Monday, February 27, 2017

UTOAJI TAARIFA ZA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMMA UNAVYOSAIDIA KUPAMBANA NA RUSHWA

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Serikali imeweka kipaumbele kikubwa katika  ujenzi wa miundombinu ya Umma  kwani ni muhimu kuwa na miundombinu mizuri na bora ili kutoa huduma bora na kurahisisha ufanyaji kazi hivyo kuharakisha maendeleo ya nchi katika nyanja zote muhimu zikiwemo za biashara, utalii na mawasiliano.

Matumizi makubwa ya fedha za Serikali yanatumika katika ujenzi wa miundombinu ya Umma ambapo matumizi hayo yanahusisha karibu asilimia 53 ya Bajeti nzima ya nchi.

Miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Umma inayoelezewa hapa ni ile ambayo inajengwa kwa fedha za Serikali kwa ajili ya matumizi ya wananchi wote ikiwemo ya barabara, hospitali na vituo vya afya,shule na vyuo,nyumba za kuishi pamoja na ofisi mbalimbali. 

Ingawa Serikali inajitahidi kuhakikisha nchi inakuwa na miundombinu bora itakayochochea maendeleo, lakini jitihada hizo zimekuwa zikikwamishwa na changamoto mbalimbali zinazojitokeza pindi mradi husika unavyoanza kwani wahusika hawatumii fedha kama zilivyopangwa na badala yake wanafanya kwa makadirio ya chini na kufanya ujenzi kutokuwa imara.

Hali hiyo inasababisha Serikali kupata hasara kwa kupoteza fedha nyingi na kuambulia kubaki na majengo yasiyo na viwango ambayo mwisho wake hushindwa kutumika na kuilazimu Serikali kuanza upya ujenzi husika. 

Kwa kuwa Serikali hii ni sikivu na imejipanga kuhakikisha nchi inafika katika uchumi wa kati basi mambo hayo hayana nafasi na hayawezi kutokea tena katika nchi hii watu kuachiwa huru kutumia vibaya fedha za Umma zinazotolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. 

Kwa kuhakikisha hilo,Serikali kupitia Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC) chini ya Mkakati wa Kukuza Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Ujenzi Tanzania (CoST-Tanzania) imejipanga kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta hiyo ili kuondokana na rushwa pamoja na ubadhilifu wowote wa fedha za Umma zinazotolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo.

Mkakati huo unalengo la kupambana na rushwa, usimamizi mbaya katika ujenzi pamoja na changamoto zingine zinazopelekea ubadhilifu wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miundombinu ya Umma kwa kukusanya taarifa za miradi hiyo ya ujenzi ili  kuhakikisha kama thamani ya miundombinu iliyojengwa inalingana na thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi husika. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,(Ujenzi), Mha. Joseph Nyamuhanga alikaririwa akisema kuwa “Sekta ya Ujenzi ni sekta moja wapo inayoonekana kukithiri kwa rushwa duniani kwa sababu takribani asilimia 10 hadi 30 ya Bajeti yake inapotea kwa njia ya rushwa na usimamizi mbaya hivyo ili kuondoa dhima hii ni lazima kukusanya na kutoa taarifa kwa wananchi juu ya ujenzi wa miundombinu hiyo”.

Mha. Nyamuhanga aliongeza kuwa ni muhimu CoST-Tanzania ikapewa hadhi ya kujitegemea na kuwa na madaraka yake kwani ni kitengo ambacho ni muhimu na kinafanya kazi kubwa ya kuchochea uwepo wa uwazi na uwajibikaji katika miradi ya ujenzi.

Akifungua mkutano wa wadau wa ujenzi kutoka nchi mbalimbali uliofanyika Jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchukuzi), Mha. Leonard Chamuriho alisema rushwa inazungumzwa sana katika suala la ujenzi wa miundombinu ya umma hivyo huu ni wakati wa kuweka wazi taarifa za ujenzi wa miundombinu hiyo ili wananchi waelewe kinachoendelea katika miradi inayotumia fedha zao.

Aliongeza kuwa kufanya hivyo kutaisaidia Serikali kupambana na rushwa na hivyo kufuta kabisa taswira ya rushwa katika miradi hiyo kwani msimamo wa Serikali ni kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa.

Maendeleo ya nchi yanachangiwa na wananchi wenyewe kwa njia ya ukusanyaji wa kodi na ushuru mbalimbali hivyo hata miundombinu ya umma inajengwa kwa kutumia fedha za wananchi zinazopatikana kwa njia ya ukusanyaji mapato.

Hivyo, ili kuifanya Serikali kuwa na taswira nzuri kwa wananchi wao pamoja na kuwafanya wananchi kuiamini Serikali yao ni vizuri kuwapa taarifa juu ya matumizi ya fedha hizo wanazozikusanya.

Kuwapa taarifa wananchi juu ya miradi mbalimbali haswa ya ujenzi wa miundombinu kutaamsha ile hali ya watu kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa sababu watajua matumizi ya fedha wanazozikusanya.

Taarifa hizo pia zitaendeleza uwajibikaji na uwazi katika ujenzi wa miundombinu hiyo hivyo kupunguza vitendo vya rushwa,kujenga miundombinu inayoendana na thamani ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi husika pamoja na kujenga miundo mbinu bora na imara.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema kuwa shughuli inayofanywa na CoST- Tanzania inalenga kuimarisha uwazi katika sekta ya ujenzi kwa kutoa taarifa juu ya ujenzi wa miundombinu ya Umma kitu ambacho kitasaidia kutambua uwezo, akiba pamoja na ufanisi wa majengo hayo.

"Kazi inayofanywa na CoST- Tanzania ni fursa kwa Serikali na Umma kwa ujumla kufuatilia jinsi fedha za Umma zinavyotumika katika ujenzi wa miundombinu ambapo ukweli na uwazi wa taarifa zinazokusanywa zitasaidia katika kupunguza rushwa na kuboresha usimamizi wa miundombinu hiyo, " alisema Waziri Kairuki.

Nae Mwenyekiti wa CoST-Tanzania, Mha. Kazungu Magili alieleza kuwa utoaji wa taarifa hizo kwa Umma kuhusiana na miradi ya ujenzi ya Umma itaruhusu umma kujua hali ya miradi mbalimbali hivyo kuifanya Serikali kuwa na sifa nzuri mbele ya wananchi.

CoST-Tanzania imejipanga kufanya tathmini ya miradi ya ujenzi isiyopungua kumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja, majengo yaliyojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) hasa ujenzi mpya wa hosteli  za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia majengo yanayojengwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF ) pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Ni muhimu kwa Serikali kupitia miradi yote iliyojengwa na inayoendelea kujengwa kwa kutumia fedha za Umma ili kugundua thamani halisi ya majengo hayo na kutoa taarifa kwa wananchi.

Jambo hili pia litasaidia vyombo husika vya kisheria kuwachukulia hatua watu wote walioshiriki kutumia vibaya fedha za wananchi kwa kujenga miundombinu iliyo chini ya kiwango au isiyoendana na thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi husika.

No comments:

Post a Comment