Monday, February 27, 2017

TAASISI YA SEKTA BINAFSI YAJIPANGA KUWAJENGEA UWEZO WAHITIMU WA VYUO VIKUU NCHINI

Na Jovina Bujulu MAELEZO Dar es Salaam

TAASISI ya sekta binafsi nchini (TPSF) imetoa wito kwa wahitimu na vijana waliopo vyuoni kuchangamkia fursa ya mpango maalum uliobuniwa baina yake na Serikali ambao umekusudia kuwajengea ujuzi kabla ya kuajiriwa ili waweze kufanya kazi kwa weledi.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye wakati alipokuwa akichangia mada kuhusu wahitimu wa vyuo vikuu kushindwa kuonyesha ujuzi baada ya kuajiriwa.

“Upo upungufu mkubwa wa mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wengi wanaomaliza vyuo vikuu nchini na imedhihirika kuwa wahitimu hao hushindwa kufanya kazi kwa weledi wanapokuwa wameajiriwa na sekta mbali mbali.

Alisema kuwa mpango huo maalum umeanzishwa kwa lengo la kuwatayarisha wahitimu wa vyuo kupata mafunzo ya muda mfupi ili kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo pindi wanapoajiriwa au kutaka kujiajiri.

Simbeye alisema Mpango huo pia umekusudia kuwapunguzia gharama waajiri, hasa wa sekta binafsi kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakitumia pesa nyingi kwa kuwapeleka waajiriwa wapya katika mafunzo ili waweze kumudu kazi zao.

Akifafanua zaidi alisema katika mpango huo waajiriwa wataweza kupata mafunzo mtambuka na gharama zote za mafunzo zinagharimiwa na Serikali.

“Chini ya mpango huu, wahitimu na vijana walioko vyuoni wanatakiwa kujiandikisha kwa hiari, na baada ya mafunzo inakuwa rahisi kwao kupata ajira kupitia katika sekta binafsi au makampuni” aliongeza Bwana Simbeye.

Aidha Bwana Simbeye alisema kuwa mpango huo pia utawawezesha wahitimu kutengeneza mazingira ya kuanzisha biashara nyingi na kupanua biashara zilizopo ili waweze kupata fursa nyingi za kuajiriwa na kujiajiri hasa katika wakati huu ambao nchi inaelekea katika uchumi wa viwanda.

Akizungumzia mpango huo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana, na Walemavu), Anthony Mavunde alisema kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa kila chuo kinajitengenezea mwongozo wake unaomwezesha kila mwanafunzi kupata nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo.

Aidha aliongeza kuwa Serikali itahakikisha kuwa mpango huo unakuwa endelevu na unafanya kazi kama ilivyokusudiwa na kutoa wito kwa sekta binafsi na waajiri kutoa maoni yao ili kuboresha mpango huo.

No comments:

Post a Comment