Sunday, March 26, 2017

SERIKALI KUJENGA MELI YA KISASA ZIWA VICTORIA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akimsikiliza Meneja wa Mamlaka ya Bandari Kanda ya Ziwa, Bw. Abel Moyo, alipokagua gati ya Bandari ya Bukoba, mkoani humo jana.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa mmoja wa Afisa Fedha kutoka Mamlaka ya Bandari (TPA), katika Bandari ya Bukoba alipokagua utendaji wa bandari hiyo na kubaini utaratibu mbovu wa ukusanyaji mapato.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiongea na mafundi wanaofanya ukarabati katika bandari ya Bukoba, alipokagua utendaji wa bandari hiyo Mkoani Kagera.
Baadhi ya Watumishi wanaofanya kazi katika taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mkoani Kagera, wakimsikiliza Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani), alipooongea nao mkoani humo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mkoani Kagera, mara baada ya kuongea nao na kuwaeleza mikakati mbalimbali ya WIzara hiyo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

………………

Serikali imewatoa wasiwasi wakazi na wafanyabishara wa Kanda ya Ziwa Victoria kuwa iko katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za ujenzi wa meli mpya kubwa na ya kisasa ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua mizigo tani 300, magari 25 na madaraja matatu kwa ajili ya sehemu ya kukaa abiria. 

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua bandari ya Bukoba, mkoani Kagera, Waziri Profesa Mbarawa amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo umechelewa kutokana na kukosa sifa kwa Makandarasi wawili waliojitokeza mwanzoni kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa ujenzi.

“Nataka kujenga meli ya kisasa ili kuweza kufupisha safari kutoka masaa 10 hadi matano kutoka Bukoba hadi Mwanza na hivyo kufanya usafiri wa majini kuwa wa kuaminika na salama”, amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, Waziri Mbarawa amefafanua kuwa kutokana na utendaji mbovu wa bandari hiyo anatarajia kuleta wafanyakazi makini kwa ajili ya kupitia taaria za kifedha za utoaji na usafirishwaji wa mizigo bandarini hapo.

Naye, Meneja wa Mamlaka ya Bandari Kanda ya Ziwa, Bw. Abel Moyo ameiomba Serikali kufanya ukarabati wa Meli nchini hasa zilizopo Kanda ya Ziwa ili kuweza kuondoa adha wanazozipata wakazi wa mikoa hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua Shirika la Posta mkoani humo na kuahidi kupeleka wakaguzi wa ndani kwa ajili ya kukagua na kujiridhisha juu ya mapato na matumizi ili kubaini ubadhilifu unaofanywa na watendaji wa Posta.

“Tunataka Posta iwe safi na kupunguza changamoto zinazoikabili kwani ni Shirika kubwa na lenye Rasilimali nyingi ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuinua mapato ya Shirika hilo”, amesisitiza Waziri Mbarawa.

Akiwa katika ofisi za Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoani humo, Waziri Prof. Mbarawa ameuagiza Wakala huo kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa katika utengenezaji wa magari yanayokuja kupata huduma katika karakana yao.

Kwa upande wake, Meneja wa TEMESA, Eng, Zephrine Bahyona amemuomba Waziri kusaidia kusisitiza Taasisi za Serikali kupeleka magari yao kwenye karakana zao na kulipa madeni kwa wakati ili kupunguzia Wakala huo mzigo wa madeni kutoka katika taasisi hizo.

Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi wilayani Bukoba, mkoani Kagera ambapo ametembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara yake.

No comments:

Post a Comment