Friday, February 3, 2017

MAKALA: MAFANIKIO YA KUKABILIANA NA UJANGILI KIMKAKATI YAANZA KUONEKANA



NA HAMZA TEMBA - WMU

"Haiwezekani maliasili yetu ikawa inapotea hovyo hovyo kwasababu ya watu wachache wenye tamaa ya kupata utajiri wa harakaharaka, hakuna wa kumbakiza, awe mkubwa, awe nani, shikeni, wala msijali mtu cheo chake, umri wake, dini yake, kabila lake, umaarufu wake, sheria ni msumeno, watafuteni wote mpaka wakiona tembo wawe wanakimbia wenyewe".

Hiyo ilikua ni kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipofanya ziara ya kushtukiza katika makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii (Mpingo House)  Jijini  Dar es Salaam tarehe 29 Oktoba, 2016 kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa operesheni ya kukabiliana na ujangili inayofanywa na kikosi kazi kilichoundwa na Wizara hiyo.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alishuhudia meno ya tembo 50 yaliyokuwa yamekamatwa katika kipindi cha siku mbili zilizopita Jijini Dar es Salaam, alioneshwa pia gari lililokuwa limebeba meno hayo na watuhumiwa wanane wanaotuhumiwa kujihusisha na mtandao wa biashara haramu ya meno ya tembo.

Rais Magufuli aliwapongeza askari wote waliopo katika kikosi cha kupambana na ujangili pamoja na raia wema wanaotoa ushirikiano katika mapambano hayo na kwamba anatambua kazi nzuri wanayofanya na anawaunga mkono.

Katika hotuba yake ya kwanza ya kulihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, Rais Magufuli alitoa vipaombele kadhaa vya kutekelezwa na wizara zake huku Wizara ya Maliasili na Utalii akiipa majukumu makuu matatu; kupambana na ujangili, kutatua migogoro ya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi na kuongeza mapato ya Serikali.

Wizara hiyo inayoongozwa na Waziri Prof. Jumanne Maghembe; Naibu Waziri, Mhandisi Ramo Makani; Katibu Mkuu, Meja Generali Gaudence Milanzi na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Aloyce Nzuki imejipanga kutekeleza majukumu yake makuu ya uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Kuendeleza Utalii pamoja na vipaombele ilivyoelekezwa.

Mara tu alipoteuliwa kuingoza wizara hiyo, Prof. Maghembe alitangaza vita na majangili na kubainisha kuwa kipaumbele chake kikubwa kitakuwa ni kupambana nao. “Niwaambie majangili sasa wakafanye kazi nyingine ama wakae nyumbani, kiama kinakuja huko”, alisema.

Alisema kuwa atasimamia kwa uhakika maliasili za Watanzania kwa sababu mambo ya maliasili ndiyo eneo alilobobea kwenye usomi wake.
“Tutajitahidi pia kutangaza utalii na kuongeza mapato ya sekta hii kama tulivyofanya kwenye miaka ya 2006 hadi 2008, tuliongeza bei za vitalu na ada kwa mnyama mmoja mmoja anayewindwa,”  alisema Profesa Maghembe siku aliyoapishwa.

Mikakati ya Wizara kukabiliana na ujangili

Ni takribani mwaka mmoja na miezi miwili tangu uongozi wa Serikali ya awamu ya tano uingie madarakani, taarifa iliyotolewa na Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii, inaonyesha kuwa katika kipindi cha mwezi Novemba, 2015 hadi mwezi Oktoba 2016 Wizara hiyo imefanikiwa kuweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ujangili ikiwemo kuanzisha kikosi kazi maalum cha kupambana na ujangili.

Kikosi kazi hicho cha kudhibiti uhalifu wa Misitu na Wanyamapori nchini(Wildlife and Forest Crime Unit),kinasimamiwa na Watendaji wa Sekta ya Wanyamapori kwa ajili ya kukabiliana na majangili katika ngazi za juu za uwezeshaji (Facilitators) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini.

Kikosi hicho kiliundwa mwezi Julai, 2016 na Katika kipindi cha miezi mitatu (Agosti hadi Oktoba, 2016) kimefanikiwa kukamata majangili 107 na kesi 9 ziko mahakamani, upelelezi wa kesi nyingine unaendelea. Nyara mbali mbali, silaha na vifaa vya kufanyia ujangili pia vimekamatwa na kikosi kazi hicho.

Wizara imefanikiwa kuimarisha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambayo ilizinduliwa rasmi mwezi Novemba, 2015 na Rais wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na kuanza majukumu yake rasmi tarehe 1 Julai, 2016.

Mamlaka hii yenye jukumu la kuendeleza shughuli za ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori nchini kwa maeneo yote yaliyopo nje ya Hifadhi za Taifa na Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti ujangili kwenye maeneo hayo.

Mabadiliko ya mfumo wa utendaji kutoka ule wa kiraia kwenda wa Jeshi Usu umenzishwa na Wizara kwa ajili ya kuimarisha nidhamu, ufanisi wa utendaji kazi za uhifadhi pamoja na mapambano dhidi ya ujangili. Katika kipindi hicho mafunzo kadhaa yametolewa kwa watumishi 425 wa TANAPA katika kuelekea mabadiliko hayo.

Watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania pia pia wamepatiwa mafunzo hayo. Lengo ni kutoa mafunzo hayo kwa watumishi wote wa taasisi za uhifadhi nchini zikiwemo za wanyamapori na misitu.

Pamoja na mafunzo hayo, matumizi ya teknolojia ya ndege zisizokuwa na rubani (drones) kwa ajili ya doria na ulinzi wa mipaka na wanyamapori yamepewa kipaombele katika hifadhi mbalimbali za taifa na Pori la Akiba la Selous kama mkakati wa kukabiliana na ujangili.

Mkakati mwingine ulioanzishwa na kuimarishwa ni ukaguzi wa nyara katika viwanja vya ndege na bandari kwa kutumia mbwa maalum wa kunusa ili kutambua nyara na kufuatilia majangili.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa ushirikiano na nchi jirani katika kutatua changamoto za uhifadhi na biashara haramu ya ujangili umeimarishwa. Katika eneo hili Tanzania inashirikiana na nchi ya Msumbiji, Zambia, Uganda na Kenya kukabili ujangili unaovuka mipaka ya nchi hizo.

Ushirikishwaji wa wananchi katika uhifadhi na vita dhidi ya ujangili ni moja ya mkakati uliowekwa na wizara. Elimu ya uhifadhi kwa wananchi  imeendelea kutolewa katika  wilaya 11 na vijiji 57 vinavozunguka Pori la Akiba la Selous, Mapori ya Akiba  ya Lukwika/Lumesule na Msanjesi na eneo la Ardhioevu la Ziwa Natron.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa;

Katika kipindi cha mwezi Novemba, 2015 hadi Oktoba 2016, taarifa ya Idara ya Wanyamapori inaeleza kuwa Sekta ya Wanyamapori imefanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 5,894 kwa makosa mbalimbali ya uvunjaji wa Sheria za Uhifadhi na kuwafungulia mashitaka. Jumla ya kesi 859 zilifunguliwa. Kesi 136 zenye watuhumiwa 248 zilihukumiwa kifungo cha jumla ya miezi 8,295 na kesi 198 zenye watuhumiwa 234 walilipa faini jumla ya shilingi 387,985,063/=.

Imeeleza kuwa silaha 254 za aina mbalimbali zilikamatwa katika kipindi hicho, Nyara za aina mbalimbali zilikamatwa ikiwemo meno ya tembo vipande 848 vyenye uzito wa kilo 2,664.48, nyamapori yenye uzito wa kilo 7,790 za wanyama mbalimbali, meno 8 ya kiboko, magunia 67 ya magamba ya kakakuona, ngozi 16 na mikia 33 ya wanyamapori mbalimbali.

Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa katika kipindi hicho ni watu sita akiwemo mfanyabiashara Yusuf Ally (34) aliyewahi kutajwa na Rais John Magufuli kwa jina maarufu la ‘Mpemba’ kuwa ni kinara wa ujangili, watuhumiwa hao ambao kesi yao bado inaendelea walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya shilingi milioni 785.6.

Mtuhumiwa mwingine maarufu wa ujangili aliyewahi kukamatwa nchini ni mwanamke wa China anayedaiwa kuongoza genge kubwa zaidi la usafirishaji wa pembe za ndovu barani Afrika. Akipewa jina la utani “Ivory Queen”, Yang Feng Glan anadaiwa kusafirisha pembe za ndovu 706 kutoka nchini kwenda Mashariki ya mbali. Glan, 66, anadaiwa kuwa na ukaribu na majangili wa Afrika Mashariki na walanguzi wa China, kesi yake bado ipo mahakamani.

Ujangili waripotiwa kuanza kupungua;

Januari 17 mwaka huu (2017), akizungumza kwenye kikao cha kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii mkoani morogoro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Generali, Gaudence Milanzi alisema ujangili hapa nchini kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba nyara zinazokamatwa kwa sasa ikiwemo meno ya tembo ni za zamani zilizokuwa zikisubiria kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Aliongeza kuwa mizoga ya wanyamapori imepungua ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambapo ni dalili pia ya kupungua kwa ujangili nchini, “mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa inayofanywa na vikosi maalum vya Askari wa wanyamapori vya kudhibiti ujangili kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini”, alisema Milanzi.

Katika hatua nyingine alieleza kuwa kitendo cha Serikali ya China kupiga marufuku biashara ya meno ya tembo nchini humo ni jambo la kupongezwa na kwamba uamuzi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msukumo wa vitendo vya ujangili nchini kwa kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa masoko makubwa ya meno hayo duniani.

Ujangili haukubaliki kwa kuwa unatishia kuathiri faida kubwa inayopatikana kupitia sekta ya utalii ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea uwepo wa wanyamapori katika hifadhi zetu, Sekta hii inachangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na ni sekta inayoongoza kwa miaka mitatu mfululizo kwa kutoa mchango wa asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni nchini.

Ni jukumu la kila Mtanzania kuona umuhimu wa rasilimali hizi na kuunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa Maliasili zetu zinaendelea kuwepo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo, Tanzania bila Ujangili inawezekana, kila mmoja akitimiza wajibu wake.
 Rais Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi alipofanya ziara ya kushtukiza makao makuu ya hiyo (MPINGO HOUSE) jijini Dar es salaam Oktoba 29, 2016. (Picha na Ikulu)

Rais Dkt John Pombe Magufuli akikagua pembe za ndovu 50 zilizokamatwa katika operesheni maalum ya kusaka majangili alipofanya ziara ya kushtukiza makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii (MPINGO HOUSE) jijini Dar es salaam Oktoba 29, 2016. (Picha na Ikulu)

No comments:

Post a Comment