Wednesday, March 29, 2017

Profesa Muhongo: Wananchi lipieni umeme ofisi za Tanesco pekee

Na Veronica Simba – Singida
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wananchi wote, hususan wanaounganishiwa huduma ya umeme vijijini, kufanya malipo husika katika Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) peke yake na siyo kwa mtu mwingine yeyote.
Aliyasema hayo hivi karibuni kijijini Mkwese, Wilaya ya Manyoni wakati akizindua Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) katika Mkoa wa Singida.
Profesa Muhongo alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakitapeliwa na watu mbalimbali kwa kuombwa rushwa ili waunganishiwe umeme au kulipishwa gharama zaidi ya zile zinazostahili, na baada ya kufuatilia, imebainika kuwa wanaofanya utapeli ni watu wasiohusika kabisa na uunganishaji umeme.

Ili kuepuka utapeli huo, Waziri Muhongo amewataka wananchi kufahamu taratibu zinazopaswa kufuatwa wakati wa kuunganishiwa umeme ikiwa ni pamoja na kujua kiasi wanachopaswa kulipia na ni nani wa kumlipa.
Aidha, aliitaka Tanesco kuhakikisha inaendelea na zoezi la kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zote wanazotoa ili wananchi wawe na uelewa wa kutosha na hivyo kuepuka kutapeliwa.
Alisema kuwa, baadhi ya wananchi wanadhani kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ndiyo wenye jukumu la kuchukua malipo kutoka kwa wananchi wanaounganishiwa umeme vijijini.
“Anayepokea malipo yote ya umeme ni Tanesco. Siyo REA wala Wizara. Wananchi mjue hilo. Mwingine yeyote akidai malipo ya umeme, kataeni,” alisisitiza.
Waziri Muhongo aliwataka Wakuu wa Wilaya mbalimbali kuhakikisha wanamkamata na kumweka ndani mtu yeyote anayepita katika maeneo yao na kudai malipo ya umeme kutoka kwa wananchi wakati siyo Ofisa wa Tanesco.
“Mambo ya malipo yote yanafanywa Tanesco. Wala huyu Mkandarasi hakusanyi fedha. Kama ataomba fedha za kuunganishia watu umeme au za nguzo, huo ni wizi na utapeli. Lazima mumshtaki.”
Akielezea kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Profesa Muhongo alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inaundoa umaskini wa wananchi kwa kuwapatia huduma muhimu ikiwemo umeme.
“Injini mojawapo nzuri na muhimu ya kuondoa umaskini wetu ni kuhakikisha tunakuwa na umeme wa uhakika, unaotabirika na wa bei nafuu.”
Alisema, Serikali inatambua kuwa wananchi walio wengi wanaishi vijijini ndiyo maana Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo inaishia mwezi wa sita mwaka huu, fedha zake nyingi zilipelekwa kwenye miradi hususan ya umeme vijijini.
Profesa Muhongo alisema kuwa, ili kuwapunguzia wananchi gharama ya kufuata huduma ya kuunganishiwa umeme kwenye Ofisi za Tanesco ambazo ziko mbali, Serikali imeagiza maafisa wa shirika hilo kutangaza tarehe watakapofika kugawa fomu za kujiandikisha pamoja na vituo vitakavyotumika kufanyia malipo.
Alitoa rai kwa Serikali za Vijiji kutoa ushirikiano kwa Tanesco, ikiwezekana kuwapatia chumba au Ofisi ya kutolea huduma kwa siku watakazopanga kutoa huduma katika vijiji husika.
Waziri Muhongo alieleza kuwa, kwa Mkoa wa Singida, Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu utatekelezwa kwa vipindi viwili tofauti ambapo sehemu ya kwanza itahusisha upelekaji umeme katika vijiji 185 kwa gharama ya shilingi bilioni 47.36. Aliongeza kuwa utekelezaji wa sehemu hiyo ya kwanza umeanza mwezi Februari mwka huu na unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 2019.
Alimtaja Mkandarasi Nakuroi Investment Co. Ltd ambaye alimtambulisha pia kwa wananchi na kumkabidhi kwa viongozi wa Serikali na Wabunge wa Singida, kuwa ni mmoja wa makandarasi watakaoshiriki katika utekelezaji wa Mradi husika katika Mkoa huo.
Aidha, Profesa Muhongo alieleza kuwa, sehemu ya pili ya mradi huo mkoani Singida, itaanza kutekelezwa baada ya sehemu ya kwanza kukamilika mwaka 2019 ambapo vijiji 82 vitapatiwa umeme na hivyo kufikisha umeme katika vijiji vyote vya Mkoa wa Singida ifikapo Mwaka 2021.
Uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa Mkoa wa Singida ulihudhuriwa na wananchi, viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na baadhi ya wafadhili wa Mradi husika ambao ni Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Katarina Rangnitly na Balozi wa Norway nchini, Hamme Hanie Kaarstad.

No comments:

Post a Comment