiyo rasmi kujiajiri kwa maendeleo ya Taifa

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama akifungua kongamano la Vijana kuelekea uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 leo Mkoani Katavi.
JENI2
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga akizungumza na Vijana (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kongamano la Vijana kuelelekea uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 leo Mkoani Katavi.
JENI3
Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Moudline Castico akizungumza na Vijana na watendaji wa Mkoa wa Katavi (hawapo katika picha) juu ya matumizi ya Tovuti ya Mkoa kabla ya kuzindua Tovuti hiyo leo Mkoani Katavi.
JENI4
Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Moudline Castico (katikati) akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Tovuti ya Mkoa wakati wa kongamano la Vijana kuelekea uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 leo Mkoani Katavi.
JENI5
Baadhi ya Vijana wa Mkoa wa Katavi wakifuatilia kwa makini mada zilizokua zikitolewa wakati wa kongamano la vijana kuelekea uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 leo Mkoani Katavi.
Picha na: Genofeva Matemu – WHUSM


Na: Genofeva Matemu – WHUSM, Katavi

Vijana Mkoani Katavi wametakiwa kujitambua, kuchukua fursa na kuchangia maendeleo ya mkoa na taifa kwa kutumia malighafi zinazopatikana mkoani humo kuwekeza na kuacha kusubiria wawekezaji kutoka mikoa mingine ama nchi za nje kufaidika na malighafi za mkoa huo.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokua akifungua kongamano la Vijana kuelekea uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 leo Mkoani Katavi na kuwataka vijana hao kuacha uvivu kwani maendeleo huletwa na jitihada za mtu binafsi.

Mhe. Jenista amesema kuwa vijana wanaweza wakajiwekeza katika sekta isiyo rasmi kwani sekta hiyo huajiri asilimia kubwa na kuwagusa vijana wengi katika kutengeneza ajira na kuwafanya vijana wasiwe tegemezi ndani ya jamii.

“Vijana wa Mkoa wa katavi mnayo kila sababu kujitafiti na kujua ni namna gani mtatumia sekta isiyo rasmi kutengeneza ajira ambazo zitawasaidia kuonyesha mchango wenu wa asilimia 55 kama vijana katika nchi ya tanzania ukaweza kutumika   kuleta maendeleo ya Mkoa na taifa kwani mnaweza, sababu mnayo, nguvu mnayo na uwezo mnao” amesema Mhe. Jenista

Kwa upande wake Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Moudline Castico amewataka vijana wa Mkoa wa Katavi kutumia Tovuti ya Mkoa iliyozinduliwa wakati wa kongamano hilo kupata taarifa kwa wakati ili waweze kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga amesema kuwa Tovuti ya Mkoa yenye kikoa/domeini ya www.katavi.go.tz itakua na taarifa za uhakika na za wakati hivyo kuwawezesha wananchi wa Mkoa wa Katavi wakiwemo vijana kujua taarifa za maendeleo za mkoa pamoja na masuala mengine muhimu kama vile kuelimisha vijana masuala muhimu ya kilimo bora, ujenzi wa viwanda vidogo na vikubwa, afya ya jamii, taaluma za kibenki na ujuzi wa aina mbalimbali za kiteknolojia utakaowawezesha vijana kujaribu.

No comments:

Post a Comment