Thursday, April 6, 2017

SERIKALI YAUNGANISHA SHULE 417 KWENYE MTANDAO WA INTANETI – WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Viettel ya Vietnam inatekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano vijijini ambao umefanikisha kuweka miundombinu ya mtandao wa intaneti kwenye shule 417 hapa nchini. 

Amesema mradi huo ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2015-2017, umewezesha pia ofisi za Halmashauri za Wilaya 123, Hospitali za Wilaya 74, Vituo vya Polisi vya Wilaya 131 na Ofisi za Posta 68 kufikiwa na mtandao huo. 

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 6, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2016/2017 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake ukiwemo Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018 

Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2016/2017, baadhi ya kazi zilizofanyika kwenye sekta ya mawasiliano ni pamoja na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; Mradi wa Anuani za Makazi na Postikodi; na kuanzisha huduma ya kituo cha Jamii Centre kitakachorahisisha utoaji wa huduma muhimu katika kituo kimoja. Huduma hizo ni kulipa pensheni, ankara na huduma za kibenki. 

“Sekta ya mawasiliano inatekeleza Programu ya Miundombinu ya Kikanda ambayo inahusisha Mradi wa Shule Mtandao (e-school), Mradi wa Video Conference ambao unahusisha ununuzi, usimikaji na ufungaji wa vifaa vya TEHAMA katika mikoa 26 na taasisi za Serikali,” amesema. 

Amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa kituo cha kuhifadhi taarifa na mifumo ya Serikali (Government Data Centre) ambacho lengo lake ni kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa unaoenda sambamba na uhakika wa upatikanaji wa taarifa za Serikali katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku. 

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa viwanda, Waziri Mkuu amesema Serikali inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kujenga uchumi wa viwanda, na kwamba inatoa kipaumbele kwenye viwanda vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa nchini, vinavyotoa ajira kwa watu wengi na vinavyozalisha bidhaa zenye soko hapa nchini na nje ya nchi. 

“Katika kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda, Serikali inahamasisha zaidi sekta binafsi ya hapa nchini pamoja na mashirika ya umma kujenga viwanda. Jitihada hizo zimewezesha mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF, PPF, LAPF, GEPF, PSPF na NHIF kuanza kufufua, kuendeleza na kujenga viwanda vipya vipatavyo 27 katika maeneo mbalimbali nchini,” amesisitiza. 

Ameyataka mashirika ya umma yahakikishe kwamba mipango yao inaendana na utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ambao dhima yake ni kujenga uchumi wa viwanda. 

Akizungumzia kuhusu juhudi za Serikali kupambana na rushwa, Waziri Mkuu amesema Serikali inapambana na rushwa kwa nguvu zake zote na haina mzaha wala uvumilivu na vitendo vya rushwa. 

“Hatua zilizochukuliwa kupambana na rushwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Novemba, 2015 zimetambuliwa na mashirika ya Kimataifa yanayojishughulisha na tafiti kuhusu masuala ya rushwa duniani. Taarifa ya Shirika la Transparency International kwenye utafiti wake kuhusu mtazamo wa rushwa mwaka 2016, imeonesha kuwa viwango vya rushwa vinaendelea kupungua hapa nchini,” amesema. 

Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali iliweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 9.75 kutokana na operesheni zilizofanywa na TAKUKURU, 

“TAKUKURU imefanya uchunguzi wa majalada 306 ya tuhuma za rushwa na kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini kuendelea na mashtaka kwa majalada 104. Katika kipindi hicho, TAKUKURU iliendesha kesi 674 zikiwemo kesi mpya 182, ambapo katika kesi 97 watuhumiwa walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini. Kesi 407 zinaendelea kusikilizwa mahakamani,” amesema. 

Amesema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaendelea na mapambano dhidi ya rushwa hususan katika eneo la ukusanyaji mapato ya Serikali, kudhibiti matumizi ya fedha za umma, malipo hewa, matumizi mabaya ya fedha za ushirika na kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo. 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imefungua balozi mpya sita katika nchi za Algeria, Israel, Korea Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki. Amesema Balozi hizo zina kazi ya kuendeleza juhudi za kuitangaza Tanzania kama nchi yenye vivutio vingi vya utalii na rasilimali zinazoweza kutumika kuvuta uwekezaji kutoka mataifa hayo ikizingatiwa utulivu na amani iliyopo nchini. 


IMETOLEWA NA: 



OFISI YA WAZIRI MKUU, 


S. L. P. 980, 






DODOMA, ALHAMISI, APRILI 4, 2017.

No comments:

Post a Comment