Monday, April 24, 2017

JOKATE MWEGELO ATEULIWA KUWA KAIMU KATIBU HAMASA NA CHIPUKIZI UVCCM

Ndugu zangu, vijana wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na vijana wote wenye mapenzi mema na chama chetu na Watanzania wote kwa ujumla.

Nitangulie kwa kuwashukuru kamati ya utekelezaji ya UVCCM TAIFA kwa kuonyesha mapenzi makubwa na imani kubwa kwangu kwa kukubali kuniteua ku-kaimu nafasi ya Katibu wa UHamasa na Chipukizi. 

Imani yenu kwangu inabaki kuwa deni na chachu ya kujitoa kwa nguvu zote, kwa akili zote kuitumikia vizuri nafasi hii. Mwenyezi Mungu anisaidie.

Pili, kama ilivyo alama ya kwenye nembo ya jumuia yetu, ile alama ya mwenge wa uhuru. Mwenge wa Uhuru unaashiria nuru na mwanga. Mwenge huu unamulika nchini na nje ya mipaka ili kuleta matumaini pale ambapo kuna kukata tamaa, upendo pale kwenye chuki na heshima pale penye dharau- hii nimenukuu. 

Hivyo sifa kuu ya mwenge wetu wa uhuru kwenye nembo ya jumuiya yetu ya vijana ni kutoa mwanga, na sifa kuu ya mwanga ni kuweza kutokomeza giza na kutoa tumaini. Hivyo sisi kama vijana tunategemewa kuwa tumaini. Sisi kama vijana tunategemewa kuonyesha si tu njia bali kuwa tumaini kwamba taifa lilioasisiwa na waasisi wa nchi hii "our founding fathers" lipo katika mikono salama. 

Na hatuishii hapo bali jukumu la kuleta tumaini hili liko kwenye sehemu sahihi kupitia jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama chetu Cha Mapinduzi. Sehemu pekee ambapo viongozi wa sasa na baadae hupikwa vilivyo kuweza kuitumikia nchi yetu kwa weledi na uadilifu uliotukuka. Hivyo basi ni lazima kutengeneza taswira itakayowapa hamu vijana wa Tanzania kutamani kuwa sehemu ya UVCCM. Ni lazima tuwe wabunifu na kuvutia vijana wengi zaidi ili kupanua wigo wetu pia.

Tatu, hii nafasi niliopewa ni ya uwakilishi tu sio yangu, mimi nawakilisha tu vijana milioni nne na ushee amabao ni wanachama wa jumuiya hii. Walikuwepo viongozi kwenye nafasi hii kabla yangu na watakuja wengine baada yangu. Hivyo basi natoa rai tushirikiane, tufanye kazi wote tujenge jumuiya hii kwa umoja wetu. Nahitaji sana maoni na ushirikiano wenu. Ni muda jumuiya yetu iendane na nyakati za sasa ili tusipoteze watu na vile vile watu wasiachwe nyuma katika harakati zetu hizi. Na hasa katika kipindi hiki tunavyojiandaa na uchaguzi wa ndani ya chama.

Nne, hivi karibuni tutazindua njia ya kisasa na kampeni itakayosaidia kurahisisha upatikanaji wa habari ndani ya jumuiya yetu. Naomba mkae tayari kupokea mapinduzi hayo ambayo ni ya kwanza ndani ya Chama chetu cha Mapinduzi (CCM).

Kuelekea sherehe za Muungano tarehe 26/04/2017, ambapo kwa mara ya kwanza yatafanyika katika makao makuu ya nchi, Dodoma. Nawakaribisha tumuunge mkono Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kwa kushiriki katika mazoezi asubuhi na kisha matembezi yatakayo hitimishwa kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma. Taarifa rasmi itatoka hivi punde.

Nihitimisha kwa kuwashukuru wote walionipongeza na kunitakia kheri katika utumishi huu. Katika falsafa za ubuntu - umuntu ngumuntu ngabantu, tunasema "I am because we are".

Nawataki kazi njema,

Wenu Katika Utumishi,

Jokate Mwegelo.
K/Katibu Hamasa na Chipukizi.
Kidumu Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hapa Kazi Tu!

No comments:

Post a Comment