Thursday, March 30, 2017

Hali ya Mzee Haji Gora Haji mtunzi wa ‘Mpewa Hapokonyeki’ ilivyo sasa, hakika inabidi Wanaonufaika na kazi zake wamtunze angali hai


Na Salum Vuai, 
MAELEZO - Zanzibar

JUMATATU ya tarehe 27 Machi, 2017, niliamua kuakhirisha mambo yangu mengine yaliyokuwemo kwenye ratiba yangu na kuamua kufunga safari hadi mtaa wa Chumbuni, Wilaya ya Mjini Unguja.

Nia yangu ilikuwa kwenda kumjulia hali msanii mkongwe wa Zanzibar, Mzee Haji Gora Haji, ambaye kwa miezi kadhaa sasa nyendo zake zimekatika kutokana na kusumbuliwa na maradhi.
Gwiji huyu wa sanaa mbalimbali ikiwemo ushairi, uandishi wa vitabu vya hadithi fupi, tenzi na mashairi ya nyimbo, ni miongoni mwa watu muhimu katika tasnia ya usanii hapa nchini.
Kwangu mimi, na ninaamini kwa wengine wanaopenda sanaa, Mzee Gora aliyezaliwa mwaka 1933 kijijini Tumbatu, ni mwalimu na mlezi katika kuwafinyanga washairi chipukizi na wa makamu ambao bado wanaendelea kujifunza kwa kuamini kwamba sanaa ni utamaduni endelevu unaokuja kivyengine kadiri siku na mambo yanavyobadilika.
Ingawa nilikuwa nikipanga kumtembelea siku nyengine isiyokuwa tarehe 27 Machi niliyoitaja awali, lakini nililazimika kubadili mpango huo na kuamua kuwahisha ziara yangu hiyo kutokana na jambo maalumu liliougusa mtima wangu usiku wa Machi 26, mwaka huu.
Ni jambo gani hilo? Endelea kusoma makala haya mstari kwa mstari, neno kwa neno, herufi kwa herufi ili ulijue.
Niliraghibika kuharakisha kwenda kumuona baada ya usiku huo wa Machi 26, 2017, kuusikia wimbo wake mashuhuri alioutunga miaka mingi kiasi, ukiimbwa katika tamasha la kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Tamasha hilo lililofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazimmoja mjini Zanzibar, lilikuwa maalumu kwa ajili ya kumpongeza Dk. Shein kwa kutimiza mwaka mmoja tokea alipoapishwa kuendelea na kipindi cha pili cha uongozi wake visiwani humu Machi 24, 2016.
Wakati nikifuatilia matangazo ya moja kwa moja ya tamasha hilo kupitia redio ya Shirika la Utangazaji Zanzibar, masikio yangu, na bila shaka mtima wangu pia, vikavutwa na sauti ya mshereheshaji wa kikundi cha Culture Musical Club, Iddi Suwedi, alipotangaza kuimbwa kwa wimbo uitwao, ‘Mpewa Hapokenyeki’.
Hapo ndipo iliponijia picha ya Mzee Haji Gora, ambaye kwa sasa ni mgonjwa na hana tena safari zilizokuwa zikimtoa ndani ya nyumba yake kwenda kwenye harakati zake za maisha.
Baada ya kufika njia ya Daraja bovu karibu na kituo cha afya maarufu Kundi, nikaegesha chombo changu cha usafiri, na nikaanza kukatisha vichochoro kwa miguu hadi nikafika nyumbani kwa mkongwe huyu wa sanaa.
Kwanza nilipokelewa na mjukuu wake wa kiume aliyekuwa akicheza mpira na watoto wenzake, na akanishindikiza hadi nyumbani kwao takriban mita 40 kutoka nilipomkuta.
Wakati tukiwa njiani na mtoto huyo, alinidokezea kuwa babu yake yupo lakini amefichwa chumbani, kauli iliyonipa mshtuko nikidhani labda amezidiwa na maradhi na nikapata wasiwasi kuwa huenda sitaruhusiwa kumuona.
Lakini nilipofika nilishusha pumzi kwani binti yake mmoja anayetarajia kuanza chuo wiki ijayo, alifungua mlango na kumjulisha juu ya ugeni wangu.
Nilishukuru kumuona Mzee Gora akiwa ametoka ndani mwenyewe huku akivaa kanzu kuja kunilaki ukumbini na hapo tukasalimiana vizuri tukiulizana habari za  harakati na mambo mengine.
Binti yake akiwa pembeni, Mzee Gora alianza kulalamika akisema, “Mimi sitaki kupigana na wala sipendi kupigana”.
Nilipomuuliza alikuwa na maana gani kwa kauli hiyo, akasema akiwalaumu watoto wake kwa kitendo cha kumfungia ndani, huku akimtaka binti yake amuite daktari kwa ajili ya kumpima ili awathibitishie kwamba ana akili zake na hakuna haja ya kumzuia kutoka nje.
Lakini ghafla, katikati ya mazungumzo yetu, Mzee Gora akanitaka ninyamaze akiniambia nisikilize huku naye akiwa ametulia kimyaa kama anayesikiliza sauti itokayo mbali.
Sijui alikuwa amesikia kitu gani ambacho mimi pamoja na kutega sikio vizuri sikuweza kunasa sauti yoyote zaidi ya zile za watoto waliokuwa nje ya nyumba wakicheza.
Hapo ndipo nilipobaini, na kwa kusimuliwa na binti yake, kwamba Bwana Haji Gora, pamoja na kuambiwa alipata homa, lakini pia ameanza kupoteza uwezo wa kufikiri na kurudisha kumbukumbu.
Masikini, Mzee huyu aliyetumia zaidi ya nusu ya umri wake akifanya kazi za kiuandishi bila ya kuwa na elimu kubwa ya skuli, sasa umri unamrejesha katika utoto kiasi cha kuhitaji kuwekwa ndani kwa wasiwasi wa kupotea.
Ndio, lazima wawe na wasiwasi kwani nilipokuwa kwake, nilimshuhudia akiinuka kitini na kwenda kusimama mlango wa nje huku akinadi kuwaita watu asiowaona kwa majina ambayo hata mimi sikuweza kuyasikia vyema wala kuyahafahamu.
Na hata nilipoaga kwa ajili ya kuondoka, Mzee Gora alikuwa wa kwanza na kama aliyeinuliwa ghafla kitini alipokuwa amekaa na kutoka nje haraka huku binti yake na mama mmoja aliyekuwa akisuka ukili, wakijaribu kumzuia lakini walipomuona hashikiki wakamuachia.
Nilipotoka nikauliza amepita njia gani ili nimfuate, lakini nikaambiwa ameingia nyumba jirani na yake.  
Sasa Mzee Gora anahitaji matunzo na uangalizi wa hali ya juu, na hili si jambo la kuachiwa familia yake pekee, ikifanya kazi ya kumchunga asipotee mbele ya macho yao.
Kwa namna Mzee huyu alivyoitangaza nchi hii kwa kutumia fasihi andishi na simulizi, na kuandika vitabu mbalimbali vikiwemo vya watoto vinavyofundisha akhlaki njema, mila na maadili ya Kizanzibari kidini, si mtu wa kuachwa augue bila ya msaada maalumu angalau kuthamini juhudi zake za kuinua utajo wa Zanzibar nje ya mipaka yake.
Nikirudi nyuma katika wimbo ‘Mpewa Hapokonyeki’, ni ukweli usio shaka kwamba ni miongoni mwa nyimbo zake zinazopendwa sana na unaoendelea kuishi ingawa miaka mingi imepita tangu alipoutunga.
Ingawa Mzee Gora alitunga wimbo huo kwa mnasaba wa wanajamii walivyo na sio kwa mtazamo wa kisiasa, lakini ni wazi umewakuna wengi ambao wameamua kuunasibisha katika mambo yao na hivyo kila wanapousikia roho zao huwa kwatu.
Na ni ukweli usiofichika kwamba uongozi wa Culture Musical Club unajua fika kwamba wimbo huo hauwezi kuachwa bila kupigwa kila wanapokuwa wanatumbuiza kwenye hafla mbalimbali za ki-nchi.
Ni wimbo unaowavutia wengi kutokana na ujumbe uliobeba na pia muziki na ufundi wa wasanii wa Culture katika kucharaza vinanda.
Sina hakika kama Mzee Gora ameusajili wimbo huu katika Idara ya Hakimiliki, lakini hata kama amefanya hivyo, anastahiki kufaidika na tunza zinazopatikana kila pale unapopigwa kwenye hadhara, ikizingatiwa hali yake ya sasa.
Na kwa kuwa wanaoupiga pia hawafanyi hivyo bure bileshi kwa maana wanalipwa chochote, ni vyema wanapogawana mapato wamkumbuke mtunzi wa wimbo huo angalau kwa ‘juisi’, japo wapo watakaohoji vipi kuhusu nyimbo za watunzi wengine zinazotumika!
Kwa namna ninavyoifahamu Culture, ninaamini nyimbo zao nyingi zinatungwa na wasanii wa ndani yaani wanamuziki wenyewe kwa hivyo bila shaka wananufaika huko.
Ninapousikia wimbo huo ukiimbwa ukumbini, mawazo yangu huwa yanasafiri hadi nyumbani kwa mtunzi wake, ambaye bila kujua masikini, nguvu zake zinatumika kuwafurahisha watu huku mwenyewe akiwa amelala Chumbuni akiugua.
Uko wapi umoja wa wasanii, kiko wapi Chama cha Washairi, Kamisheni ya Utamaduni na Baraza linalohusika na sanaa Zanzibar, mko wapi mnaonufaika kwa namna moja au nyengine na kazi za msanii Mzee Gora katika wakati huu anaokuhitajini sana.
Kwa muktadha huo, niwasifu pia Chama cha Kiswahili Zanzibar (CHAKIZA) kwa kujipangia ziara za kumtembelea ili kumfariji mzee na mwalimu wetu huyu. 
Huu ndio wakati wa kumuonesha upendo na kumthamini, chambilecho mwimbaji wa Mombasa Bi. Zuhra Saleh aliyeimba, “Mpende bado yuko hai, Pendo alithamini. Ukimpenda yuko kaburini umelitupa pendo lako hewani”.
Ninamuomba Mwenyezi Mungu amponye na ampe umri mrefu Mzee Gora, lakini mtu aliyesaidia sana harakati za kukienzi na kukisambaza Kiswahili kwa vitendo akitunga vitabu mbalimbali likiwemo Kamusi la Kitumbatu, ni mtu wa kutunzwa sasa badala ya kusubiri afe ndipo kila mtu amsifu kwa maneno mengi ambayo wakati huo hayatakuwa na faida yoyote kwake.
Mapenzi yetu kwake tuyaoneshe sasa, na asiwe mwenzetu wakati wa uzima tu, na hili litampa faraja yeye na familia yake wakitambua jamii na nchi zinathamini mchango wake.
Kabla sijahitimisha makala haya, napenda kumshukuru na kumpongeza kwa dhati, mwandishi mwenzangu Ali Saleh ‘Alberto’ kwa kuwa wa kwanza hapa Zanzibar na Tanzania kwa jumla, kuandika kitabu kuhusu maisha ya Mzee Gora ambacho alikizindua miezi kadhaa iliyopita. 
Mtu akikisoma kitabu hicho alichokipa jina la ‘Maisha ya Haji Gora’, anapelekwa mbali mno tangu enzi za utoto wa msanii huyo na si ajabu akajikuta anajiweka pahala pake au kama anayemuona kwa ufundi wa lugha yenye kuonesha picha uliotumika katika uandishi wake.
Angalau Ali ameonesha njia, vipi kumuenzi mtu akiwa hai. Tufuate nyayo zake katika kumsaidia gwiji huyu ambaye vitabu vyake vimetapakaa Afrika Mashariki nzima na kwengineko Kiswahili kinakotumika.

Tel: 0777 865050
E-mail: salumss@yahoo.co.uk
          

   

No comments:

Post a Comment