Friday, March 3, 2017

WACHAPISHAJI NCHINI WAMETAKIWA KUJIANDIKISHA KWA MPIGA CHAPA MKUU WA SERIKALI.


Jovina Bujulu- MAELEZO

Serikali imewataka wachapishaji wote nchini waliojiandikisha kwa Msajili wa Makampuni ( BRELA) na Mamlaka ya Mapato (TRA), kufika katika ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ili wajiorodheshe na watambuliwe na Serikali na wananchi kabla ya Machi 30 mwaka huu.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ndugu Cassian Chibogoyo alipokuwa akizungumzia kuwepo kwa wimbi kubwa la wachapishaji hewa nchini.

Chibogoyo amesema kuwa hatua hiyo inafuatia uwepo wa utitiri wa wachapishaji ambao hawatambuliki na Serikali, kwa sababu baada ya kujiandikisha kwa mamlaka husika kama kampuni, utawakuta wana mitambo ya uchapishaji ambayo mara nyingi wanaitumia kuchapisha nyaraka bandia za Serikali bila kuwa na kibali kutoka katika mamlaka yenye dhamana ya uchapishaji.

“Kwa sasa tumeanzisha utaratibu maalum wa kuwatambua wachapishaji ambapo wanatakiwa kujiorodhesha kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, hii ni kutokana na kuwepo kwa uchapaji holela na bandia wa nyaraka za Serikali” alisema Chibogoyo.

Aliongeza kuwa chini ya utaratibu uliowekwa sasa wachapishaji wanatakiwa kuwasilisha nyaraka halali za kampuni, shughuli wanazofanya, historia ya kampuni na mahali kampuni inapofanyia kazi zake.

Adha, Chibogoyo alisema kuwa faida za wachapishaji kujiandikisha ni pamoja na kutambuliwa kisheria na Serikali ili hata wanaposhutumiwa waweze kulindwa na Serikali, kukumbushana majukumu yao , wigo wao wa kazi, na pia wataelimishwa kuhusu nyaraka wanazopashwa kuchapisha maana si kila nyaraka wanapashwa kuzichapisha.

Zaidi ya hayo, Chibogoyo alitaja madhara ya kuchapisha nyaraka bandia kuwa ni pamoja na kuikosesha Serikali mapato kutokana na uchapishaji wa stakabadhi mbalimbali bandia, uvamizi wa mawasiliano ya Serikali uchapishaji wa vyeti vya usajili wa makampuni, na uchapishaji bandia wa vyeti vya elimu ambavyo hupelekea mtu kuajiriwa kwa kazi ambayo hana ujuzi nayo.

Akizungumzia hatua ambao zinaweza kuchukuliwa dhidi ya wachapishaji wa nyaraka bandia, Chibogoyo alisema kuwa ni pamoja na kutaifisha mitambo ya wahusika.

Akizungumza suala hilo hivi karibuni katika kipindi cha “Tujikumbushe”, Chibogoyo alisema kuwa makosa ya uhalifu wa nyaraka bandia yanaangukia katika sheria za ushahidi, sheria ya makosa ya jinai, sheria ya usalama wa Taifa ya mwaka 1970, pamoja na sheria ya nembo na alama za Taifa.

Mpiga Chapa huyo Mkuu wa Serikali alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kupambana na vita hii kwa kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi ili kutokomeza janga hilo.

“Tunawaomba wananchi tuwe na mshikamano katika kufichua janga hili la uchapishaji holela na bandia kwani ni janga la kitaifa, linagusa maslahi ya nchi na wananchi, nalifananisha na ujambazi wa hali ya juu” alisisitiza Chibogoyo.

Baadhi ya nyaraka ambazo zimekuwa zikighushiwa mara kwa mara ni pamoja na vyeti vya elimu katika ngazi mbalimbali, risiti za serikali, vyeti vya kuzaliwa na ndoa, kadi za magari na pikipiki, mihuri na nembo ya Taifa.

No comments:

Post a Comment