Wednesday, March 29, 2017

MABALOZI WA SWEDEN, NORWAY WAPONGEZA MIRADI YA REA




Ø Waahidi kuendelea kusaidia sekta ya nishati nchini

Na Veronica Simba – Singida

Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hamme-Hanie Kaarstad na Balozi Katarina Rangnitly anayewakilisha Sweden hapa nchini, wameipongeza Serikali kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa miradi ya umeme vijijini, hivyo wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano hususan katika sekta ya nishati.

Wakizungumza hivi karibuni, kwa nyakati tofauti, katika uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kwa Mkoa wa Singida, Mabalozi hao walisema Serikali za nchi zao zinafurahi kuona jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha wananchi, hususan wa vijijini wanapata umeme wa uhakika na wa bei nafuu.

Akizungumzia kuhusu Mradi wa REA III mkoani Singida, Balozi Kaarstad, mbali na kumshukuru Rais John Pombe Magufuli, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo pamoja na watendaji wengine wa Wizara kwa kuwezesha kutekelezwa kwa miradi husika ya umeme vijijini, alisema kuwa ni matarajio yake kwamba Mradi utawezesha maisha ya wananchi wa Singida kuwa mazuri zaidi.

Aidha, alisema kuwa anaamini Mradi huo utaleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wanawake wa Mkoa huo.

“Mradi huu utaleta mabadiliko kimaisha kwa watu wote lakini zaidi kwa maisha ya wanawake.”

Akifafanua zaidi, Balozi Kaarstad alisema kuwa, matumizi ya umeme katika kuwezesha miradi ya maji, yatawasaidia wanawake kupata muda wa kutekeleza majukumu mengine ya kiuchumi.

Alisema, kwa muda ambao utaokolewa kwa wanawake kuacha kwenda kutafuta maji mbali, utasaidia wasichana kupata muda wa kujisomea nyumbani baada ya muda wa masomo, hivyo kufanya vizuri katika masomo yao.

Aliongeza kuwa, matumizi ya taa za mitaani, ambazo zitatoa mwanga, zitawezesha wanawake kutembea bila hofu hata nyakati za usiku.

Vilevile, alisema kuwa, kupatikana kwa umeme kutawezesha siyo wanawake tu bali jamii nzima kupata mafanikio katika maisha yao.

Halkadhalika, Balozi Kaarstad alieleza kuwa, matumizi ya umeme katika viwanda vidogo vidogo, yataongeza thamani ya mazao pamoja na kuzalisha kazi mbalimbali kwa wananchi hivyo kuwezesha nchi kukua kiuchumi.

“Katika nchi yangu ya Norway, uzalishaji wa nishati kutokana na maporomoko ya maji ulikuwa ni msingi mkubwa wa kupatikana kwa maendeleo. Tumeshuhudia maendeleo makubwa yanayobadilisha maisha ya watu kutokana na umeme. Ndiyo maana ninafurahi kushuhudia uzinduzi wa mradi huu wa umeme kwani najua hata hapa Singida, tunaweza kutumia nishati kupata maendeleo hayo.”

Alisema kuwa, Norway iko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika jitihada za kuiwezesha itoke katika kundi la nchi za Ulimwengu wa Tatu kwenda kundi la nchi za Ulimwengu wa Pili.

Balozi huyo wa Norway aliwashauri wananchi kuwa umeme watakaounganishiwa utumike katika kuendeleza jamii zao na kwamba anatarajia akirudi tena Singida atakuta maendeleo na mabadiliko makubwa kiuchumi.

Kwa upande wake, Balozi Rangnitly alisema kuwa, Sweden imekuwa mshirika wa Tanzania kuanzia miaka ya 1960 na kwamba kwa muda wote huo nchi yake imekuwa ikiunga mkono sekta ya nishati.

“Hii inajumuisha hatua mbalimbali, kuanzia kwenye uzalishaji wa umeme mathalani Mtambo wa kuzalisha umeme wa Hale pamoja na usafirishaji na usambazaji wa umeme,” alifafanua.

Alisema kuwa, upatikanaji wa umeme wa uhakika, utabadili maisha ya wananchi na kwamba utawezesha wanafunzi kufanya kazi zao za shuleni wakati wa usiku. 

Balozi Rangnitly alitolea mfano wa maendeleo ambayo nchi yake ilipata baada ya kuunganishwa na nchi nyingine za jirani ikiwemo Ujerumani kwa kuuziana umeme kati ya nchi na nchi.

“Kwa kawaida bei za umeme hushuka na pia kunakuwa na umeme wa uhakika. Itakuwa hivyo hata hapa Tanzania, kupitia Mradi wa Umeme wa Backbone.”

Aidha, Balozi huyo wa Sweden alitilia mkazo umuhimu wa matumizi ya nishati jadidifu ambapo alisema uwepo wa jua la kutosha Tanzania, unaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha umeme wa jua.

Hata hivyo alitanabaisha kuwa, upatikanaji wa umeme pekee hautoshi katika kuleta maendeleo isipokuwa, umeme ukipatikana kunatakiwa kuwepo na mazingira mazuri na wezeshi ya kibiashara pamoja na upatikanaji wa mitaji.

“Sweden itashirikiana na Tanzania katika Nyanja hizo pia. Hata hivyo, umeme ni msingi wa mambo hayo yote,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri Muhongo, ambaye alikuwa ni Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo, aliwashukuru wafadhili wote wanaochangia katika miradi ya umeme nchini, hususan Mabalozi hao wawili waliohudhuria hafla ya uzinduzi.

Waziri Muhongo alisema kuwa, wafadhili hao wameshawishika kuendelea kufadhili miradi ya umeme nchini kutokana na Tanzania kuwa nchi inayoheshimika kimataifa, yenye uongozi safi, rasilimali za kutosha na yenye wananchi wanaojituma.

Awali, akitoa maelezo ya utangulizi katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alisema kuwa wafadhili mbalimbali wamekuwa wakichangia fedha katika miradi ya umeme vijijini na kwamba jumla ya fedha zilizotolewa na wafadhili katika Mradi wa Umeme wa Backbone kwa ajili ya kuunganishia umeme vijiji vilivyopitiwa na Mradi huo ni Euro milioni 28 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 60.

Alisema kuwa, fedha hizo ni kwa ajili ya kugharamia usambazaji wa umeme katika vijiji 121 katika Mikoa mitano (5) ambayo imepitiwa na Mradi wa Usafirishaji wa Umeme mkubwa wa kilovolti 400. Mikoa hiyo ni Iringa, Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akiwatambulisha Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hamme-Hanie Kaarstad (katukati) na Balozi wa Sweden nchini, Katarina Rangnitly (kulia); kwa wananchi (hawapo pichani) waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kwa Mkoa wa Singida.

 Kamishna wa Nishati na Masuala ya Mafuta, Mhandisi Innocent Luoga (mwenye suti nyeusi) na Afisa kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) (wa pili kutoka kushoto), wakiwatafsiria kwa lugha ya kiingereza wageni walioambatana na Mabalozi wa Sweden na Norway katika hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kwa Mkoa wa Singida.




Sehemu ya umati wa wananchi waliohudhuria katika hafla ya  uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kwa Mkoa wa Singida.

No comments:

Post a Comment