Saturday, April 1, 2017

KISHAPU YAPONGEZA SHULE KUMI BORA KWENYE MTIHANI WA TAIFA 2016


Mwakilishi wa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Sigisbert Rwezaula akizungumza katika hafla ya kupongeza shule za msingi kumi bora kwa mtihani wa taifa wa mwaka 2016 
Afisa Elimu Msingi Wilaya, Sosthenes Mbwilo akitambulisha walimu na waratibu elimu kata katika hafla hiyo. 
Mgeni rasmi, Sigisbert Rwezaula akitoa cheti kwa mmoja wa walimu wakuu wa shule zilizofanya vizuri. Wengine pichani kulia ni Afisa Ugavi Wilaya, George Ngwesa. 
Walimu wakifurahia cheti walichopewa kwa kutambua kufanya vizuri kwa shule yao. 
Wageni waalikwa wakiserebuka muziki ikiwa ni moja ya shamrashara za kupongezana kwa kazi nzuri. 
Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na walimu wakuu wa shule kumi bora pamoja na maofisa elimu mbalimbali. 
Mwakilishi wa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Sigisbert Rwezaula akizungumza katika hafla ya kupongeza shule za msingi kumi bora kwa mtihani wa taifa wa mwaka 2016. . Wengine pichani kuanzia kushoto ni Afisa Ugavi Wilaya, George Ngwesa, Afisa Elimu Msingi Wilaya, Sosthenes Mbwilo na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paul Sheka.

Walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamepongezwa kazi nzuri na kupata matokeo mazuri ya shule zao za msingi katika mtihani wa taifa wa mwaka jana.

Pongezi hizo zilitolewa jana na mwakilishi wa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Sigisbert Rwezaula wakati wakati wa hafla ya kupongeza shule kumi zilizofanya vizuri katika mitihani ya mwaka jana.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Mwadui wilayani Kishapu ikiambatana na utoaji vyeti kwa walimu wakuu, Rwezaula ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema hakuna muujiza wa kufanya vizuri bali ni walimu kujituma.

Aliwataka walimu wakuu wa shule ambazo hazikufanya vizuri kuhakikisha wanaweka mikakati ili ziweze kuibuka vinara kama walivyo wenzao na kuwataka kuendelea kujituma.

”Najua kuna changamoto nyingi kwa walimu kama upungufu au ukosefu wa fedha lakini nawaomba tuvumilie na tukabiliane nazo, jambo kubwa ni kutoa elimu bora kwa wanafunzi wetu na hatimaye wafanye vizuri,” alisisitiza.

Aidha Rwezaula aliongeza kwa kutoa rai kwa walimu wa shule hizo za msingi zilizopo katika halmashauri hiyo kuwa na utamaduni wa kujiendeleza kimasomo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Alisema hivi sasa dunia ipo katika utandawazi ambapo kunashuhudiwa ugunduzi mkubwa wa kiteknolojia ambao unahitaji maarifa makubwa ili kuendesha masuala mbalimbali ya kitaaluma.

”Ni vizuri walimu mkajiendeleza kielimu msiishe hapo mlipo, msikubali kuwa nyuma ya wakati kwani hivi sasa elimu ni muhimu sana na mnashuhudia dunia ni kama kijiji mnaweza kupata habari kwa mitandao,” alisema.

Rwezaula aliwataka kuwa na utaratibu wa kufidia vipindi vilivyopotea wakati mwalimu kapata dharura au ruhusa na kushindwa kuingia darasani na kuwafundisha wanafunzi.

Alisema kwa kuwa na utaratibu huo kutawawezesha wanafunzi kupata wasaa wa kujifunza na kuelewa masomo yao kwa wakati na hivyo kufanya vizuri zaidi kwenye mitihani yao.

Awali wanataaluma hao walifanya kikao kazi cha kutathmini mambo yaliyojiri kitaaluma katika Idara ya Elimu Msingi halmashauri ya wilaya hiyo kipindi cha mwaka 2016.

Kikao hicho kilichofanyika Mwadui kilihusisha maofisa elimu msingi, waratibu elimu kata, walimu wakuu na badhi ya walimu wa shule mbalimbali za msingi zilizopo Wilaya ya Kishapu 

No comments:

Post a Comment